Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

 

7. SURAT AL- A'RAAF

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeteremka Makka isipo kuwa Aya nane, nazo ni 163 mpaka 170. Na idadi za Aya zake ni 206.
Mwanzo wa Sura hii ni kuendeleza yaliyo kuja mwisho wa Sura ya Al-Ana'm, na baada ya hayo imeingia kueleza khulka ya kibinaadamu. Ikataja kisa cha Adam na Hawa, na walivyo toka kwenye Bustani kwa kutiwa wasiwasi na Shet'ani, na ikaeleza huo wasiwasi unaoendelea kwa watu katika mavazi na chakula. Kisha Aya za Sura hii tukufu, kama sura nyengine za Qur'ani zikaingia kutupia jicho kwenye mbingu na ardhi na viliomo ndani yao, na kuzingatia uumbaji wake wa ajabu.
Kadhaalika Sura hii imeeleza hadithi za Manabii kama Nuhu na Hud na kaumu yake kina A'ad. Kisha hadithi ya Saleh na kaumu yake, Thamud, walio sifika kwa nguvu zao na wakapewa utajiri; na hadithi ya Lut' na kaumu yake, na ikataja maovu waliyo kuwa wakiyafanya; na hadithi ya Shua'ib na watu wa Madyana. Na baada ya hadithi hizo za kweli Sura imeeleza mafunzo na mazingatio yaliyomo. Naye Subhanahu wa Ta'ala amefuatilizia hayo kwa kisa cha Musa na yaliyo tokea katika mambo ya Firauni.
Na Sura ikakhitimishia kwa kumathilisha nini hali ya mwenye kupewa hidaya khalafu akabanduka kwenye uwongofu akaingia kwenye upotovu kwa kumfwata Shet'ani, na Sura pia ikamalizia kueleza Wito wa kuendea Haki alio kuja nao Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake.
 

 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. ALIF LAM MYM 'SAAD Maelezo

2. Kitabu kilicho teremshwa kwako - basi isiwe dhiki kifuani kwako kwa ajili yake, upate kuonya kwacho, na kiwe ni ukumbusho kwa Waumini. Maelezo

3. Fuateni mliyo teremshiwa kutoka kwa Mola Mlezi wenu, wala msifuate rafiki au walinzi wengine badala yake. Ni machache mnayo yakumbuka. Maelezo

4. Na miji mingapi tuliiangamiza, ikaifikia adhabu yetu usiku au walipo kuwa wamelala adhuhuri. Maelezo

5. Basi hakikuwa kilio chao ilipo wafikia adhabu yetu, isipo kuwa kusema: Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu. Maelezo

6. Na kwa yakini tutawauliza wale walio pelekewa Ujumbe, na pia tutawauliza hao Wajumbe. Maelezo

7. Tena tutawasimulia kwa ilimu; wala Sisi hatukuwa mbali. Maelezo

8. Na Siku hiyo kipimo kitakuwa kwa Haki. Basi watakao kuwa na uzani mzito, hao ndio watakao fanikiwa. Maelezo

9. Na watakao kuwa na uzani khafifu, basi hao ndio walio zitia khasarani nafsi zao kwa sababu ya kuzipinga Ishara zetu. Maelezo

10. Na hakika tumekuwekeni katika ardhi, na tumekujaalieni humo njia za kupatia maisha. Ni kuchache kushukuru kwenu. Maelezo

11. Na hakika tulikuumbeni, kisha tukakutieni sura, kisha tukawaambia Malaika: Msujudieni Adam. Basi wakasujudu isipo kuwa Iblisi, hakuwa miongoni mwa walio sujudu. Maelezo

12. Mwenyezi Mungu akasema: Nini kilicho kuzuia kumsujudia nilipo kuamrisha? Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo. Maelezo

13. Akasema: Basi teremka kutoka humo! Haikufalii kufanya kiburi humo. Basi toka! Hakika wewe u miongoni mwa walio duni. Maelezo

14. Akasema: Nipe muhula mpaka siku watakapo fufuliwa. Maelezo

15. Akasema: Utakuwa miongoni mwa walio pewa muhula. Maelezo

16. Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika Njia yako Iliyo Nyooka. Maelezo

17. Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani. Maelezo

18. Akasema: Toka humo, nawe umekwisha fedheheka, umekwisha fukuzwa. Hapana shaka atakaye kufuata miongoni mwao, basi nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote. Maelezo

19. Na wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii, na kuleni humo mpendapo. Wala msiukaribie mti huu, mkawa katika wale walio dhulumu. Maelezo

20. Basi Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizo fichiwa, na akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele. Maelezo

21. Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanao kunasihini. Maelezo

22. Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao zilifichuka na wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi akawaita: Je, sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa dhaahiri? Maelezo

23. Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika. Maelezo

24. Akasema: Teremkeni! Mtakuwa nyinyi kwa nyinyi maadui. Na kwenye ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda. Maelezo

25. Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo mtatolewa. Maelezo

26. Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu mpate kukumbuka. Maelezo

27. Eny wanaadamu! Asije Shet'ani kukufitinini kama alivyo watoa wazazi wenu Peponi, akawavua nguo zao kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila yake wanakuoneni, na nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya Mashet'ani kuwa ni marafiki wa wasio amini. Maelezo

28. Na wanapo fanya mambo machafu husema: Tumewakuta nayo baba zetu, na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi mambo machafu. Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua? Maelezo

29. Sema: Mola Mlezi wangu ameamrisha uadilifu, na mumuelekeze nyuso zenu kila mnapo sujudu, na muombeni Yeye kwa kumsafia Dini. Kama alivyo kuumbeni mwanzo ndivyo mtavyo rudi, Maelezo

30. Hali ya kuwa kundi moja amelihidi, na kundi jengine limethibitikiwa na upotofu. Kwa hakika hao waliwafanya mashet'ani kuwa ndio marafiki walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, na wanadhani kuwa wao wameongoka. Maelezo

31. Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu. Maelezo

32. Sema: Ni nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo watolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walio amini katika uhai wa duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanao jua. Maelezo

33. Sema: Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya dhaahiri na ya siri, na dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asicho kiletea uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua. Maelezo

34. Na kila umma una muda wake. Utakapo fika muda wao basi hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia. Maelezo

35. Enyi wanaadamu! Watakapo kufikieni Mitume miongoni mwenu wakakuelezeni Ishara zangu, basi watakao mchamngu na wakatengenea haitakuwa khofu kwao, wala hawatahuzunika. Maelezo

36. Na wale watakao kanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hao ni watu wa Motoni; humo watadumu. Maelezo

37. Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au anaye zikanusha Ishara zake? Hao itawafikia sehemu yao waliyo andikiwa, mpaka watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha, watawaambia: Wako wapi mlio kuwa mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea! Na watajishuhudia wenyewe kwamba walikuwa makafiri. Maelezo

38. Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizo pita kabla yenu za majini na watu. Kila utakapo ingia umma utawalaani wenzake. Mpaka watakapo kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya Motoni marudufu. Atasema: Itakuwa kwenu nyote marudufu, lakini nyinyi hamjui tu. Maelezo

39. Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao: Basi nyinyi pia hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyachuma. Maelezo

40. Hakika wale wanao zikanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wakosefu. Maelezo

41. Jahannamu itakuwa kitanda chao na juu yao nguo za moto za kujifunika. Na hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu. Maelezo

42. Na wale wanao amini na wakatenda mema - hatumkalifishi mtu yoyote ila kwa kiasi cha uwezo wake - hao ndio watu wa Peponi. Wao watadumu humo. Maelezo

43. Na tutaondoa chuki vifuani mwao, na mbele yao iwe inapita mito. Na watasema: Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuhidi kufikia haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakutuhidi. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. Na watanadiwa kwamba: Hiyo ndiyo Pepo mliyo rithishwa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyafanya. Maelezo

44. Na watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni: Sisi tumekuta aliyo tuahidi Mola wetu Mlezi kuwa ni kweli. Je, na nyinyi pia mmekuta aliyo kuahidini Mola wenu Mlezi kuwa ni kweli? Watasema: Ndiyo! Basi mtangazaji atawatangazia: Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu, Maelezo

45. Wale ambao walikuwa wakizuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na wakataka kuipotosha, nao wanaikanusha Akhera. Maelezo

46. Na baina ya makundi mawili hayo patakuwapo pazia. Na juu ya Mnyanyuko patakuwa watu watakao wajua wote kwa alama zao, na wao watawaita watu wa Peponi: Assalamu Alaykum, Amani juu yenu! Wao bado hawajaingia humo, lakini wanatumai. Maelezo

47. Na yanapo geuzwa macho yao kuelekea watu wa Motoni, watasema: Mola Mlezi wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu walio dhulumu. Maelezo

48. Na hao watu wa Mnyanyukoni watawaita watu wanao wajua kwa alama zao. Watasema: Kujumuika kwenu hakukufaini kitu, wala hicho mlicho kuwa mnafanyia kiburi. Maelezo

49. Je, hawa sio wale mlio kuwa mkiwaapia kuwa Mwenyezi Mungu hatawafikishia rehema. Ingieni Peponi, hapana khofu kwenu, wala hamtahuzunika! Maelezo

50. Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi: Tumimieni maji, au chochote alicho kuruzukuni Mwenyezi Mungu. Nao watasema: Hakika Mwenyezi Mungu ameviharimisha hivyo kwa makafiri, Maelezo

51. Ambao waliifanya dini yao kuwa ni pumbao na mchezo, na maisha ya dunia yakawadanganya. Basi leo Sisi tunawasahau kama walivyo usahau mkutano wa Siku yao hii, na kwa sababu ya kule kuzikataa Ishara zetu. Maelezo

52. Na hakika tumewaletea Kitabu tulicho kipambanua kwa ilimu, uwongofu na rehema kwa watu wenye kuamini. Maelezo

53. Je, lipo wanalo lingojea isipo kuwa matokeo yake? Siku yatapo fika matokeo yake watasema wale walio kisahau: Kweli Mitume wa Mola Mlezi wetu walileta Haki! Je, tunao waombezi ili watuombee? Au turudishwe ili tufanye yasiyo kuwa yale tuliyo kuwa tukiyafanya? Bila ya shaka wamejikhasiri nafsi zao, na yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua. Maelezo

54. Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. Maelezo

55. Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa siri. Hakika Yeye hawapendi warukao mipaka. Maelezo

56. Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa. Na muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyzi Mungu iko karibu na wanao fanya mema. Maelezo

57. Na Yeye ndiye anaye peleka pepo (za kuvuma) kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata hizo pepo zinapo beba mawingu mazito tunayachunga mpaka kwenye nchi iliyo kufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, ndio kama hivyo tukatolesha kila aina ya matunda. Basi hali kadhaalika tunavyo wafufua wafu, ili mpate kukumbuka. Maelezo

58. Na ardhi njema, yenye udongo wa rutba, hutoa mimea yenye kukua vizuri yenye uhai, kwa idhini ya Mola Mlezi wake. Na ardhi mbaya haitoi ila mimea michache, isiyo na faida, tena kwa shida. Na hivyo ndivyo tunavyo zipambanua Ishara (Aya) kwa watu wanao shukuru. Maelezo

59. Tulimpeleka Nuhu kwa kaumu yake, naye akasema: Enyi kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku iliyo kuu. Maelezo

60. Wale watukufu katika kaumu yake wakasema: Hakika sisi tunakuona wewe umo katika upotofu ulio dhaahiri. Maelezo

61. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotofu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote. Maelezo

62. Nakufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na ninakunasihini; na ninayajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi. Maelezo

63. Je, mnastaajabu kukujieni mawaidha yanayotoka kwa Mola Mlezi wenu kwa njia ya mtu aliye ni mmoja katika nyinyi, ili akuonyeni na ili mumchemngu, na ili mpate kurehemewa? Maelezo

64. Basi walimkanusha. Nasi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika jahazi. Na tukawazamisha wale walio kanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu vipofu. Maelezo

65. Na kwa A'adi tulimpeleka ndugu yao, Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu ila Yeye. Basi je, hamumchi? Maelezo

66. Wakasema watukufu wa wale walio kufuru katika kaumu yake: Sisi tunakuona umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakufikiria kuwa wewe ni katika waongo. Maelezo

67. Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu. Lakini mimi ni Mtume niliye toka kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote. Maelezo

68. Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi kwenu ni mwenye kukunasihini, muaminifu. Maelezo

69. Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu Mlezi kwa mtu aliye mmoja wenu nyinyi ili akuonyeni? Na kumbukeni alivyo kufanyeni mshike pahala pa kaumu ya Nuhu, na akakuzidisheni katika umbo. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa. Maelezo

70. Wakasema: Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli. Maelezo

71. Akasema: Bila ya shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha kukuangukieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Mnabishana nami kwa ajili ya majina tu mliyo yaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha uthibitisho? Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wanao ngoja. Maelezo

72. Basi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye kwa rehema zetu, na tukakata mizizi ya wale walio zikanusha Ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini. Maelezo

73. Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu. Maelezo

74. Na kumbukeni alivyo kufanyeni wa kushika pahala pa A'adi na akakuwekeni vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake, na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu wala msitende uovu katika nchi kwa ufisadi. Maelezo

75. Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia wanao onewa wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola Mlezi wake? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa. Maelezo

76. Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayo yaamini. Maelezo

77. Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na wakasema: Ewe Saleh! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume. Maelezo

78. Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipo kucha wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa. Maelezo

79. Basi Saleh akwaacha na akasema: Enyi watu wangu! Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi hamwapendi wenye nasaha. Maelezo

80. Na tulimtuma Lut', alipo waambia watu wake: Je, mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe vyote! Maelezo

81. Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mkwawacha wanawake? Kumbe nyinyi ni watu wafujaji! Maelezo

82. Na haikuwa jawabu ya kaumu yake isipo kuwa kuambizana: Wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanao jitakasa. Maelezo

83. Basi tukamwokoa yeye na watu wake, isipo kuwa mkewe, alikuwa miongoni mwa walio bakia nyuma. Maelezo

84. Na tukawamiminia mvua. Basi tazama jinsi ulivyo kuwa mwisho wa wakosefu. Maelezo

85. Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu mwengine isipo kuwa Yeye. Imekwisha kufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini. Maelezo

86. Wala msikae katika kila njia mkitisha watu, na kuwazuilia na Njia ya Mwenyezi Mungu wale wenye kumuamini, na mkataka njia ipotoke. Na kumbukeni mlipo kuwa wachache, naye akakufanyeni kuwa wengi. Na tazameni jinsi ulivyo kuwa mwisho wa mafisadi. Maelezo

87. Na kama liko kundi miongoni mwenu lililo amini haya niliyo tumwa, na kundi jengine halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yetu. Naye ndiye Mbora wa wenye kuhukumu. Maelezo

88. WAHESHIMIWA WALIO TAKABARI katika kaumu yake wakasema: Ewe Shua'ib! Tutakutoa wewe pamoja na wale walio kuamini katika mji wetu, au mrejee katika mila yetu. Akasema: Je, ingawa tunaichukia? Maelezo

89. Bila ya shaka itakuwa tumemzulia uwongo Mwenyezi Mungu tukirudi katika mila yenu baada ya kwisha tuokoa nayo Mwenyezi Mungu. Wala haiwi kwetu sisi kuirejea mila hiyo, ila akitaka Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu. Ujuzi wa Mola Mlezi wetu umeenea katika kila kitu. Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea. Ewe Mola Mlezi wetu! Tuhukumie baina yetu na kaumu yetu kwa haki, nawe ndiye mbora wa wanao hukumu. Maelezo

90. Na waheshimiwa walio kufuru katika kaumu yake wakasema: Mkimfuata Shua'ib, basi hakika hapo nyinyi mtakuwa mlio khasiri. Maelezo

91. Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na wakaamkia majumbani mwao wamejifudikiza, wamekwisha kufa. Maelezo

92. Wale walio mkanusha Shua'ib wakawa kama kwamba hawakuwako. Walio mkanusha Shua'ib ndio walio kuwa wenye kukhasiri. Maelezo

93. Basi akawaachilia mbali na akasema: Enyi kaumu yangu! Nimekufikishieni Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na nimekunasihini; basi vipi niwahuzunikie watu makafiri? Maelezo

94. Na hatukumtuma Nabii yeyote katika mji ila tuliwapatiliza wakaazi wake kwa taabu na mashaka ili wapate kunyenyekea. Maelezo

95. Kisha Sisi hubadilisha mahala pa ubaya kwa wema, hata wakazidi, na wakasema: Taabu na raha ziliwafikia baba zetu. Basi kwa ghafla tukawashika, hali ya kuwa hawajatambua. Maelezo

96. Na lau kuwa watu wa miji wangeli amini na wakamchamngu, kwa yakini tungeli wafungulia baraka kutoka mbinguni na katika ardhi. Lakini walikanusha basi tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyachuma. Maelezo

97. Je, watu wa mijini wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafika usiku, nao wamelala? Maelezo

98. Au watu wa mijini wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafika mchana, nao wanacheza? Maelezo

99. Je, wamejiaminisha na mipango ya Mwenyezi Mungu? Kwani hawajiaminishi na mipango ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye kukhasiri. Maelezo

100. Je, hawahidiki hawa wanao rithi ardhi baada ya wale wenyewe kwamba tukitaka tutawapatiliza kwa madhambi yao, na tutapiga muhuri juu ya nyoyo zao, na kwa hivyo hawatasikia? Maelezo

101. Miji hiyo, tunakusimulia baadhi ya khabari zake. Na hapana shaka Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo waziwazi. Lakini hawakuwa wenye kuamini waliyo yakanusha zamani. Namna hivi Mwenyezi Mungu anazipiga muhuri nyoyo za makafiri. Maelezo

102. Wala hatukuwaona wengi wao kuwa wanatimiza ahadi; bali kwa hakika tuliwakuta wengi wao ni wapotofu. Maelezo

103. Kisha baada yao tukamtuma Musa na Ishara zetu kwa Firauni na waheshimiwa wake. Nao wakazikataa. Basi tazama ulikuwaje mwisho wa waharibifu. Maelezo

104. Na Musa alisema: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote. Maelezo

105. Inafaa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila lilio la Haki. Nami hakika nimekujieni na dalili waziwazi kutokana na Mola Mlezi wenu. Basi waache Wana wa Israili wende nami. Maelezo

106. Akasema Firauni: Ikiwa umekuja na Ishara, basi ilete ukiwa ni katika wasemao kweli. Maelezo

107. Basi akaitupa fimbo yake, na mara ikawa nyoka dhaahiri. Maelezo

108. Na akatoa mkono wake, mara ukawa mweupe kwa watazamao. Maelezo

109. Wakasema waheshimiwa wa kaumu ya Firauni: Hakika huyo ni mchawi mjuzi. Maelezo

110. Anataka kukutoeni katika nchi yenu. Basi mnatoa shauri gani? Maelezo

111. Wakasema: Mwache kidogo yeye na nduguye, na watume mijini wakusanyao, Maelezo

112. Wakuletee kila mchawi mjuzi. Maelezo

113. Wakaja wachawi kwa Firauni, wakasema: Hakika tutapata ujira ikiwa tutashinda. Maelezo

114. Akasema: Naam! Nanyi bila ya shaka mtakuwa katika wa karibu nami. Maelezo

115. Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe, au tutakuwa sisi tutao tupa? Maelezo

116. Akasema: Tupeni! Basi walipo tupa waliyazuga macho ya watu na wakawatia khofu, na wakaleta uchawi mkubwa. Maelezo

117. Nasi tukamfunulia Musa kumwambia: Tupa fimbo yako. Mara ikavimeza vyote vile walivyo vibuni. Maelezo

118. Kweli ikathibiti na yakabat'ilika waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

119. Kwa hivyo walishindwa hapo, na wakageuka kuwa wadogo. Maelezo

120. Na wachawi wakapoomoka wakisujudu. Maelezo

121. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa viumbe vyote, Maelezo

122. Mola Mlezi wa Musa na Haarun. Maelezo

123. Akasema Firauni: Mmemuamini kabla sijakupeni idhini? Hizi ni njama mlizo panga mjini mpate kuwatoa wenyewe. Lakini karibu mtajua! Maelezo

124. Lazima nitaikata mikono yenu na miguu yenu mbali mbali. Kisha nitakutundikeni misalabani. Maelezo

125. Wakasema: Sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. Maelezo

126. Nawe hukuudhika nasi ila kwa kuwa tumeziamini Ishara za Mola Mlezi wetu zilipo tujia. Ewe Mola Mlezi wetu! Tumiminie uvumilivu na utufishe hali ni Waislamu. Maelezo

127. Wakasema waheshimiwa wa kaumu ya Firauni: Unamuacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi na wakuache wewe na miungu yako? Akasema: Tutawauwa wavulana wao, na tutawaacha hai wanawake wao. Na bila ya shaka sisi ni wenye nguvu juu yao. Maelezo

128. Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu, na subirini. Hakika ardhi ni ya Mwenyezi Mungu. Naye humrithisha amtakaye katika waja wake. Na mwisho ni wa wachamngu. Maelezo

129. Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia, na baada ya wewe kutujia! Musa akasema: Huenda Mola wenu Mlezi akamhiliki adui wenu, na akakufanyeni nyinyi ndio wa kufuatia kushika nchi, ili atazame mtavyo kuja tenda nyinyi. Maelezo

130. Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa miyaka (ya ukame) na kwa upungufu wa mazao, ili wapate kukumbuka. Maelezo

131. Likiwafika jema wakisema: Haya ni haki yetu. Na likiwafika ovu husema: Musa na walio pamoja naye ni wakorofi. Hakika ukorofi wao huo unao wafikia unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui. Maelezo

132. Na wakisema: Hata ukituletea Ishara yoyote kutuzuga hatuto kuamini. Maelezo

133. Basi tukawapelekea tufani, na nzige, na chawa, na vyura, na damu, kuwa ni Ishara mbali mbali. Nao wakapanda kiburi, na wakawa watu wakosefu. Maelezo

134. Na ilipo waangukia adhabu wakasema: Ewe Musa! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa aliyo kuahidi. Ukituondolea adhabu hii hapana shaka tutakuamini, na tutawaachilia Wana wa Israili wende nawe. Maelezo

135. Lakini tukiwaondolea adhabu mpaka muda fulani wao waufikie, mara wakivunja ahadi yao. Maelezo

136. Basi tuliwapatiliza, tuka- wazamisha baharini kwa sababu walizikanusha Ishara zetu, na wakaghafilika nazo. Maelezo

137. Na tukawarithisha watu walio kuwa wanadharauliwa mashariki na magharibi ya ardhi tuliyo ibariki. Na likatimia neno jema la Mola Mlezi wako juu ya Wana wa Israili, kwa vile walivyo subiri. Na tukayaangamiza aliyo kuwa akiyafanya Firauni na kaumu yake, na waliyo kuwa wakiyajenga. Maelezo

138. Na tukawavusha bahari Wana wa Israili, wakafika kwa watu wanao abudu masanamu yao. Wakasema: Ewe Musa! Hebu tufanyie na sisi miungu kama hawa walivyo kuwa na miungu. Musa akasema: Hakika nyinyi ni watu msio jua kitu. Maelezo

139. Hakika haya waliyo nayo watu hawa yatakuja angamia, na hayo waliyo kuwa wakiyafanya yamepotea bure. Maelezo

140. Akasema: Je, nikutafutieni mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye aliye kufadhilisheni juu ya viumbe vyote? Maelezo

141. Na pale tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio kupeni adhabu za mwisho wa uovu. Wakiwauwa wavulana wenu, na wakawaacha hai wanawake wenu. Na katika hayo yalikuwa majaribio makubwa kutokana na Mola wenu Mlezi. Maelezo

142. Tulimuahidi Musa masiku thalathini na tukayatimiza kwa kumi; ikatimia miadi ya Mola wake Mlezi masiku arubaini. Na Musa akamwambia nduguye Haarun: Shika mahala pangu kwa watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu. Maelezo

143. Na alipo kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamsemeza, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutoniona. Lakini utazame huo mlima. Ukibaki pahala pake basi utaniona. Basi alipo jionyesha Mola Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike, na Musa akaanguka chini amezimia. Alipo zindukana alisema: Subhanaka, Umetakasika! Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini. Maelezo

144. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteuwa wende kwa watu na Ujumbe wangu na maneno yangu. Basi chukua niliyo kupa na uwe katika wanao shukuru. Maelezo

145. Na tukamuandikia katika mbao kila kitu, mawaidha na maelezo ya mambo yote. (Tukamwambia): Basi yashike kwa nguvu na uwaamrishe watu wako wayashike kwa ubora wake. Nami nitakuonyesheni makaazi ya wapotofu. Maelezo

146. Nitawatenga na Ishara zangu wale wanao fanya kiburi katika nchi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu, na wameghafilika nazo. Maelezo

147. Na walio zikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera a'mali zao zimeharibika. Kwani watalipwa ila kwa yale waliyo kuwa wakiyatenda? Maelezo

148. Na baada yake walimfanya ndama kutokana na mapambo yao (kumuabudu), kiwiliwili tu kilicho kuwa na sauti. Hivyo, hawakuona kuwa hawasemezi wala hawaongoi njia? Wakamuabudu, na wakawa wenye kudhulumu. Maelezo

149. Na walipo juta na wakaona ya kwamba wamekwisha potea, walisema: Ikiwa Mola wetu Mlezi hakuturehemu na akatusamehe, bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa walio khasiri. Maelezo

150. Na alipo rudi Musa kwa watu wake, naye amekasirika na kuhuzunika, alisema: Ni maovu yalioje mlio nifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu Mlezi? Na akaziweka chini zile mbao, na akamkamata kichwa ndugu yake akimvutia kwake. (Haarun) akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika hawa watu wamenidharau, na wakakaribia kuniuwa. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu, wala usinifanye pamoja na watu madhaalimu. Maelezo

151.(Musa) akasema: Mola Mlezi wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu, na ututie katika rehema yako. Nawe ni Mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu. Maelezo

152. Hakika wale walio muabudu ndama, itawapata ghadhabu ya Mola wao Mlezi na madhila katika maisha ya dunia. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wazushi. Maelezo

153. Na walio tenda maovu, kisha wakatubia baada yake na wakaamini, hapana shaka kuwa Mola Mlezi wako baada ya hayo ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. Maelezo

154. Na Musa ilipo mtulia ghadhabu aliziokota zile mbao. Na katika maandiko yake mna uwongofu na rehema kwa wanao mwogopa Mola wao Mlezi. Maelezo

155. Na Musa akawateuwa watu sabiini katika kaumu yake kwa miadi yetu. Na ulipo fika mtetemeko mkubwa alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ungeli taka ungeli wahiliki wao na mimi zamani! Unatuhiliki kwa waliyo yafanya wajinga katika sisi? Haya si chochote ila ni mtihani wako, umpoteze umtakaye na umhidi umtakaye. Wewe ndiye Rafiki Mlinzi wetu. Basi tughufirie na uturehemu. Na Wewe ndiye mbora wa kughufiria. Maelezo

156. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika Akhera. Sisi tumerejea kwako. (Mwenyezi Mungu) akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye. Na rehema yangu imeenea kila kitu. Lakini nitawaandikia khasa wanao mchamngu, na wanao toa Zaka, na wale ambao wanaziamini Ishara zetu, Maelezo

157. Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanaye mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao. Basi wale walio muamini yeye, na wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyo teremshwa pamoja naye - hao ndio wenye kufanikiwa. Maelezo

158. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliye tumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye anaye huisha na anaye fisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka. Maelezo

159. Na katika kaumu ya Musa lipo kundi linao waongoa watu kwa haki na kwa haki wanafanya uadilifu. Maelezo

160. Na tuliwagawanya katika makabila kumi na mbili, mataifa mbali mbali. Na tulimfunulia Musa walipo muomba maji watu wake kumwambia: Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatibuka humo chemchem kumi na mbili, na kila watu wakajua mahali pao pa kunywea. Na tukawafunika kivuli kwa mawingu, na tukawateremshia Manna na Salwa. Tukawaambia: Kuleni vizuri hivi tulivyo kuruzukuni. Wala hawakutu- dhulumu Sisi, bali wamejidhulumu wenyewe. Maelezo

161. Na pale walipo ambiwa: Kaeni katika mji huu, na mle humo mpendapo, na semeni: Tufutie dhambi zetu. Na ingieni katika mlango wake kwa unyenyekevu, tupate kukusameheni makosa yenu. Walio wema tutawazidishia. Maelezo

162. Lakini walio dhulumu miongoni mwao walibadilisha kauli, sio ile waliyo ambiwa. Basi tukawapelekea adhabu kutoka mbinguni kwa vile walivyo kuwa wakidhulumu. Maelezo

163. Na waulize khabari za mji ulio kuwa kando ya bahari, wakiivunja Sabato (Jumaamosi ya mapumziko). Samaki walikuwa wakiwajia juu juu siku ya mapumziko yao, na siku zisio kuwa za kupumzika hawakuwa wakiwajia. Kwa namna hiyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakifanya upotovu. Maelezo

164. Na kikundi kati yao walisema: Kwa nini mnawawaidhi watu ambao tangu hapo Mwenyezi Mungu atawateketeza au atawaadhibu adhabu kali? Wakasema: Ili uwe ni udhuru kwa Mola Mlezi wenu, na huenda nao wakamchamngu. Maelezo

165. Basi walipo yasahau waliyo kumbushwa, tuliwaokoa walio kuwa wakikataza maovu, na tukawatesa walio dhulumu kwa adhabu mbaya kwa vile walivyo kuwa wakifanya upotovu. Maelezo

166. Walipo jifakharisha katika waliyo kanywa tuliwaambia: Kuweni manyani wa kudharauliwa. Maelezo

167. Na pale alipo tangaza Mola wako Mlezi kwamba hapana shaka atawaletea watu ambao watawaadhibu kwa adhabu mbaya mpaka Siku ya Kiyama. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwepesi wa kuadhibu, na bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na Mwenye kurehemu. Maelezo

168. Na tuliwafarikisha katika ardhi makundi makundi. Wako kati yao walio wema, na wengine kinyume cha hivyo. Na tukawajaribu kwa mema na mabaya ili wapate kurejea. Maelezo

169. Na wakafuatia baada yao kizazi kibaya walio rithi Kitabu. Wakashika anasa za haya maisha duni, na wakasema: Tutasamehewa! Na ikiwajia tena anasa kama hiyo wataishika pia. Je, hawakufanyiwa agano la Kitabu kuwa wasiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila Haki tu? Nao wamekwisha soma yaliomo humo. Na nyumba ya Akhera ni bora kwa wanao jikinga na maasi. Basi je, hamtii akilini? Maelezo

170. Na wale wanao kishikilia Kitabu, na wakashika Sala - hakika Sisi hatupotezi ujira wa watendao mema. Maelezo

171. Na pale tulipo unyanyua mlima juu yao ukawa kama kwamba ni kiwingu kilicho wafunika, na wakadhani kuwa utawaangukia, (tukawaambia): Kamateni kwa nguvu tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kumcha Mungu. Maelezo

172. Na pale Mola wako Mlezi alipo waleta katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo. Maelezo

173. Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu? Maelezo

174. Ndio kama hivyo tunavyo zipambanua Ishara, kwa kutaraji kuwa watarejea. Maelezo

175. Na wasomee khabari za yule ambaye tulimpa Ishara zetu, naye akajivua nazo. Na Shet'ani akamuandama, akawa miongoni walio potea. Maelezo

176. Na tungelitaka tungeli mtukuza kwa hizo Ishara, lakini yeye aliushikilia ulimwengu na akafuata pumbao lake. Basi mfano wake ni mfano wa mbwa. Ukimhujumu hupumua na kutoa ulimi na ukimwacha pia hupumua na kutoa ulimi. Huo ni mfano wa kaumu wanao zikanusha Ishara zetu. Basi simulia hadithi, huenda wakatafakari. Maelezo

177. Huu ni mfano muovu kabisa wa watu wanao kanusha Ishara zetu na wakajidhulumu nafsi zao. Maelezo

178. Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemhidi basi huyo amehidika; na alio waacha kupotea basi hao ndio walio khasirika. Maelezo

179. Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika. Maelezo

180. Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo. Na waacheni wale wanao haribu utakatifu wa majina yake. Hao watakuja lipwa waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

181. Na katika tulio waumba wako watu wanao ongoza kwa Haki, na kwayo wanafanya uadilifu. Maelezo

182. Na wale walio kadhibisha Ishara zetu, tutawapururia pole pole kwa namna ambayo wenyewe hawaijui. Maelezo

183. Nami nitawapa muda. Hakika mpango wangu ni madhubuti. Maelezo

184. Je, hawafikiri? Huyu mwenzao hana wazimu. Hakuwa yeye ila ni mwonyaji aliye dhaahiri. Maelezo

185. Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi, na vitu alivyo viumba Mwenyezi Mungu, na pengine ajali yao imekwisha karibia? Basi maneno gani baada ya haya watayaamini? Maelezo

186. Aliye mwacha Mwenyezi Mungu kupotea hana wa kumwongoa. Atawaacha hao wakitangatanga katika upotofu wao. Maelezo

187. Wanakuuliza hiyo Saa (ya mwisho) itakuwa lini? Sema: Kuijua kwake kuko kwa Mola Mlezi wangu. Haidhihirishi hiyo kwa wakati wake ila Yeye. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haikujiini ila kwa ghafla tu. Wanakuuliza kama kwamba wewe una pupa ya kuijua. Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu. Lakini aghlabu ya watu hawajui. Maelezo

188. Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu ninge jizidishia mema mengi, wala ovu lisinge nigusa. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mbashiri kwa watu wanao amini. Maelezo

189. Yeye ndiye aliye kuumbeni katika nafsi moja; na katika hiyo hiyo akamfanya mwenzi wake, ili akae naye kwa utulivu. Na anapo muingilia hubeba mzigo mwepesi, akitembea nao. Anapo kuwa mja mzito, wote wawili humwomba Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wao: Kama ukitupa mwana mwema tutakuwa katika wanao shukuru. Maelezo

190. Basi anapo wapa mwana mwema, wanamfanyia washirikina Mwenyezi Mungu katika kile kile alicho wapa. Mwenyezi Mungu ametukuka na huko kushirikisha kwao. Maelezo

191. Ati wanawafanya viumbe kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu, nao hawaumbi, bali wao ndio wanaumbwa? Maelezo

192. Wala hawana uwezo wa kuwanusuru wala wenyewe hawajinusuru. Maelezo

193. Na mkiwaita kwenye uwongofu, hawakufuateni. Ni mamoja kwenu ikiwa mtawaita au mkinyamaza. Maelezo

194. Hakika hao mnao waomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu ni waja mfano wenu nyinyi. Hebu waombeni, nao wakuitikieni, kama mnasema kweli. Maelezo

195. Je, wao wanayo miguu ya kwendea? Au wanayo mikono ya kutetea? Au wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikizia? Sema: Iiteni hio miungu yenu ya ushirikina. Kisha nifanyieni mimi vitimbi, wala msinipe muhula. Maelezo

196. Hakika Mlinzi wangu ni Mwenyezi Mungu aliye teremsha Kitabu. Naye ndiye awalindae walio wema. Maelezo

197. Na hao mnao waomba asiye kuwa Mwenyezi hawawezi kukunusuruni, wala hawajinusuru wenyewe. Maelezo

198. Na mkiwaita kwenye uwongofu hawasikii. Na unawaona wanakutazama, nao hawaoni. Maelezo

199. Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na majaahili. Maelezo

200. Na uchochezi wa Shet'ani ukikuchochea basi omba ulinzi wa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Msikizi, Mjuzi. Maelezo

201. Hakika wale wamchao Mungu, zinapo wagusa pepesi za Shet'ani, mara huzindukana na hapo huwa wenye kuiona haki. Maelezo

202. Na ndugu zao wanawavutia kwenye upotofu, kisha wao hawaachi. Maelezo

203. Na usipo waletea Ishara waitakayo husema: Kwa nini hukuibuni? Sema: mimi ninafuata yanayo funuliwa kwangu kutokana na Mola Mlezi wangu. Hii (Qur'ani) ni hoja zinazo toka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu na rehema kwa watu wanao amini. Maelezo

204. Na isomwapo Qur'ani isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemewa. Maelezo

205. Na mkumbuke Mola Mlezi wako nafsini kwako kwa unyenyekevu na khofu, na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni. Wala usiwe miongoni wa walio ghafilika. Maelezo

206. Hakika wale walioko kwa Mola wako Mlezi hawajivuni wakaacha kumuabdu, na wanamtakasa na wanamsujudia. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani