Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

12. SURAT YUSUF

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii ni ya Makka, na Aya zake ni mia na kumi na moja. Ndani yake Mwenyezi Mungu amesimulia hadithi ya Yusuf katika Aya tisiini na nane, na ameitangulizia kwa Aya tatu alizo taja ndani yake huu ufunuo alio mteremshia Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zishuke juu yake.  Na ameuita ufunuo huu katika Aya ya kwanza: Kitabu kinacho bainisha. Na katika Aya ya pili akauiita: Qur'ani kwa Kiarabu, kuwa ni kuashiria kwamba ni haki yake uhifadhiwe kwa maandishi na katika vifua vya watu vile vile.  Kisha katika Aya ya tatu akataja kuwa ufunuo huu umekusanya simulizi nzuri kabisa, na ukataja kuwa Nabii Muhammad hakuwa akiyajua hayo kabla hakuteremshiwa huo Wahyi (ufunuo). Na hiyo ni dalili kuwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kisa hichi na Sura hii imemalizikia kwa kutilia mkazo yaliyo anzia. Na akamuelekeza Nabii mnamo Aya kumi azingatie kuwa masimulizi haya ni katika khabari za ghaibu, ambazo yeye Nabii, Salla Llahu alayhi wasallama, hakuwa akizijua, na kuzijua ukweli wake zilivyo, kabla ya kuteremshiwa Wahyi. Wala yeye hakuwa pamoja na hao ndugu zake Yusuf walipo kuwa wakipanga mipango yao, na wakiunda njama zao za shari kumuundia ndugu yao kwa baba. Kisha Qur'ani inamwambia Mtume kuwa inda na husda huwapelekea watu wengi kuingia ukafirini. Na kwamba pupa yake Mtume s.a.w. kuwa waamini wengi wao haitomfalia kitu, lakini Qur'ani inampoza kwa hayo kwa kuwa yeye hataki ujira, ila ni kuwa yeye anawaletea Qur'ani iwe ni uwongofu na ukumbusho kwa watu wote. Na mwisho wa Sura inaashiria Mitume ambao hadithi zao zimesimuliwa, na ukasimuliwa msimamo wa kaumu zao, na vipi mwishoe walivyo washinda makafiri wakosefu. Na katika hadithi hizi za Manabii pana mazingatio kwa wenye akili. Hakika hii Qur'ani inayo simulia masimulio haya na mengineyo si kitu cha kutungwa tu na kuzuliwa kuwa kinatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa uwongo. Hakika hii ni haki na kweli tupu, na hichi ni Kitabu kinacho sadikisha Vitabu sahihi vilivyo toka mbinguni, na ni uwongofu, na rehema kwa watu wanao zingatia na wakaamini.
Linalo onekana wazi katika sifa za Sura hii ni kuwa kimesimuliwa kisa cha Yusuf kwa ukamilifu wake. Na pia imeonekana kuwa katika ule ule ukoo mmoja upo uhasidi ulio enea na pia katika baadhi yao yapo mapenzi. Husda ya wana wa Yaaqub iliwapelekea kumtumbukiza ndugu yao kisimani. Lakini Mwenyezi Mungu alimlinda na vitimbi vyao, kama alivyo mkinga na matamanio ya mke wa Mheshimiwa pale Yusuf alipo fikilia utuuzima nyumbani kwa Mheshimiwa. Mwenyezi Mungu akamweka vizuri katika nchi ya Misri, na akamjaalia kuwa nchi hiyo iwe makimbilio (mategemeo) ya wale walio mpangia njama za kumdhuru.  Basi ni hivyo shani yake Subhanahu wa Taa'la kwa Manabii wake na vipenzi vyake. Huwanusuru dhidi ya maadui zao, na huwathibitisha na kuwaweka vyema katika ardhi maadamu wanaishika Haki na wanaiamini, na wanaishikilia kamba ya Mwenyezi Mungu.
 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alif Lam Raa. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha. Maelezo

2. Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu ili mpate kuzingatia. Maelezo

3. Sisi tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur'ani hii. Na ijapo kuwa kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasio jua. Maelezo

4. Yusuf alipo mwambia baba yake: Ewe babaangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja, na jua, na mwezi. Nimeota zikinisujudia. Maelezo

5. (Baba) akasema: Ewe mwanangu! Usiwasimulie nduguzo ndoto yako, wasije wakakufanyia vitimbi. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu. Maelezo

6. Na kadhaalika Mola wako Mlezi atakuteuwa na atakufundisha tafsiri ya mambo. Na atatimiza neema zake juu yako na juu ya ukoo wa Yaa'qub, kama alivyo watimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni Mjuzi Mwenye hikima. Maelezo

7. Kwa yakini katika Yusuf na nduguze ziko ishara kwa wanao uliza. Maelezo

8. Pale walipo sema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi, hali sisi ni kikundi chenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu wa dhaahiri. Maelezo

9. Muuweni Yusuf, au mtupeni nchi mbali ili uso wa baba yenu ukuelekeeni nyinyi. Na baada ya haya mtakuwa watu wema. Maelezo

10. Akasema msemaji kati yao: Msimuuwe Yusuf. Lakini mtumbukizeni ndani ya kisima. Wasafiri watakuja mwokota; kama nyinyi mna sharti ya kufanya jambo. Maelezo

11. Wakasema: Ewe baba yetu! Una nini hata hutuamini kwa Yusuf? Na hakika sisi ni wenye kumtakia kheri! Maelezo

12. Mpeleke kesho pamoja nasi, ale kwa furaha na acheze; na bila ya shaka sisi tutamhifadhi. Maelezo

13. Akasem: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninaogopa asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye. Maelezo

14. Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na hali sisi ni kundi lenye nguvu kabisa, basi bila ya shaka sisi tutakuwa khasarani. Maelezo

15. Basi walipo mchukua na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima, tulimfunulia Yusuf: Hapana shaka yoyote utakuja waambia kwa jambo lao hili, na wala wao hawatambui. Maelezo

16. Wakaja kwa baba yao usiku wakilia. Maelezo

17. Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana na tukamwacha Yusuf penye vitu vyetu. Basi mbwa mwitu akamla. Lakini wewe hutuamini ijapo kuwa tunasema kweli. Maelezo

18. Wakaja na kanzu yake ina damu ya uwongo. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayo yaeleza. Maelezo

19. Ukafika msafara, wakamtuma mchota maji wao, naye akatumbukiza ndoo yake. Alisema: Kheri Inshallah! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili kumfanya ni bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayo yatenda. Maelezo

20. Na wakamuuza kwa thamani duni, kwa akali ya pesa. Wala hawakuwa na haja naye. Maelezo

21. Na yule aliye mnunua huko Misri alimwambia mkewe: Mtengenezee makaazi ya hishima huyu; huenda akatufaa au tukamfanya mwenetu. Na kama hivyo tulimweka Yusuf katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo lake, lakini watu wengi hawajui. Maelezo

22. Na alipo fikilia utu uzima tulimpa hukumu na ilimu. Na kama hivi tunawalipa wanao tenda mema. Maelezo

23. Na yule bibi wa nyumba aliyo kuwamo Yusuf alimtamani kinyume cha nafsi yake, na akafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yusuf akasema: Audhubillahi! Najikinga na Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi. Maelezo

24. Na hakika yule mwanamke alimtamani, na Yusuf angeli mtamani lau kuwa hakuona ishara ya Mola wake Mlezi. Hayo hivyo ni kwa ajili tumuepushe na uovu na uchafu. Hakika yeye alikuwa katika waja wetu walio safishwa. Maelezo

25. Na wote wawili wakakimbilia mlangoni, na mwanamke akairarua kanzu yake Yusuf kwa nyuma. Na wakamkuta bwana wake mlangoni. Mwanamke akasema: Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipo kuwa kufungwa au kupewa adhabu chungu. Maelezo

26. Yusuf akasema: Yeye ndiye aliye nitaka bila ya mimi kumtaka. Na shahidi aliye kuwa katika jamaa za mwanamke alisema: Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele basi mwanamke amesema kweli, naye Yusuf ni katika waongo. Maelezo

27. Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma, basi mwanamke amesema uwongo, naye Yusuf ni katika wakweli. Maelezo

28. Basi yule bwana alipoona kanzu yake imechanwa kwa nyuma, alisema: Hakika haya ni katika vitimbi vyenu wanawake. Bila ya shaka vitimbi vyenu ni vikuu. Maelezo

29. Yusuf! Wachilia mbali haya. Na wewe, mwanamke, omba msamaha kwa dhambi zako. Kwa hakika wewe ni katika walio fanya makosa. Maelezo

30. Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa Mheshimiwa anamtamani mtumishi wake ! Hakika amesalitika kwa mapenzi. Sisi hakika tunamwona yumo katika upotovu ulio dhaahiri. Maelezo

31. Alipo sikia yule bibi masengenyo yao aliwaita, na akawawekea matakia ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu. Akamwambia Yusuf: Tokeza mbele yao. Basi walipo mwona waliona ni kitu kikubwa kabisa, na wakajikata mikono yao. Wakasema: Hasha Lillahi! Huyu si mwanaadamu. Hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu. Maelezo

32. Yule bibi aksema: Huyu basi ndiye huyo mliye nilaumia! Na kweli mimi nilimtaka naye akakataa. Na akitofanya ninayo muamrisha basi hapana shaka atafungwa gerezani, na atakuwa miongoni mwa walio chini kabisa. Maelezo

33. Yusuf akasema: Ee Mola Mlezi wangu! Nastahabu kifungo kuliko haya anayo niitia. Na usipo niondoshea vitimbi vya wanawake mimi nitamili kwao, na nitakuwa katika wajinga. Maelezo

34. Basi Mola wake Mlezi akamwitikia, na akamwondoshea vitimbi vyao. Hakika Yeye ni Msikizi Mjuzi. Maelezo

35. Basi ikawadhihirikia baada ya kuona Ishara kuwa wamfunge kwa muda. Maelezo

36. Wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Na mwingine akasema: Mimi nimeota nimebeba mikate juu ya kichwa changu, na ndege wanaila. Hebu tuambie tafsiri yake, kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema. Maelezo

37. Akasema: Hakitakufikilieni chakula mtakacho pewa ila nitakwambieni hakika yake kabla hakijakufikieni. Haya ni katika yale aliyo nifundisha Mola wangu Mlezi. Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasio muamini Mwenyezi Mungu, na wakawa hawaiamini Akhera. Maelezo

38. Na nimefuata mila ya baba zangu, Ibrahim, na Is-haq, na Yaa'qub. Hatuna haki ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote. Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu; lakini watu wengi hawashukuru. Maelezo

39. Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, mabwana wengi wanao farikiana wao kwa wao ni bora au Mwenyezi Mungu Mmoja Mwenye nguvu? Maelezo

40. Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyo yapanga nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipo kuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini Iliyo Nyooka. Lakini watu wengi hawajui. Maelezo

41. Enyi wafungwa wenzangu wawili! Ama mmoja wenu atamnywesha bwana wake mvinyo. Na ama mwengine atasulubiwa, na ndege watamla kichwa chake. Imekwisha katwa hukumu ya hilo jambo mlilo kuwa mkiuliza. Maelezo

42. Na akamwambia yule aliye jua kuwa atavuka katika wale wawili: Nikumbuke kwa bwana wako. Lakini Shet'ani alimsahaulisha kumtaja kwa bwana wake. Basi Yusuf akakaa gerezani miaka kadhaa. Maelezo

43. Na siku moja mfalme alisema: Hakika mimi nimeota ng'ombe saba wanene wanaliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu. Enyi waheshimiwa! Nambieni maana ya ndoto zangu, ikiwa nyinyi mnaweza kuagua ndoto. Maelezo

44. Wakasema: Hizi ni ndoto zilizo paraganyika, wala sisi sio wenye kujua tafsiri ya ndoto hizi. Maelezo

45. Hapo akasema yule aliye okoka katika wale wawili akakumbuka baada ya muda: Mimi nitakwambieni tafsiri yake. Basi nitumeni. Maelezo

46. Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu, ili nirejee kwa watu wapate kujua. Maelezo

47. Akasema: Mtalima miaka saba kwa juhudi. Mtacho vuna kiwacheni katika mashuke yake, isipo kuwa kidogo mtacho kula. Maelezo

48. Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayo kula kile mlicho iwekea isipo kuwa kidogo mtacho kihifadhi. Maelezo

49. Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao katika mwaka huo watu watasaidiwa, na watakamua. Maelezo

50. Na mfalme akasema: Mleteni kwangu! Basi mjumbe alipo mjia Yusuf alisema: Rejea kwa bwana wako ukamuulize khabari ya wale wanawake walio jikata mikono yao. Hakika Mola wangu Mlezi anazijua vyema hila zao. Maelezo

51. Mfalme alisema: Mlikuwa mna nini mlipo mtaka Yusuf kinyume na nafsi yake? Wakasema: Hasha Lillahi! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa Mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliye mtaka kinyume na nafsi yake, na hakika yeye ni katika wakweli. Maelezo

52. Hayo ni apate kujua ya kwamba mimi sikumfanyia khiyana nyuma yake; na ya kwamba Mwenyezi Mungu haziongoi hila za makhaini. Maelezo

53. NAMI sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu, isipo kuwa ile ambayo Mola wangu Mlezi aliyo irehemu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Msamehevu na Mwenye kurehemu. Maelezo

54. Basi mfalme akasema: Mleteni kwangu, awe wangu mwenyewe khasa. Basi alipo msemeza alinena: Hakika wewe leo umekwisha tamakani kwetu na umeaminika. Maelezo

55. Yusuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi. Maelezo

56. Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa humo popote anapo penda. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema. Maelezo

57. Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa walio amini na wakawa wachamngu. Maelezo

58. Wakaja ndugu zake Yusuf, na wakaingia kwake. Yeye akawajua na wao hawakumjua. Maelezo

59. Na alipo watengenezea tayari haja yao alisema: Nileteeni ndugu yenu kwa baba. Je! Hamwoni ya kwamba mimi ninatimiza kipimo, nami ni mbora wa kukirimu? Maelezo

60. Na msipo niletea basi hampati kipimo chochote kwangu, wala msinikurubie. Maelezo

61. Wakasema: Sisi tutamrairai baba yake; na bila ya shaka tutafanya hayo. Maelezo

62. Na Yusuf akawaambia watumishi wake: Tieni bidhaa zao katika mizigo yao, ili wazione watakapo rudi kwa watu wao wapate kurejea tena. Maelezo

63. Basi walipo rejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula zaidi, basi mpeleke nasi ndugu yetu ili tupate kupimiwa; na yakini sisi tutamlinda. Maelezo

64. Je, nikuaminini kwa huyu ila kama nilivyo kuaminini kwa nduguye zamani? Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kulinda, naye ndiye Mbora wa kurehemu kuliko wenye kurehemu wote. Maelezo

65. Na walipo fungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa. Wakasema: Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa. Wacha tuwaletee watu wetu chakula, na tutamlinda ndugu yetu, na tutaongeza shehena ya ngamia. Na hicho ni kipimo kidogo. Maelezo

66. Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwamba lazima mtamrejeza kwangu, ila ikiwa mmezungukwa. Basi walipo mpa ahadi yao alisema: Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa tuyasemayo. Maelezo

67. Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbali mbali. Wala mimi sikufaeni kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukumu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea, na juu yake Yeye wategemee wanao tegemea. Maelezo

68. Na walipo ingia kama alivyo waamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu, isipo kuwa ni haja tu iliyo kuwa katika nafsi ya Yaa'qub aliitimiza. Na hakika yeye alikuwa na ilimu kwa sababu tulimfundisha; lakini watu wengi hawajui. Maelezo

69.Na walipo ingia kwa Yusuf alimchukua nduguye akasema: Mimi hakika ni nduguyo. Basi usihuzunike kwa waliyo kuwa wakiyafanya . Maelezo

70. Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia kikopo cha kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi wasafiri! Hapana shaka nyinyi ni wezi! Maelezo

71. Wakasema nao wamewakabili: Kwani mmepoteza nini? Maelezo

72. Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na ataye lileta atapewa shehena nzima ya ngamia. Nami ni dhaamini wa hayo. Maelezo

73. Wakasema: Wallahi! Mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya uharibifu katika nchi hii, wala sisi si wezi. Maelezo

74. Wakasema: Basi malipo yake yatakuwa nini ikiwa nyinyi ni waongo? Maelezo

75. Wakasema: Malipo yake ni yule ambaye ataonekana nalo yeye huyo ndiye malipo yake. Hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu. Maelezo

76. Basi akaanza kwenye mizigo yao kabla ya mzigo wa nduguye. Kisha akakitoa katika mzigo wa nduguye. Hivi ndivyo tulivyo mpangia Yusuf. Hakuweza kumzuia nduguye kwa sharia ya mfalme isipo kuwa alivyo taka Mwenyezi Mungu. Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao; na juu ya kila ajuaye yupo ajuaye zaidi. Maelezo

77. Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile aliiba zamani. Lakini Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha. Akawaambia: Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi hayo mnayo singizia. Maelezo

78. Wakasema: Ewe Mheshimiwa! Huyu anaye baba mzee sana. Kwa hivyo mchukue mmoja wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema. Maelezo

79. Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali kumshika yeyote yule isipo kuwa tuliye mkuta naye kitu chetu. Hivyo basi tutakuwa wenye kudhulumu. Maelezo

80. Walipo kata tamaa naye wakenda kando kunong'ona. Mkubwa wao akasema: Je! Hamjui ya kwamba baba yenu amechukua ahadi kwenu kutokana na Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo mlimkosa katika agano lenu juu ya Yusuf? Basi mimi sitotoka nchi hii mpaka baba yangu anipe ruhusa au Mwenyezi Mungu anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu. Maelezo

81. Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu! Mwanao ameiba. Na sisi hatutoi ushahidi ila kwa tunayo yajua. Wala sisi hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu. Maelezo

82. Na waulize watu wa mji tulio kuwako, na msafara tulio kuja nao. Na hakika sisi tunasema kweli. Maelezo

83. Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye jambo fulani. Subira ni njema! Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima. Maelezo

84. Naye akajitenga nao, na akasema: Ah! Masikini Yusuf! Na macho yake yakawa meupe kwa huzuni aliyo kuwa akiizuia. Maelezo

85. Wakasema: Wallahi! Huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa au uwe katika walio hiliki. Maelezo

86. Akasema: Hakika mimi namshitakia Mwenyezi Mungu sikitiko langu na huzuni yangu. Na ninajua kwa Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi. Maelezo

87. Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa watu makafiri. Maelezo

88. Basi walipo ingia kwa Yusuf walisema: Ewe Mheshimiwa! Imetupata shida, sisi na watu wetu. Na tumeleta mali kidogo. Basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa watoao sadaka. Maelezo

89. Akasema: Je! Mmejua mliyo mfanyia Yusuf na nduguye mlipo kuwa wajinga? Maelezo

90. Wakasema: Kumbe wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anaye mcha Mungu na akasubiri, basi Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa wafanyao mema. Maelezo

91. Wakasema: Wallahi! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi, na hakika sisi tulikuwa wenye kukosa. Maelezo

92. Akasema: Leo hapana lawama juu yenu. Mwenyezi Mungu atakusameheni, naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanao rehemu. Maelezo

93. Nendeni na kanzu yangu hii na mumwekee usoni baba yangu, atakuwa mwenye kuona. Na mje nao watu wenu wote wa nyumbani. Maelezo

94. Na ulipo ondoka tu msafara baba yao alisema: Hakika mimi nasikia harufu ya Yusuf, lau kuwa hamtanituhumu. Maelezo

95. Wakasema: Wallahi! Hakika bado ungali katika upotovu wako wa zamani. Maelezo

96. Basi alipo fika mbashiri na akaiweka kanzu usoni pake alirejea kuona. Akasema: Je! Sikukwambieni kuwa mimi najua ya Mwenyezi Mungu msiyo yajua nyinyi? Maelezo

97. Wakasema: Ee baba yetu! Tuombee msamaha kwa dhambi zetu. Hapana shaka sisi tulikuwa na makosa. Maelezo

98. Akasema: Nitakuja kuombeeni msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye maghfira na Mwenye kusamehe. Maelezo

99. Na walipo ingia kwa Yusuf aliwakumbatia wazazi wake na akasema: Ingieni Misri, Inshallah, mmo katika amani. Maelezo

100. Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na Mwenyezi Mungu amenifanyia wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani baada ya Shet'ani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole kwa alitakalo. Bila ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima. Maelezo

101. Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika umenipa utawala, na umenifunza tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na nichanganyishe na watendao mema. Maelezo

102. Hizi ni katika khabari za ghaibu tulizo kufunulia. Na hukuwa pamoja nao walipo azimia shauri yao, walipo fanya njama zao wakizua vitimbi. Maelezo

103. Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi vipi.. Maelezo

104. Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote. Maelezo

105. Na ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazo zipitia, na hali ya kuwa wanazipuuza. Maelezo

106.Na wengi katika wao hawamuamini Mwenyezi Mungu pasina kuwa ni washirikina. Maelezo

107. Je! Wanaaminisha kuwa haitowajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ya kuwagubika, au haitawafikia Saa ya Kiyama kwa ghafla, na hali hawatambui? Maelezo

108. Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina. Maelezo

109. Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipo kuwa wanaume tulio wafunulia wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya Akhera ni bora kwa wamchao Mungu. Basi hamfahamu? Maelezo

110. Hata Mitume walipo kata tamaa na wakaona kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusura yetu, wakaokolewa tuwatakao. Na adhabu yetu haitowawacha kaumu ya wakosefu. Maelezo

111. Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani