Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

17. SURA AL ISRAAI (BANI ISRAIL)

(Imeteremka Makka)

 

 Sura hii tukufu ina Aya 111, nayo ni Sura ya Makka ila Aya hizi: 26, 32, 33, 57 na tangu Aya 73 mpaka Aya 80. Aya zote hizi, nazo ni 12, ni za Madina. Sura hii imeanza kwa kumsabihi, kumtakasa, Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kisha ikaitaja Israi, nayo ni safari ya usiku aliyo chukuliwa Mtume s.a.w. kutoka Makka mpaka Bait Al Muqaddas (Yerusalemu), na baadae akapelekwa mbinguni, na kurejeshwa Makka usiku ule ule.
Baadae Sura inaeleza Ujumbe wa Nabii Musa a.s., na yaliyo kuwa ya Wana wa Israili. Kisha ikaashiria cheo cha Qur'ani Tukufu katika uwongofu, na zikatajwa Aya za uumbaji usiku na mchana, na yatakayo watokea watu Siku ya Kiyama katika kulipwa kwa vitendo walivyo vitenda duniani. Na Subhanahu amebainisha sababu za kuharibika umma, na hali ya watu katika kuhangaika kwao, na matokeo ya vitendo vyao huko Akhera. Tena zikaja Aya za kutukuzwa wazazi, baba na mama, na hali ya watu kukhusu mali zao; na zikaja Amri Kumi za kuunda umma ulio bora. Kisha Subhanahu akauvunja uzushi wa washirikina kukhusu Malaika, kisha akabainisha Qur'ani inavyo eleza hoja zake.
Kisha Subhanahu akaashiria anavyo stahiki kuhimidiwa, na upinzani wa washirikina, akawapa wasia Waumini. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akaeleza namna anavyo watendea makafiri duniani na Akhera. Tena akaeleza asili ya uumbaji wa binaadamu na Shet'ani, na akawatisha washirikina kwa Aya zake. Baada ya hayo Subhanahu alibainisha utukufu wa binaadamu, na akataja adhabu za Siku ya Kiyama. Akataja vipi washirikina wanavyo jaribu kumzuia Nabii asitimize Wito wake, na vipi Mwenyezi Mungu anavyo mtia nguvu. Baada ya hayo Allahu Subhanahu wa Taa'la akamuusia Nabii kwa wasia za uwongofu, na wito mnasaba. Kisha akaashiria cheo cha Qur'ani Tukufu, na akataja khabari za Roho, na akaashiria siri zake. Kisha akataja umuujiza wa Qur'ani, kushindwa majini na watu kuleta mfano wake. Na akabainisha Subhanahu uwezo wake kuleta Ishara nyengine. Tena akataja vipi Qur'ani ilivyo kusanya Haki, na hali za Waumini wema katika Imani zao, na inavyo takikana kuwa daima wawe wanamhimidi Mwenyezi Mungu na wakimtukuza
 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona. Maelezo

2. Na tukampa Musa Kitabu, na tukakifanya uwongofu kwa Wana wa Israili. (Tukawambia): Msiwe na mtegemewa ila Mimi! Maelezo

3. Enyi kizazi tuliyo wachukua pamoja na Nuhu! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani. Maelezo

4. Na tukawahukumia Wana wa Israili katika Kitabu kwamba: Hakika nyinyi mtafanya fisadi katika nchi mara mbili, na kwa yakini mtapanda kiburi, kiburi kikubwa. Maelezo

5. Basi itapo fika ahadi ya kwanza yake tutakupelekeeni waja wetu wa kali kwa vita. Watakuingilieni ndani ya majumba. Na hii ilikuwa ahadi iliyo timizwa. Maelezo

6. Kisha tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao, na tukakusaidieni kwa mali na wana, na tukakujaalieni mkawa wengi zaidi. Maelezo

7. Basi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na mkifanya ubaya, mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa. Maelezo

8. Huenda Mola wenu Mlezi akakurehemuni. Na mkirudia na Sisi tutarudia. Na tumeifanya Jahannamu kuwa ni gereza kwa ajili ya makafiri. Maelezo

9. Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa. Maelezo

10. Na yakwamba wale wasio iamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu. Maelezo

11. Na mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani mwanaadamu ni mwenye pupa. Maelezo

12. Na tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili. Tena tukaifuta ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu. Na kila kitu tumekifafanua waziwazi.

13. Na kila mtu tumemfungia a'mali yake shingoni mwake. Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakacho kikuta kiwazi kimekunjuliwa. Maelezo

14. Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu. Maelezo

15. Anaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anaye potea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume. Maelezo

16. Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa. Maelezo

17. Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuhu! Na Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja wake. Maelezo

18. Anaye taka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka kumletea hapa hapa tunayo yataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannamu; ataingia humo hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa. Maelezo

19. Na anaye itaka Akhera, na akazifanyia juhudi a'mali zake, naye ni Muumini, basi hao juhudi yao itakuwa ni ya kushukuriwa. Maelezo

20. Wote hao tunawakunjulia - hawa na hao - katika neema za Mola wako Mlezi. Wala neema za Mola wako Mlezi hazizuiliki. Maelezo

21. Angalia vipi tulivyo wafadhili baadhi yao kuliko wenginewe. Na hakika Akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi. Maelezo

22. Usimfanye mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukawa wa kulaumiwa uliye tupika. Maelezo

23. Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Maelezo

24. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni. Maelezo

25. Mola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu. Ikiwa nyinyi mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanao tubia kwake. Maelezo

26. Na mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini, na msafiri; wala usitumie ovyo kwa fujo. Maelezo

27. Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashet'ani. Na Shet'ani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi. Maelezo

28. Na ikiwa unajikurupusha nao, nawe unatafuta rehema ya Mola wako Mlezi unayo itaraji, basi sema nao maneno laini. Maelezo

29. Wala usiufanye mkono wako kama ulio fungwa shingoni mwako, wala usiukunjue wote kabisa, utabaki ukilaumiwa muflisi. Maelezo

30. Hakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua na kuwaona. Maelezo

31. Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa. Maelezo

32. Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya. Maelezo

33. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki. Na aliye uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka mrithi wake. Lakini asipite mpaka katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa. Maelezo

34. Wala msiyakaribie mali ya yatima, isipo kuwa kwa njia iliyo bora, mpaka afike utuuzimani. Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa. Maelezo

35. Na timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni wema kwenu na khatimaye ndio bora. Maelezo

36. Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa. Maelezo

37. Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima. Maelezo

38. Haya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako Mlezi. Maelezo

39. Haya ni katika hikima alizo kufunulia Mola wako Mlezi. Wala usimweke pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije ukatupwa katika Jahannamu ukilaumiwa na kufurushwa. Maelezo

40. Je! Mola wenu Mlezi amekuteulieni wavulana, na Yeye akawafanya Malaika ni banati zake? Kwa hakika nyinyi mnasema usemi mkubwa. Maelezo

41. Na tumekwisha bainisha katika Qur'ani hii ili wapate kukumbuka. Lakini haikuwazidisha ila kuwa mbali nayo. Maelezo

42. Sema: Lau kuwa wangeli kuwa pamoja naye miungu mingine kama wasemavyo, basi wangeli tafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti cha Enzi. Maelezo

43. Subhanahu Wa Taa'la, Ametakasika na Ametukuka juu kabisa na hayo wanayo yasema. Maelezo

44. Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake. Hakika Yeye ni Mpole na Mwenye maghfira. Maelezo

45. Na unapo soma Qur'ani tunaweka baina yako na wale wasio iamini Akhera pazia linalo wafunika. Maelezo

46. Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu, na tunaweka kwenye masikio yao uziwi. Na unapo mtaja katika Qur'ani Mola wako Mlezi peke yake, basi wao hugeuka nyuma wakenda zao. Maelezo

47. Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayo sikilizia wanapo kusikiliza, na wanapo nong'ona. Wanapo sema hao madhaalimu: Nyinyi hamumfuati isipo kuwa mtu aliye rogwa. Maelezo

48. Tazama vipi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea. Kwa hivyo hawawezi kuipata njia. Maelezo

49. Na walisema: Je! Tutapo kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika, tutafufuliwa kwa umbo jipya? Maelezo

50. Sema: Kuweni hata mawe na chuma. Maelezo

51. Au umbo lolote mnalo liona kubwa katika vifua vyenu. Watasema: Nani atakaye turudisha tena? Sema: Yule yule aliye kuumbeni mara ya kwanza! Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa karibu! Maelezo

52. Siku atakapo kuiteni, na nyinyi mkamuitikia kwa kumshukuru, na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mdogo tu. Maelezo

53. Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shet'ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu. Maelezo

54. Mola wenu Mlezi anakujueni vilivyo. Akipenda atakurehemuni, na akipenda atakuadhibuni. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao. Maelezo

55. Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo mbinguni na katika ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine; na Daudi tulimpa Zaburi. Maelezo

56. Sema: Waombeni hao mnao wadaia badala yake Yeye. Hawawezi kukuondoleeni madhara, wala kuyaweka pengine. Maelezo

57. Hao wanao waomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno - na wanataraji rehema zake na wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi yafaa kutahadhari nayo. Maelezo

58. Na hapana mji wowote ila Sisi tutauteketeza kabla ya Siku ya Kiyama, au tutaupa adhabu kali. Haya yamekwisha andikwa katika Kitabu. Maelezo

59. Na hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki Ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha. Maelezo

60. Na tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amekwisha wazunguka hao watu. Na hatukuifanya ndoto tulio kuonyesha ila ni kuwajaribu watu, na mti ulio laaniwa katika Qur'ani. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa. Maelezo

61. Na pale tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam. Wakamsujudia isipo kuwa Iblisi. Akasema: Je! Nimsujudie uliye muumba kwa udongo? Maelezo

62. Akasema: Hebu nambie khabari ya huyu uliye mtukuza juu yangu. Ukiniakhirisha mpaka Siku ya Kiyama, hapana shaka nitawaangamiza dhuriya zake wasipo kuwa wachache tu. Maelezo

63. Akasema Mwenyezi Mungu: Ondokelea mbali! Atakaye kufuata katika wao, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yenu, malipo ya kutimia. Maelezo

64. Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali na wana, na waahidi. Na Shet'ani hawapi ahadi ila ya udanganyifu. Maelezo

65. Hakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu. Na Mola wako Mlezi anatosha kuwa ni wa kutegemewa. Maelezo

66. Mola wenu Mlezi ndiye anaye kuendesheeni marikebu katika bahari ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kukurehemuni nyinyi. Maelezo

67. Na inapo kufikieni taabu katika bahari, hao mnao waomba wanapotea, isipo kuwa Yeye tu. Na anapo kuvueni mkafika nchi kavu, mnageuka. Ama mwanaadamu ni mwingi wa kukanusha. Maelezo

68. Je! Mmeaminisha ya kuwa hatakudidimizeni upande wowote katika nchi kavu, au kwamba hatakuleteeni tufani la kokoto? Kisha msipate wa kumtegemea. Maelezo

69. Au mmeaminisha ya kuwa hatakurudisheni humo mara nyengine na kukupelekeeni kimbunga cha upepo akakuzamisheni kwa mlivyo kufuru, na kisha msipate wa kukunusuruni nasi. Maelezo

70. Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba. Maelezo

71. Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho - basi atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe. Maelezo

72. Na aliye kuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu Akhera, na atakuwa aliye ipotea zaidi Njia. Maelezo

73. Na hakika walikaribia kukushawishi uache tuliyo kufunulia ili utuzulie mengineyo. Na hapo ndio wangeli kufanya rafiki. Maelezo

74. Na lau kuwa hatukukuweka imara ungeli karibia kuwaelekea kidogo. Maelezo

75. Hapo basi bila ya shaka tungeli kuonjesha adhabu mardufu ya uhai, na adhabu mardufu ya kifo. Kisha usinge pata mtu wa kukunusuru nasi. Maelezo

76. Na walitaka kukukera ili uitoke nchi. Na hapo wao wasingeli bakia humo ila kwa muda mchache tu. Maelezo

77. Huo ndio mwendo kwa Mitume tulio watuma kabla yako. Wala hupati mabadiliko katika mwendo wetu. Maelezo

78. Shika Sala jua linapo pinduka mpaka giza la usiku, na Qur'ani ya al fajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa daima. Maelezo

79. Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna khasa kwako wewe. Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika. Maelezo

80. Na sema: Mola wangu Mlezi! Niingize muingizo mwema, na unitoe kutoka kwema. Na unipe nguvu zinazo toka kwako zinisaidie. Maelezo

81. Na sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke! Maelezo

82. Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara. Maelezo

83. Na mwanaadamu tunapo mneemesha hugeuka na kujitenga kando. Na inapo mgusa shari hukata tamaa. Maelezo

84. Sema: Kila mmoja anafanya kwa namna yake. Na Mola wenu Mlezi anajua aliye ongoka katika njia. Maelezo

85. Na wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu. Maelezo

86. Na tungeli penda tungeli yaondoa tuliyo kufunulia. Kisha usingeli pata mwakilishi wa kukupigania kwetu kwa haya. Maelezo

87. Isipo kuwa iwe rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika fadhila yake kwako ni kubwa. Maelezo

88. Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur'ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao. Maelezo

89. Na hakika tumewaeleza watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano. Lakini watu wengi wanakataa isipo kuwa kukanusha tu. Maelezo

90. Na walisema: Hatutakuamini mpaka ututimbulie chemchem katika ardhi hii. Maelezo

91. Au uwe na kitalu cha mitende na mizabibu, na utupitishie mito kati yake ikimiminika. Maelezo

92. Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyo dai; au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika uso kwa uso. Maelezo

93. Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni. Wala hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome. Sema: Subhana Rabbi, Ametakasika Mola wangu Mlezi! Kwani mimi ni nani isipo kuwa ni mwanaadamu na Mtume? Maelezo

94. Na nini kilicho wazuilia watu kuamini ulipo wajia uwongofu isipo kuwa walisema: Je! Mwenyezi Mungu humtuma mwanaadamu kuwa ni Mtume? Maelezo

95. Sema: Ingeli kuwa duniani wapo Malaika wanatembea kwa utulivu wao, basi bila ya shaka tungeli wateremshia Malaika kuwa ni Mtume wao. Maelezo

96. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi baina yangu na nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona. Maelezo

97. Na anaye mhidi Mwenyezi Mungu basi huyo ndiye aliye hidika. Na anaye wapotoa basi huto wapatia walinzi badala yake. Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu. Maelezo

98. Hayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa ishara zetu, na wakasema: Hivyo tukisha kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika tutafufuliwa kwa umbo jipya? Maelezo

99. Kwani hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mfano wao? Na Yeye amewawekea muda usio na shaka yoyote. Lakini madhaalimu hawataki ila ukafiri. Maelezo

100. Sema: Lau kuwa nyinyi mnazimiliki khazina za rehema za Mola wangu Mlezi, basi hapana shaka mngeli zuia kuzitumia kwa ajili ya kukhofu. Na mwanaadamu tangu hapo tabia yake ni mchoyo! Maelezo

101. Na kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi. Waulize Wana wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia: Hakika mimi nakuona wewe Musa umerogwa! Maelezo

102. Musa akasema: Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya hakuyateremsha ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa kuonekana. Na hakika mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha angamia. Maelezo

103. Basi Firauni akataka kuwafukuza katika nchi. Kwa hivyo tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote. Maelezo

104. Na tukawaambia baada yake Wana wa Israili: Kaeni katika nchi. Itapo kuja ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja. Maelezo

105. Na kwa Haki tumeiteremsha, na kwa Haki imeteremka. Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na mwonyaji. Maelezo

106. Na Qur'ani tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo. Maelezo

107. Sema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale walio pewa ilimu kabla yake, wanapo somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu. Maelezo

108. Na wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe! Maelezo

109. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu. Maelezo

110. Sema: Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu), au mwombeni Rahman (Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani Yeye ana majina mazuri mazuri. Wala usitangaze Sala yako kwa sauti kubwa, wala usiifiche kwa sauti ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo. Maelezo

111. Na sema: Alhamdulillah, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye hana mwana, wala hana mshirika katika ufalme, wala hana rafiki wa kumsaidia kwa sababu ya udhaifu wake. Na mtukuze kwa utukufu mkubwa. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani