Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani¬  (Nani Yeye?)

 

18. SURA AL KAHF

(Imeteremka Makka)

Sura hii ni ya Makka, isipo kuwa Aya 38, na Aya zinazo anzia 83 mpaka 101. Basi zimo Aya ishirini za Madina. Nayo imeanzia kwa kumhimidi Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuiteremsha Qur'ani Tukufu, na kubainisha kuwa Qur'ani ni onyo na bishara. Ndani yake lipo onyo kwa wanao dai kuwa ati Mwenyezi Mungu ana mwana. Na humu imetajwa hamu kubwa aliyo nayo Nabii ya kutaka waamini wale anao waita kwenye mlingano wa Mwenyezi Mungu.¬  Kisha kikatajwa kisa cha Ahlil Kahf, Watu wa Pangoni, walio lala usingizi kisha wakaamka baada ya kukaa katika pango lao muda wa miaka mia tatu na tena wakazidishiwa tisa. Na watu hao walikuwa Wakristo walio kuwa wakikimbia udhalimu wa mtawala wa Kirumi. Wakalala katika pango muda huo, kisha wakaamka ili kuwa ni ishara ya uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kufufua baada ya kufa.
Kisha baada ya hayo Mwenyezi Mungu akamuamrisha kusoma Qur'ani na aitumie kwa kuonya na kubashiri. Kisha imebainishwa hali ya watu wa Peponi na watu wa Motoni. Na Mwenyezi Mungu akapiga mifano ya watu wawili, mmoja tajiri anajitapa kwa mali yake na wanawe. Na wa pili anatafakhari kwa Mwenyezi Mungu wake. Na amebainisha Subhanahu kuwa ulinzi wake ndio wa Haki. Na tena Subhanahu ameeleza starehe ya duniani inayo pita, na neema ya daima au adhabu chungu ya Siku ya Kiyama. Tena Subhanahu ametaja hadithi ya Musa pamoja na Mja Mwema aliye pewa ilimu kutokana na Mwenyezi Mungu. Na katika kisa hichi inapatikana sura ya vipi mtu anaweza asijue mambo, hata akiwa Nabii Mtume katika Mitume imara - Ulul a'zmi - kwa kudra yake Mwenyezi Mungu, ila akiwa Yeye Mwenyezi Mungu akimjuulisha.¬  Tena anatajwa Dhul-qarnaini na kufika kwake mashariki ya mbali, na alivyo jenga Ukuta. Kisha yatakayo kuwa Siku ya Kiyama, na malipo ya Waumini, na ilimu ya Mwenyezi Mungu na maneno yake yasiyo malizika. Na Sura ikakhitimishia kwa kueleza Njia ya Kumridhi Subhanahu.
¬ 

 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

 

1. Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo. Maelezo

 

2. Kimenyooka sawa, ili kitoe onyo kali kutoka kwake, na kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri. Maelezo

 

3. Wakae humo milele. Maelezo

 

4. Na kiwaonye wanao nena: Mwenyezi Mungu ana mwana. Maelezo

 

5. Wao hawana ujuzi wa jambo hili, wala baba zao. Ni neno kuu hilo litokalo vinywani mwao. Hawasemi ila uwongo tu. Maelezo

 

6. Huenda ukajihiliki nafsi yako kwa ajili yao, kuwasikitikia kwa kuwa hawayaamini mazungumzo haya! Maelezo

 

7. Kwa hakika tumevifanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi. Maelezo

 

8. Na hakika Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya ardhi kuwa kama nchi ilio pigwa na ukame. Maelezo

 

9. Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu? Maelezo

 

10. Vijana hao walipo kimbilia kwenye pango walisema: Mola wetu Mlezi! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengezee uwongofu katika jambo letu. Maelezo

 

11. Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa. Maelezo

 

12. Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa. Maelezo

 

13. Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu. Maelezo

 

14. Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na wakasema: Mola wetu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita mwenginewe kabisa badala yake kuwa ni Mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka. Maelezo

 

15. Hawa watu wetu wameshika miungu mingine badala yake Yeye. Kwa nini basi hawawatolei uthibitisho ulio dhaahiri? Na nani aliye dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu? Maelezo

 

16. Na mkijitenga nao na vile wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu, basi kimbilieni pangoni, akufungulieni Mola wenu Mlezi rehema yake, na akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu. Maelezo

 

17. Na unaliona jua linapo chomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapo kuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na anaye muacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi. Maelezo

18. Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeli watokea hapana shaka ungeli geuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu. Maelezo

 

19. Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote. Maelezo

 

20. Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa! Maelezo

 

21. Na namna hivi tuliwa juulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo kuwa wakigombania jambo lao wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi anawajua vyema. Wakasema walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao. Maelezo

 

22. Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule. Maelezo

 

23. Wala usisema kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho - Maelezo

 

24. Isipo kuwa Mwenyezi Mungu akipenda. Na mkumbuke Mola wako Mlezi pale unapo sahau, na sema: Asaa Mola wangu Mlezi ataniongoa kwenye uwongozi ulio karibu zaidi kuliko huu. Maelezo

 

25. Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa. Maelezo

 

26. Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda walio kaa. Ni zake tu siri za mbingu na ardhi. Kuona kulioje na kusikia kwake! Hawana mlinzi isipo kuwa Yeye, wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake. Maelezo

 

27. Na soma uliyo funuliwa katika Kitabu cha Mola wako Mlezi. Hapana wa kubadilisha maneno yake. Wala nawe hutapata makimbilio isipo kuwa kwake. Maelezo

 

28. Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi yake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya dunia. Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka. Maelezo

 

29. Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae. Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu Moto ambao utawazunguka kama khema. Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyo tibuka. Yatayo wababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno! Na matandiko hayo ya kupumzikia ni maovu mno! Maelezo

 

30. Hakika wale walio amini na wakatenda mema - hakika Sisi hatupotezi ujira wa anaye tenda mema. Maelezo

 

31. Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito kati yake. Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri na at'ilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia! Maelezo

 

32. Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimpa vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende, na kati yake tukatia mimea ya nafaka. Maelezo

 

33. Na hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hayo kilicho tindikia. Na ndani yake tukapasua mito. Maelezo

 

34. Naye alikuwa na mazao mengi. Basi akamwambia mwenzake naye akibishana naye: Mimi nimekushinda wewe kwa mali na nguvu za watu! Maelezo

 

35. Na akaingia kitaluni kwake, naye hali anajidhulumu nafsi yake. Akasema: Sidhani kabisa kuwa haya yataharibika. Maelezo

 

36. Wala sidhani kuwa hiyo Saa (ya Kyama) itatokea. Na ikiwa nitarudishwa kwa Mola wangu Mlezi, bila ya shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya. Maelezo

 

37. Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je! Unamkufuru aliye kuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya mtu kaamili? Maelezo

 

38. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi. Wala simshirikishi na yeyote. Maelezo

 

39. Na lau kuwa ulipo ingia kitaluni kwako ungeli sema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe, Maelezo

 

40. Basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako, naye akapitisha kudra yake kutoka mbinguni kukilitea hicho chako, na kikageuka ardhi tupu inayo teleza. Maelezo

 

41. Au maji yake yakadidimia wala usiweze kuyagundua. Maelezo

 

42. Yakateketezwa matunda yake, akabaki akipindua pindua viganja vyake, kwa vile alivyo yagharimia, na miti imebwagika juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti nisingeli mshiriki Mola wangu Mlezi na yeyote! Maelezo

 

43. Wala hakuwa nacho kikundi cha kumsaidia badala ya Mwenyezi Mungu, wala mwenyewe hakuweza kujisaidia. Maelezo

 

44. Huko ulinzi ni wa Mwenyezi Mungu wa Haki tu. Yeye ndiye mbora wa malipo, na mbora wa matokeo. Maelezo

 

45. Na wapigie mfano wa maisha ya dunia. Hayo ni kama maji tunayo yateremsha kutoka mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi, kisha hiyo mimea ikawa vibuwa vinavyo peperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Maelezo

 

46. Mali na wana ni pambo la maisha ya dunia. Na mema yanayo bakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini. Maelezo

 

47. Na siku tutapo iondoa milima na ukaiona ardhi iwazi, na tukawafufua - wala hatutamwacha hata mmoja kati yao - Maelezo

 

48. Na wakahudhurishwa mbele ya Mola wako Mlezi kwa safu (wakaambiwa): Mmetujia kama tulivyo kuumbeni mara ya kwanza! Bali mlidai kwamba hatutakuwekeeni miadi. Maelezo

 

49. Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyo ogopa kwa yale yaliomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyo yatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Mlezi hamdhulumu yeyote. Maelezo

 

50. Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Walimsjudia isipo kuwa Iblisi. Yeye alikuwa miongoni mwa majini, na akavunja amri ya Mola wake Mlezi. Je! Mnamshika yeye na dhuriya zake kuwa marafiki badala yangu, hali wao ni adui zenu? Ni ovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu. Maelezo

 

51. Sikuwashuhudisha kuumbwa kwa mbingu na ardhi, wala kuumbwa kwa nafsi zao. Wala sikuwafanya wapotezao kuwa ni wasaidizi. Maelezo

 

52. Na siku atakapo sema (Mwenyezi Mungu): Waiteni hao mlio dai kuwa ni washirika wangu. Basi watawaita, na wao hawato waitikia. Nasi tutaweka baina yao maangamio. Maelezo

 

53. Na wakhalifu watauona Moto na watajua ya kwamba wao lazima wataingia humo; wala hawatapata pa kuuepuka. Maelezo

 

54. Na bila ya shaka tumewaelezea watu katika hii Qur'ani kila namna ya mfano. Lakini mwanaadamu amezidi kuliko kila kitu kwa ubishi. Maelezo

 

55. Na hapana kilicho wazuia watu kuamini ulipo wajia uwongofu na wakaomba maghfira kwa Mola wao Mlezi, isipo kuwa yawafikie ya wale wa zamani, au iwafikie adhabu jahara. Maelezo

 

56. Na hatuwatumi Mitume ila wawe wabashiri na waonyaji. Na walio kufuru wanabishana kwa uwongo, ili kwa uwongo huo waivunje kweli. Na wanazifanya Ishara zangu na yale waliyo onywa kuwa ni mzaha. Maelezo

 

57. Na ni nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye kumbushwa Ishara za Mola wake Mlezi, naye akazipuuza na akasahau yaliyo tangulizwa na mikono yake? Hakika Sisi tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao ili wasifahamu, na uziwi kwenye masikio yao. Na ukiwaita kwenye uwongofu hawakubali kabisa kuongoka. Maelezo

 

58. Na Mola wako Mlezi ni Msamehevu Mwenye rehema. Lau angeli wachukulia kwa mujibu waliyo yachuma, bila ya shaka angeli wafanyia haraka kuwaadhibu. Lakini wanayo miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya kuepukana nayo. Maelezo

 

59. Na miji hiyo tuliwaangamiza watu wake walipo dhulumu. Na tukawawekea miadi ya maangamizo yao. Maelezo

 

60. Na pale Musa alipo mwambia kijana wake: Sitoacha kuendelea mpaka nifike zinapo kutana bahari mbili, au nitaendelea kwa muda mrefu. Maelezo

 

61. Basi wawili hao walipo fika zinapo kutana hizo bahari mbili walimsahau samaki wao, naye akashika njia yake kaporonyokea baharini. Maelezo

 

62. Walipo kwisha pita alimwambia kijana wake: Tupe chakula chetu cha mchana. Kwa hakika tumepata machofu kweli kwa hii safari yetu. Maelezo

 

63. Akasema (kijana): Waona! Pale tulipo pumzika penye jabali basi mimi nilimsahau yule samaki. Na hapana aliye nisahaulisha nisimkumbuke ila Shet'ani tu. Naye akashika njia yake baharini kwa ajabu. Maelezo

 

64. (Musa) akasema: Hayo ndiyo tuliyo kuwa tunayataka. Basi wakarudi nyuma kwa kufuata njia waliyo jia. Maelezo

 

65. Basi wakamkuta mja katika waja wangu tuliye mpa rehema kutoka kwetu, na tukamfunza mafunzo yaliyo toka kwetu. Maelezo

 

66. Musa akamwambia: Nikufuate ili unifunze katika ule uwongofu ulio funzwa wewe? Maelezo

 

67. Akasema: Hakika wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami. Maelezo

 

68. Na utawezaje kuvumilia yale usiyo yajua vilivyo undani wake? Maelezo

 

69. Akasema: Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, utaniona mvumilivu, wala sitoasi amri yako. Maelezo

 

70. Akasema: Basi ukinifuata usiniulize kitu mpaka mimi nianze kukutajia. Maelezo

 

71. Basi wawili hao wakatoka, hata walipo panda jahazi (yule mtu) akaitoboa. (Musa) akasema: Unaitoboa uwazamishe watu wake? Hakika umefanya jambo baya. Maelezo

 

72. Akasema: Sikukwambia hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami? Maelezo

 

73. (Musa) akasema: Usinichukulie kwa niliyo sahau, wala usinipe uzito kwa jambo langu. Maelezo

 

74. Basi wakatoka wawili hao mpaka wakamkuta kijana, akamuuwa. (Musa) akasema: Ala! Umemuuwa mtu asiye na kosa, na wala hakuuwa! Ama hakika umefanya jambo baya kabisa! Maelezo

 

75. AKASEMA: Je! Sikukwambia kwamba hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami? Maelezo

 

76. Akasema: Nikikuuliza kitu chochote baada ya haya usifuatane nami, kwani umekwisha pata udhuru kwangu. Maelezo

 

77. Basi wakatoka mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja. Wakawaomba watu wake wawape chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, (yule mja mwema) akausimamisha. (Musa) akasema: Ungeli taka ungeli chukua ujira kwa haya. Maelezo

 

78. (Yule mtu) akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Sasa nitakueleza maana ya yale uliyo kuwa huwezi kuyastahamilia. Maelezo

 

79. Ama ile jahazi ilikuwa ya masikini za Mungu wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuiharibu, kwani nyuma yao alikuwako mfalme anaghusubu majahazi yote. Maelezo

 

80. Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa ni Waumini. Tukakhofu asije watia mashakani kwa uasi na ukafiri. Maelezo

 

81. Basi tulitaka Mola wao Mlezi awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma. Maelezo

 

82. Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako khazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima na wajitolee khazina yao wenyewe, kuwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria. Maelezo

 

83. Na wanakuuliza khabari za Dhul- Qarnaini. Waambie: Nitakusimulieni baadhi ya hadithi yake. Maelezo

 

84. Sisi tulimtilia nguvu katika ardhi na tukampa njia za kila kitu. Maelezo

 

85. Basi akaifuata njia. Maelezo

 

86. Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika checmchem yenye matope meusi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema. Maelezo

 

87. Akasema: Ama aliye dhulumu basi tutamuadhibu, na kisha atarudishwa kwa Mola wake Mlezi amuadhibu adhabu isiyo juulikana. Maelezo

 

88. Na ama aliye amini na akatenda mema basi atapata malipo mazuri. Nasi tutamwambia lilio jepesi katika amri yetu. Maelezo

 

89. Kisha akaifuata njia. Maelezo

 

90. Hata alipo fika matokeo ya jua aliliona linawachomozea watu tusio wawekea pazia la kuwakinga nalo. Maelezo

 

91. Ndio hivyo hivyo. Na Sisi tulizijua vilivyo khabari zake zote. Maelezo

 

92. Kisha akaifuata njia. Maelezo

 

93. Hata alipo fika baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wanafahamu lolote. Maelezo

 

94. Wakasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Hakika Juju-wa-maajuju wanafanya uharibifu katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome? Maelezo

 

95. Akasema: Yale Mola wangu aliyo niwezesha ni bora zaidi. Lakini nyinyi nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitakujengeeni kizuizi baina yenu na wao. Maelezo

 

96. Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya (chuma) kama moto akasema: Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie. Maelezo

 

97. Basi hawakuweza kuukwea, wala hawakuweza kuutoboa. Maelezo

 

98. Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu Mlezi. Na itapo fika ahadi ya Mola wangu Mlezi atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola wangu Mlezi ni kweli tu. Maelezo

 

99. Na siku hiyo tutawaacha wakisongana wao kwa wao. Na baragumu litapulizwa, na wote watakusanywa pamoja. Maelezo

 

100. Na siku hiyo tutawadhihirishia wazi Jahannamu makafiri waione. Maelezo

 

101. Wale ambao kwamba macho yao yalikuwa paziani hayanikumbuki, na wakawa hawawezi kusikia. Maelezo

 

102. Je, wanadhani walio kufuru ndio wawafanye waja wangu ndio walinzi wao badala yangu Mimi? Hakika Sisi tumeiandaa Jahannamu iwe ndipo mahala pa kuteremkia makafiri. Maelezo

 

103. Sema: Je, tukutajieni wenye khasara mno katika vitendo vyao? Maelezo

 

104. Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri. Maelezo

 

105. Hao ni wale walio zikanusha Ishara za Mola wao Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya Kiyama hatutawathamini kitu. Maelezo

 

106. Hiyo Jahannamu ni malipo yao kwa walivyo kufuru na wakafanyia kejeli Ishara zangu na Mitume wangu. Maelezo

 

107. Hakika wale walio amini na wakatenda mema mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi. Maelezo

 

108. Watadumu humo; hawatataka kuondoka. Maelezo

 

109. Sema: Lau kuwa bahari ndio wino kwa maneno ya Mola wangu Mlezi, basi bahari ingeli malizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu Mlezi, hata tungeli ileta mfano wa hiyo kuongezea. Maelezo

 

110. Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi. Ninaletewa Wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi naatende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi. Maelezo ¬ ¬ 


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani