Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

 

15. SURATUL HIJR

(Imeteremka Makka)

 

Suratul Hijr ni Sura ya Makka. Nayo ina Aya 99. Imeanza kwa harufi za kutamkwa zenye kueleza kwamba Qur'ani imejengeka kwa harufi hizi hizi mnazo zitumia katika maneno yenu, na juu ya hivyo ni Muujiza kwenu, hamwezi kuleta kama hii. Kwani aliye iteremsha ni Mwenyezi Mungu, Aliye takasaika, na Akatukuka. Na hizo harufi pia ni kama kuwazindua wale wanao ipuuza Qur'ani, inawalingania, inawaita, waisikilize. Asaa wakanufaika, na wakahidika kumfuata Mwenyezi Mungu.
Sura hii tukufu inabainisha ili watu wazingatie yaliyo wapata kaumu zilizo tangulia, na khabari za  Manabii walio kwisha pita, na yaliyo wapata kutokana na watu wao. Na pia Sura hii inaonyesha ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu, katika mbingu zilizo nyanyuliwa na zenye sayari ziilizo hifadhiwa, na ardhi iliyo tandikwa, na kukunjuliwa, na milima iliyo simama imara, na pepo zenye kubeba maji, na zenye kupandishia miti. Na Sura hii pia inaashiria mpambano wa mwanzo katika maumbile ya asli baina ya maluuni Iblisi na Adam na mkewe, na kuendelea mpambano huo baina ya kheri na shari mpaka imalizike dunia. Kisha tena malipo ya shari Siku ya Kiyama, na malipo ya kheri. Na baada ya hayo Mwenyezi Mungu anasimulia visa vya Manabii wawili, Ibrahim na Luut'i, na watu wa Al Hijr. Na Sura inaeleza cheo cha Qur'ani, na hali ya washirikina katika kuipokea, na impasavyo Nabii kwa mnasaba wa ukafiri wao, navyo ni kufikisha ujumbe wake, na kuutangaza, na kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka ifike amri ya yakini.
 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alif Lam Ra. (A.L.R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur'ani inayo bainisha. Maelezo

2. HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu. Maelezo

3. Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua. Maelezo

4. Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu. Maelezo

5. Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa. Maelezo

6. Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu. Maelezo

7. Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli? Maelezo

8. Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula. Maelezo

9. Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda. Maelezo

10. Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo. Maelezo

11. Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli. Maelezo

12. Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu. Maelezo

13. Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale. Maelezo

14. Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda, Maelezo

15. Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa. Maelezo

16. Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia. Maelezo

17. Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye. Maelezo

18. Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana. Maelezo

19. Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. Maelezo

20. Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku. Maelezo

21. Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu. Maelezo

22. Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka. Maelezo

23. Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi. Maelezo

24. Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua walio taakhari. Maelezo

25. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi. Maelezo

26. Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura. Maelezo

27. Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto. Maelezo

28. Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura. Maelezo

29. Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia. Maelezo

30. Basi Malaika wote pamoja walimsujudia, Maelezo

31. Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu. Maelezo

32. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu? Maelezo

33. Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yenye sura. Maelezo

34.(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni! Maelezo

35. Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo. Maelezo

36. Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapo fufuliwa. Maelezo

37. (Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula Maelezo

38. Mpaka siku ya wakati maalumu. Maelezo

39. Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote, Maelezo

40. Ila waja wako walio safika. Maelezo

41. Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka. Maelezo

42. Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata. Maelezo

43. Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote. Maelezo

44. Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa. Maelezo

45. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. Maelezo

46. (Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani. Maelezo

47. Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana. Maelezo

48. Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo. Maelezo

49. Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo

50. Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu! Maelezo

51. Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim. Maelezo

52. Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni. Maelezo

53. Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi. Maelezo

54. Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria? Maelezo

55. Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanao kata tamaa. Maelezo

56. Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea? Maelezo

57. Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe? Maelezo

58. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu! Maelezo

59. Isipo kuwa walio mfuata Luut'i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote. Maelezo

60. Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma. Maelezo

61. Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut'i, Maelezo

62. Alisema (Luut'i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana. Maelezo

63. Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka. Maelezo

64. Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli. Maelezo

65. Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa. Maelezo

66. Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali. Maelezo

67. Na wakaja watu wa mji ule nao furahani. Maelezo

68. Akasema: Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe. Maelezo

69. Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi. Maelezo

70. Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote? Maelezo

71. Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji. Maelezo

72. Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo. Maelezo

73. Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa. Maelezo

74. Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni. Maelezo

75. Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi. Maelezo

76. Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa. Maelezo

77. Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini. Maelezo

78. Na hakika watu wa Kichakani walikuwa wenye kudhulumu. Maelezo

79. Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia ilio wazi. Maelezo

80. Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume. Maelezo

81. Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza. Maelezo

82. Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani. Maelezo

83. Basi ukelele ukawatwaa asubuhi. Maelezo

84. Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma. Maelezo

85. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri. Maelezo

86. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi. Maelezo

87. Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur'ani Tukufu. Maelezo

88. Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini. Maelezo

89. Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha. Maelezo

90. Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa, Maelezo

91. Ambao wakaifanya Qur'ani vipande vipande. Maelezo

92. Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote, Maelezo

93. Kwa waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

94. Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina. Maelezo

95. Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli. Maelezo

96. Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine. Basi, watakuja jua! Maelezo

97. Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo. Maelezo

98. Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanao msujudia. Maelezo

99. Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani