Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

11. SURAT HUD

(Imeteremka Makka)

 

Surat Hud ni Sura ya Makka. Ina Aya 123. Imeanza kwa kuisifu Qur'ani Tukufu, na kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na kuonya, na kubashiria. Kisha ikabainisha uwezo wa Mwenyezi Mungu na kuwa  Yeye ndiye Mola Mlezi. Na ikaeleza hali za watu katika kuzipokea kwao neema zake Mola Mlezi, na adhabu zake. Kisha ikataja cheo cha Qur'ani, na kufuru za makafiri bila ya udhuru wowote kwa ukafiri wao, na malipo ya Waumini.
Naye Subhanahu baada ya hayo amesimulia hadithi za Manabii, na majadiliano ya kaumu zao nao, na kuwateremkia makafiri adhabu ya duniani na kuokoka kwa Waumini. Subhanahu wa Taa'la akataja hadithi ya Nuhu kwa kupambanua zaidi kuliko ilivyo kuwa katika Surat Yunus. Humu imeelezwa fikra za kafiri na inadi yake, na imebainishwa ilivyo mteremkia chuki. Na baada ya hadithi ya Nuhu Mwenyezi Mungu Subhanahu ametaja kisa cha A'ad pamoja na Nabii wa Mwenyezi Mungu Hud, kwa kueleza wazi mawazo ya ukafiri, na yaliyo wateremkia makafiri juu ya kuwa walikuwa na nguvu na wakali.
Kisha kikatajwa mfano wa hayo kisa cha Nabii wa Mwenyezi Mungu, Saleh pamoja na kabila la Thamud, na tena kisa cha Nabiyyu Llah na rafiki yake, Ibrahim. Kisha hadithi wa Nabiyyu Llah, Lut'. Kisha kisa cha Nabiyyu Llah, Shua'ib.
Kisha Subhanahu wa Taala ametaja nini mafunzo ya hadithi hizi za kweli, na akamalizia Subhanahu kwa kuwataka Waumini watende mema, na wangojee malipo. Tena ukatajwa ujuzi ulio kamilika wa Mwenyezi Mungu  Aliye takasika na kutukuka, na waajibu wa kumtegemea Yeye.
 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye Khabari, Maelezo

2. Ili msimuabudu isipo kuwa Allah, Mwenyezi Mungu. Hakika mimi kwenu ni mwonyaji na mbashiri nitokae kwake. Maelezo

3. Na ili mumwombe msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu. Na atampa kila mwenye fadhila, fadhila yake. Na ikiwa mtakengeuka basi mimi nakukhofieni adhabu ya hiyo Siku Kubwa. Maelezo

4. Marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu tu. Naye ni Muweza wa kila kitu. Maelezo

5. Hebu angalia! Ati wanafunika vilivyomo vifuani mwao ili wamfiche Mwenyezi Mungu! Jueni kuwa wanapo jigubika nguo zao Yeye anajua wanayo yaficha na wanayo yatangaza. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. Maelezo

6. NA HAKUNA mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha. Maelezo

7. Na Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Na Kiti chake cha Enzi kilikuwa juu ya maji, ili akufanyieni mtihani ajuulikane ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo. Na wewe ukisema: Nyinyi hakika mtafufuliwa baada ya kufa; wale walio kufuru husema: Hayakuwa haya ila ni uchawi uliyo wazi. Maelezo

8. Na tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda ulio kwisha hisabiwa wao husema: Nini kinacho izuia hiyo adhabu? Jueni! Siku itakapo wajia basi haitoondolewa hiyo kwao. Na yatawazunguka yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha. Maelezo

9. Na tukimwonjesha mtu rehema inayo toka kwetu, kisha tukamwondolea, hukata tamaa akakufuru. Maelezo

10. Na tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyo mpata husema: Taabu zimekwisha niondokea. Hakika yeye hujitapa na kutafakhari. Maelezo

11. Ila wale walio subiri wakatenda mema. Hao watapata msamaha na ujira mkubwa. Maelezo

12. Basi labda utaacha baadhi ya yale yaliyo funuliwa kwako, na kifua kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema: Mbona hakuteremshiwa khazina, au wakaja naye Malaika? Wewe ni mwonyaji tu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu. Maelezo

13. Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni Sura kumi zilizo zuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli. Maelezo

14. Na wasipo kuitikieni, basi jueni ya kwamba (hii Qur'ani) imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana mungu ila Yeye. Basi je! Nyinyi ni Waislamu? Maelezo

15. Wanao taka maisha ya dunia na pumbao lake tutawalipa humo vitendo vyao kaamili. Na wao humo hawatopunjwa. Maelezo

16. Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu Akhera ila Moto, na yataharibika waliyo yafanya, na yatapotea bure waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

17. Basi je, mtu aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake Mlezi, inayo fuatwa na shahidi anaye toka kwake, na kabla yake kilikuwa Kitabu cha Musa kilicho kuwa mwongozi na rehema - hao wanamuamini, na anaye mkataa katika makundi, basi Moto ndio pahala pa miadi yao. Basi usiwe na shaka juu ya hayo. Hii ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi; lakini watu wengi hawaamini. Maelezo

18. Na nani aliye dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao Mlezi, na mashahidi watasema: Hawa ndio walio mtungia uwongo Mola wao Mlezi. Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu, Maelezo

19. Ambao wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanaitakia ipotoke, na wanaikataa Akhera. Maelezo

20. Hao hawawezi kushinda katika ardhi, wala hawana walinzi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu. Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona. Maelezo

21. Hao ndio walio zikhasiri nafsi zao, na yakawapotea waliyo kuwa wakiyazua. Maelezo

22. Bila ya shaka hakika wao ndio wenye kukhasiri huko Akhera. Maelezo

23. Hakika wale walio amini,na wakatenda mema, na wakanyenyekea kwa Mola wao Mlezi, hao ndio watu wa Peponi, na humo watadumu. Maelezo

24. Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu kiziwi, na mwenye kuona na anasikia. Je, wawili hawa wanakuwa sawa kwa kufananishwa? Basi, je, hamfikiri? Maelezo

25. Na Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akawaambia: Hakika mimi ni mwonyaji kwenu ninaye bainisha, Maelezo

26. Ya kwamba msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu tu. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Chungu. Maelezo

27. Na wakasema wakuu walio kufuru katika kaumu yake: Hatukuoni wewe ila ni mtu tu kama sisi, wala hatukuoni wamekufuata ila wale walio kuwa kwetu watu duni, wasio kuwa na akili. Wala hatukuoneni kuwa mna ubora wowote kutushinda sisi. Bali tuna hakika nyinyi ni waongo. Maelezo

28. Akasema: Enyi watu wangu! Hebu fikirini! Ikiwa mimi ninayo hoja wazi iliyo toka kwa Mola wangu Mlezi, na amenipa rehema kutoka kwake, nayo ikakufichikieni; je, tukulazimisheni kuikubali hali nyinyi mnaichukia? Maelezo

29. Na enyi watu wangu! Mimi sikuombeni mali kwa ajili ya haya. Mimi sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walio amini. Hakika wao watakutana na Mola wao Mlezi, lakini mimi nakuoneni mnafanya ujinga. Maelezo

30. Na enyi watu wangu! Ni nani atakaye nisaidia kwa Mwenyezi Mungu nikiwafukuza hawa? Basi je, hamfikiri? Maelezo

31. Wala sikwambiini kuwa nina khazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi najua mambo ya ghaibu; wala sisemi: Mimi ni Malaika. Wala siwasemi wale ambao yanawadharau macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri - Mwenyezi Mungu anajua yaliomo katika nafsi zao - hapo bila ya shaka ninge kuwa miongoni mwa wenye kudhulumu. Maelezo

32. Wakasema: Ewe Nuhu! Umejadiliana, na umekithirisha kutujadili. Basi tuletee hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli. Maelezo

33. Akasema: Mwenyezi Mungu atakuleteeni akipenda. Wala nyinyi si wenye kumshinda. Maelezo

34. Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kukuachieni mpotee. Yeye ndiye Mola wenu Mlezi; na kwake mtarejeshwa. Maelezo

35. Au ndio wanasema: Ameizua? Sema: Ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi sikhusiki na makosa myatendayo. Maelezo

36. Na akafunuliwa Nuhu akaambiwa: Hataamini yeyote katika watu wako ila wale walio kwisha amini. Basi usisikitike kwa waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

37. Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu. Wala usinisemeze kuwatetea walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa. Maelezo

38. Na akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Yeye akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi tunakukejelini kama mnavyo tukejeli. Maelezo

39. Nanyi mtakuja jua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu. Maelezo

40.Hata ilipo kuja amri yetu, na tanuri ikafoka maji, tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike, kutoka kila aina, na ahali zako, isipo kuwa wale ambao imekwisha wapitia hukumu; na watu walio amini. Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu. Maelezo

41. Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillahi, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. Maelezo

42. Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuhu akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi, wala usiwe pamoja na makafiri. Maelezo

43. Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. (Nuhu) akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu ila aliye mrehemu mwenyewe. Na wimbi likawatenganisha, akawa katika walio zama. Maelezo

44. Na ikasemwa: Ewe ardhi! Meza maji yako. Na Ewe mbingu! Jizuie. Basi maji yakadidimia chini, na amri ikapitishwa, na (jahazi) likasimama juu ya (mlima) wa Al Juudiy. Na ikasemwa: Wapotelee mbali watu walio dhulumu! Maelezo

45. Na Nuhu alimwomba Mola wake Mlezi: Ee Mola Mlezi wangu! Hakika mwanangu ni katika ahali zangu, na hakika ahadi yako ni haki. Na Wewe ni Mwenye haki kuliko mahakimu wote. Maelezo

46. Akasema: Ewe Nuhu! Huyu si katika ahali zako. Mwendo wake si mwema. Basi usiniombe jambo usio na ujuzi nalo. Mimi nakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa wajinga. Maelezo

47. Nuhu akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi najikinga kwako nisikuombe nisio na ujuzi nalo. Na kama hunisamehe na ukanirehemu, nitakuwa katika walio khasiri. Maelezo

48. Ikasemwa: Ewe Nuhu! Shuka kwa salama itokayo kwetu, na baraka nyingi juu yako na juu ya watu walio pamoja nawe. Na zitakuwapo kaumu tutakazo zistarehesha, na kisha zitashikwa na adhabu chungu itokayo kwetu. Maelezo

49. Hizi ni katika khabari za ghaibu tunazo kufunulia. Hukuwa ukizijua wewe, wala watu wako, kabla ya hii. Basi subiri! Hakika Mwisho ni wa wachamngu. Maelezo

50. Na kwa kina A'adi tulimtuma ndugu yao Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu! Nyinyi hamna mungu isipo kuwa Yeye. Nyinyi si chochote ila ni wazushi tu. Maelezo

51. Enyi watu wangu! Sikuombeni ujira kwa ajili ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa Yule aliye niumba. Basi hamtumii akili? Maelezo

52. Na enyi watu wangu! Muombeni msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua ya kumiminika, na atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke mkawa wakosefu. Maelezo

53. Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi. Wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kufuata kauli yako. Na wala sisi hatukuamini wewe. Maelezo

54. Sisi tunasema: Baadhi katika miungu yetu imekusibu kwa baa. Akasema: Hakika mimi namshuhudisha Mwenyezi Mungu, na nyinyi shuhudieni, ya kwamba mimi najitenga mbali na hao mnao wafanya washirika, Maelezo

55. Mkamwacha Yeye. Basi nyote nyinyi nipangieni vitimbi, na kisha msinipe muhula! Maelezo

56. Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wangu na Mola Mlezi wenu. Hapana kiumbe yeyote ila Yeye anamwendesha atakavyo. Hakika Mola wangu Mlezi yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

57. Na ikiwa watarudi nyuma, basi mimi nimekwisha kufikishieni niliyo tumwa kwenu. Na Mola wangu Mlezi atawaleta watu wengine badala yenu, wala nyinyi hamumdhuru kitu Yeye. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu. Maelezo

58. Ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Hud na walio amini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu. Na tukawaokoa na adhabu ngumu. Maelezo

59. Na hao ndio kina A'adi. Walizikanusha Ishara za Mola wao Mlezi, na wakawaasi Mitume wake, na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inda. Maelezo

60. Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na Siku ya Kiyama. Basi tambueni mtanabahi! Hakika kina A'adi walimkufuru Mola wao Mlezi. Na tambueni mtanabahi kuwa hakika waliangamizwa kina A'adi, kaumu ya Hud. Maelezo

61. Na kina Thamud tuliwapelekea ndugu yao Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Yeye ndiye aliye kuumbeni katika ardhi, na akakuwekeni humo. Basi mwombeni msamaha, kisha mtubu kwake. Hakika Mola wangu Mlezi yupo karibu, anaitikia maombi. Maelezo

62. Wakasema: Ewe Saleh! Hakika kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa kheri kwetu. Je, unatukataza tusiwaabudu waliyo kuwa wakiwaabudu baba zetu? Na hakika sisi tuna shaka na wasiwasi kwa hayo unayo tuitia. Maelezo

63. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninazo dalili zilizo wazi kutokana na Mola wangu Mlezi, naye akawa kanipa rehema kutoka kwake - je, ni nani atakaye ninusuru kwa Mwenyezi Mungu nikimuasi? Basi nyinyi hamtanizidishia ila khasara tu. Maelezo

64. Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu ni Ishara kwenu. Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya, isije ikakuangamizeni adhabu iliyo karibu. Maelezo

65. Wakamchinja. Basi (Saleh) akasema: Stareheni katika mji wenu muda wa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyo kuwa ya uwongo. Maelezo

66. Basi ilipo kuja amri yetu tulimwokoa Saleh na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu kutokana na hizaya ya siku ile. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kushinda. Maelezo

67. Na ukelele uliwaangamiza wale walio dhulumu, wakapambazukiwa nao ni maiti majumbani mwao. Maelezo

68. Kama kwamba hawakuwako huko. Hebu zingatieni! Hakika kina Thamud walimkufuru Mola wao Mlezi. Hebu zingatieni! Thamud wamepotelea mbali! Maelezo

69. Na wajumbe wetu walimjia Ibrahim kwa bishara njema, wakasema: Salama! Naye akasema: Salama! Hakukaa ila mara akaleta ndama wa kuchoma. Maelezo

70. Basi alipoona mikono yao haimfikilii aliwatilia shaka, na akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut'. Maelezo

71. Na mkewe alikuwa kasimama wima, akacheka. Basi tukambashiria (kuzaliwa) Is-haq, na baada ya Is-haq Yaaqub. Maelezo

72. Akasema: Je, hivyo mimi nizae, na hali yangu ni kikongwe na huyu mume wangu ni kizee? Hakika haya ni mambo ya ajabu! Maelezo

73. Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye ndiye Msifiwa wa kutukuzwa. Maelezo

74. Basi khofu ilipo mwondoka Ibrahim, na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya kaumu ya Lut'. Maelezo

75. Hakika Ibrahim alikuwa mpole, ana huruma, na mwepesi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu. Maelezo

76. (Akaambiwa): Ewe Ibrahim! Wachilia mbali haya! Kwa hakika amri ya Mola wako Mlezi imekwisha kuja, na hakika hao itawafikia adhabu isiyo rudi nyuma. Maelezo

77. Na wajumbe wetu walipo kuja kwa Lut' aliwahuzunukia na akawaonea dhiki. Akasema: Hii leo ni siku ngumu! Maelezo

78. Wakamjia kaumu yake mbio mbio. Na kabla ya haya walikuwa wakitenda maovu. Yeye akasema: Enyi watu wangu! Hawa binti zangu, ndio wametakasika zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi mbele ya wageni wangu. Hivyo, hamna hata mtu mmoja miongoni mwenu aliye ongoka? Maelezo

79. Wakasema: Bila shaka umekwisha jua hatuna haki juu ya binti zako, na unayajua tunayo yataka. Maelezo

80. Akasema: Laiti ningeli kuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu! Maelezo

81. (Wajumbe) wakasema: Ewe Lut'! Sisi ni wajumbe wa Mola wako Mlezi. Hawa hawatakufikia. Na wewe ondoka pamoja na ahali zako usiku ungalipo. Wala yeyote miongoni mwenu asitazame nyuma, isipo kuwa mkeo, kwani yeye utamfika msiba utakao wafika hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Je, asubuhi si karibu? Maelezo

82. Basi ilipo fika amri yetu tuliigeuza nchi juu chini, na tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu ulio kamatana wa Motoni, Maelezo

83. Zilizo tiwa alama kwa Mola wako Mlezi. Na haya hayako mbali na wenye kudhulumu wengineo. Maelezo

84. Na kwa watu wa Madyana tuliwatumia ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye, wala msipunguze vipimo na mizani. Mimi nakuoneni mmo katika hali njema, nami nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa hiyo itakayo kuzungukeni. Maelezo

85. Na enyi watu wangu! Timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwakhini watu vitu vyao; wala msieneze uovu katika nchi mkafanya uharibifu. Maelezo

86. Alivyo kubakishieni Mwenyezi Mungu ndiyo bora kwa ajili yenu, ikiwa nyinyi ni Waumini. Wala mimi siye mlinzi wenu. Maelezo

87. Wakasema: Ewe Shua'ibu! Ni sala zako ndizo zinazo kuamrisha tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu, au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu? Ama hakika wewe ni mstahamilivu kweli na mwongofu! Maelezo

88. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili wazi inayo tokana na Mola wangu Mlezi, na ikawa Yeye ameniruzuku riziki njema kutoka kwake? Wala mimi sipendi kukukhalifuni nikafanya yale ninayo kukatazeni. Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyo weza. Na sipati kuwezeshwa haya ila na Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye ninategemea, na kwake Yeye naelekea. Maelezo

89. Na enyi watu wangu! Kukhalifiana nami kusikupelekeeni hata mkasibiwa kama walivyo sibiwa watu wa Nuhu, au watu wa Hud, au watu wa Saleh. Na watu wa Lut' si mbali nanyi. Maelezo

90. Na ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi, tena tubuni kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kurehemu na Mwenye upendo. Maelezo

91. Wakasema: Ewe Shua'ibu! Mengi katika hayo unayo yasema hatuyafahamu. Na sisi tunakuona huna nguvu kwetu. Lau kuwa si jamaa zako tunge kupiga mawe, wala wewe si mtukufu kwetu. Maelezo

92. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu? Na Yeye mmemueka nyuma ya migongo yenu! Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuyazunguka yote mnayo yatenda. Maelezo

93. Na enyi watu wangu! Fanyeni mwezayo, na mimi pia ninafanya. Karibuni mtajua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na nani aliye mwongo. Na ngojeni, mimi pia ninangoja pamoja nanyi. Maelezo

94. Na ilipo fika amri yetu, tulimwokoa Shua'ibu na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu. Na ukelele uliwanyakua walio dhulumu, na wakapambaukiwa majumbani mwao wamekufa kifudifudi! Maelezo

95. Kama kwamba hawakuwamo humo. Zingatia walivyo angamia watu wa Madyana, kama walivyo angamia watu wa Thamud! Maelezo

96. Na hakika tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na uthibitisho ulio wazi Maelezo

97. Kwa Firauni na waheshimiwa wake. Lakini wao walifuata amri ya Firauni, na amri ya Firauni haikuwa yenye uwongofu. Maelezo

98. Siku ya Kiyama atawatangulia watu wake na atawaingiza Motoni. Na muingio muovu ulioje huo! Maelezo

99. Nao wamefuatishiwa laana hapa duniani na Siku ya Kiyama. Ni mabaya yalioje watakayo pewa! Maelezo

100. Hizi ni katika khabari za miji, tunakusimulia. Mingine ipo bado na mingine imefyekwa. Maelezo

101. Na Sisi hatukuwadhulumu, lakini wao wenyewe wamejidhulumu. Na miungu yao waliyo kuwa wakiiomba badala ya Mwenyezi Mungu haikuwafaa kitu ilipo kuja amri ya Mola wako Mlezi. Na hiyo miungu haikuwazidishia ila maangamizo tu. Maelezo

102. Na ndio kama hivyo ndivyo inavyo kuwa Mola wako Mlezi anapo ikamata miji inapo kuwa imedhulumu. Hakika mkamato wake ni mchungu na mkali. Maelezo

103. Hakika katika haya ipo ishara kwa yule anaye ogopa adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo Siku itakayo kusanyiwa watu, na hiyo ndiyo Siku itakayo shuhudiwa. Maelezo

104. Na Sisi hatuiakhirishi ila kwa muda unao hisabiwa. Maelezo

105. Siku hiyo itakapo fika, hatosema hata mtu mmoja ila kwa idhini yake Mwenyezi Mungu. Kati yao watakuwamo waliomo mashakani na wenye furaha. Maelezo

106. Ama wale wa mashakani hao watakuwamo Motoni wakiyayayatika na kukoroma. Maelezo

107. Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hakika Mola wako Mlezi hutenda apendavyo. Maelezo

108. Na ama wale walio bahatika, wao watakuwamo Peponi wakidumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipo kuwa apendavyo Mola wako Mlezi. Hicho ni kipawa kisio na ukomo. Maelezo

109. Basi usiwe na shaka juu ya wanayo yaabudu hao. Hawaabudu ila kama walivyo abudu baba zao zamani. Na hakika Sisi tutawatimilizia fungu lao bila ya kupunguzwa. Maelezo

110. Na kwa yakini tulimpa Musa Kitabu; zikazuka khitilafu ndani yake. Na lau kuwa si neno lilio kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka ingeli hukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka juu yake inayo wahangaisha. Maelezo

111. Na hakika Mola wako Mlezi atawatimilizia malipo ya vitendo vyao. Hakika Yeye anayo khabari ya wayatendayo. Maelezo

112. Basi, simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wewe na wale wanao elekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo. Maelezo

113. Wala msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, wala tena hamtasaidiwa. Maelezo

114. Na shika Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka. Maelezo

115. Na subiri, kwani Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanao fanya wema. Maelezo

116. Basi mbona hawakuwamo katika watu wa kabla yenu wenye vyeo na wasaa wanao kataza uharibifu katika nchi, isipo kuwa wachache tu, ambao ndio tulio waokoa? Na walio dhulumu walifuata starehe zao, na wakawa ni wakosefu. Maelezo

117. Wala hakuwa Mola wako Mlezi wa kuihiliki miji kwa dhulma tu na hali watu wake ni watenda mema. Maelezo

118. Na Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana, Maelezo

119. Isipo kuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako Mlezi: Kweli kweli nitaijaza Jahannam kwa majini na watu pamoja. Maelezo

120. Na yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini. Maelezo

121. Na waambie wale wasio amini: Fanyeni muwezavyo, nasi pia tunafanya. Maelezo

122. Na ngojeni, na sisi tunangoja. Maelezo

123. Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo fichikana katika ardhi na mbingu, na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu Yeye na umtegemee Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki na yale mnayo yatenda. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani