Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

19. SURAT MARYAM

(Imeteremka Makka)

 

Hii ni Sura iliyo teremka Makka, na hamna Aya za Madina ila Aya 57 na 71. Hisabu ya Aya zake ni 98. Imeanzia kwa harufi moja moja kama Sura nyingi nyenginezo. Ndani ya Sura hii kipo kisa cha kuzaliwa Yahya bin Zakariya (Alayhima Ssalam). Zakariya alitamani mwana na hali kesha fikilia ukongwe na mkewe ni tasa. Na kimetajwa pia kisa cha Bibi Bikra Maryam (A.S.) na kumzaa kwake Masihi (A.S.). Kisha kikatajwa kisa cha Ibrahim (A.S) na Wito wake kulingania Upweke wa Mwenyezi Mungu, na alivyo mtaka babaake aache kuabudu masanamu, na majibizano yao yaliyo jiri kwa ajili ya masanamu, na madaraka ya Shet'ani.
Pia wameashiriwa Manabii wengine katika dhuriya za Ibrahim, nao Ismail na Is-haq na dhuriya wa Is-haq. Tena kikagusiwa kisa cha Idris (A.S.).  Na tena Mwenyezi Mungu Subhanahu akataja khabari za walio fuatia wakaja baada ya Manabii, watu wat'iifu na wengine maasi. Na akataja kuwa Pepo ndiyo malipo ya Waumini, na Moto ni malipo ya makafiri, na akazitaja hali za makafiri katika Jahannamu. Na tena Subhanahu akagusia ya wapotovu wanao sema kwamba Mwenyezi Mungu ana mwana.
Na Subhanahu amebainisha cheo cha Qur'ani, na amewaonya makafiri, na amepiga mifano ya watavyo teketea wanao waasi Manabii. Na akaashiria kwamba hao wamepotea kabisa, hawakuacha hata ukumbusho.
 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Kaf Ha Ya A'yn S'ad Maelezo

2. Huu ni Ukumbusho wa rehema ya Mola wako Mlezi kwa mja wake, Zakariya. Maelezo

3. Alipo mwita Mola wake Mlezi kwa siri. Maelezo

4. Akasema: Mola wangu Mlezi! Mafupa yangu yamedhoofika, na kichwa kinameremeta kwa mvi; wala, Mola wangu Mlezi, sikuwa mwenye bahati mbaya kwa kukuomba Wewe. Maelezo

5. Na hakika mimi nawakhofia jamaa zangu baada yangu. Na mke wangu ni tasa. Basi nipe mrithi kutoka kwako. Maelezo

6. Atakaye nirithi mimi na awarithi ukoo wa Yaaqub. Ewe Mola wangu Mlezi! Na umjaalie awe mwenye kuridhisha. Maelezo

7. (Akaambiwa): Ewe Zakariya! Hakika Sisi tunakubashiria mwana; jina lake ni Yahya. Hatujapata kumpa jina hilo yeyote kabla yake. Maelezo

8. Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi nitakuwa na mwana na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimesha fikia ukongwe katika uzee? Maelezo

9. Akasema: Ndio hivyo hivyo amesema Mola wako Mlezi: Haya ni mepesi kwangu. Na hakika Mimi nilikwisha kuumba wewe zamani na hali hukuwa kitu. Maelezo

10. Akasema: Mola wangu Mlezi nijaalie Ishara. Akasema Ishara yako ni kuwa hutasema na watu kwa masiku matatu, na hali ni mzima. Maelezo

11. Basi akawatokea watu wake kutoka mihirabuni. Akawaashiria: Msabihini Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni. Maelezo

12. Ewe Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu! Nasi tulimpa hikima angali mtoto. Maelezo

13. Na tukampa huruma itokayo kwetu, na utakaso, na akawa mchamungu. Maelezo

14. Na akawa mwema kwa wazazi wake, wala hakuwa jabari mua'si. Maelezo

15. Na amani iwe juu yake siku ya kuzaliwa, na siku ya kufa, na siku ya kufufuliwa. Maelezo

16. Na mtaje Maryamu katika Kitabu, pale alipo jitenga na jamaa zake mahali upande wa mashariki; Maelezo

17. Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea Roho wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu. Maelezo

18. (Maryamu) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa Rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mchamngu. Maelezo

19. (Malaika) akasema: Hakika mimi ni mwenye kutumwa na Mola wako Mlezi ili nikubashirie tunu ya mwana aliye takasika. Maelezo

20. Akasema: Nitampataje mwana hali mwanaadamu yeyote hajanigusa, wala mimi si kahaba? Maelezo

21. (Malaika) akasema: Ndio hivyo hivyo! Mola wako Mlezi amesema: Haya ni mepesi kwangu! Na ili tumfanye kuwa ni Ishara kwa watu, na Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lilio kwisha hukumiwa. Maelezo

22. Basi akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mpaka mahali pa mbali. Maelezo

23. Kisha uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende; akasema: Laiti ningeli kufa kabla ya haya, na nikawa niliye sahaulika kabisa! Maelezo

24. Pakatangazwa kutoka chini yake: Usihuzunike! Hakika Mola wako Mlezi amejaalia chini yako kijito kidogo cha maji! Maelezo

25. Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu. Maelezo

26. Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu. Maelezo

27. Akenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu! Maelezo

28. Ewe dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba. Maelezo

29. Akawaashiria (mtoto). Wakasema: Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi? Maelezo

30. (Mtoto) akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu, na amenifanya Nabii. Maelezo

31. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai, Maelezo

32. Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu. Maelezo

33. Na amani iko juu yangu siku niliyo zaliwa, na siku nitakayo kufa, na siku nitakayo fufuliwa kuwa hai. Maelezo

34. Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka. Maelezo

35. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapo lihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa. Maelezo

36. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

37. Lakini makundi yakakhitalifiana wao kwa wao. Basi ole wao hao walio kufuru kwa kuhudhuria Siku iliyo kuu! Maelezo

38. Watasikia na wataona vizuri vilioje Siku watakayo tufikia! Lakini madhaalimu sasa wamo katika upotofu ulio dhaahiri. Maelezo

39. Na waonye siku ya majuto itapo katwa amri. Nao wamo katika ghafla, wala hawaamini. Maelezo

40. Hakika Sisi tutairithi ardhi na walio juu yake. Na kwetu watarejeshwa. Maelezo

41. Na mtaje katika Kitabu Ibrahim. Hakika yeye alikuwa mkweli, Nabii. Maelezo

42. Alipo mwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyo sikia, na visivyo ona, na visivyo kufaa chochote? Maelezo

43. Ewe baba yangu! Kwa yakini imenifikia ilimu isiyo kufikia wewe. Basi nifuate mimi, nami nitakuongoza Njia Iliyo Sawa. Maelezo

44. Ewe baba yangu! Usimuabudu Shet'ani. Hakika Shet'ani ni mwenye kumuasi Mwingi wa Rehema. Maelezo

45. Ewe baba yangu! Hakika mimi naogopa isikupate adhabu inayo toka kwa Mwingi wa Rehema ukaja kuwa mwenziwe Shet'ani. Maelezo

46. (Baba) akasema: Unaichukia miungu yangu, ewe Ibrahim? Kama huachi, basi lazima nitakupiga mawe. Na niondokelee mbali kwa muda! Maelezo

47. (Ibrahim) akasema: Salamun a'laika! Amani iwe juu yako! Mimi nitakuombea msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ananihurumia sana. Maelezo

48. Nami najitenga nanyi na hayo mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Na ninamwomba Mola wangu Mlezi; asaa nisiwe mwenye kukosa bahati kwa kumwomba Mola wangu Mlezi. Maelezo

49. Basi alipo jitenga nao na yale waliyo kuwa wakiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, tulimpa Is-haq na Yaaqub, na kila mmoja tukamfanya Nabii. Maelezo

50. Na tukawapa rehema zetu na tukawajaalia kupewa sifa za kweli tukufu. Maelezo

51. Na mtaje Musa katika Kitabu. Hakika yeye alikuwa ni mwenye kuchaguliwa, na alikuwa Mtume, Nabii. Maelezo

52. Na tulimwita upande wa kulia wa mlima na tukamsogeza kunong'ona naye. Maelezo

53. Nasi kwa rehema zetu tukampa nduguye, Harun, awe Nabii. Maelezo

54. Na mtaje katika Kitabu Ismail. Bila ya shaka yeye alikuwa ni mkweli wa ahadi, na alikuwa Mtume, Nabii. Maelezo

55. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake Sala na Zaka, na alikuwa mbele ya Mola wake Mlezi mwenye kuridhiwa. Maelezo

56. Na mtaje katika Kitabu Idris. Hakika yeye alikuwa ni mkweli Nabii. Maelezo

57. Na tulimuinua daraja ya juu. Maelezo

58. Hao ndio alio waneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii katika uzao wa Adam, na katika uzao wa wale tulio wapandisha pamoja na Nuhu, na katika uzao wa Ibrahim na Israil, na katika wale tulio waongoa na tukawateuwa. Wanapo somewa Aya za Mwingi wa Rehema huanguka kusujudu na kulia. Maelezo

59. Lakini wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha Sala, na wakafuata matamanio. Basi watakuja kuta malipo ya ubaya. Maelezo

60. Isipo kuwa walio tubu, wakaamini, na wakatenda mema. Hao, basi, wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa chochote. Maelezo

61. Bustani za milele alizo waahidi Rahmani waja wake katika siri. Hakika ahadi yake hapana shaka itafika. Maelezo

62. Humo hawatasikia upuuzi, ila Salama tu. Na watapata humo riziki zao asubuhi na jioni. Maelezo

63. Hiyo ndiyo Pepo tutayo warithisha katika waja wetu walio kuwa wachamngu. Maelezo

64. (Nao watasema:) Wala hatuteremki ila kwa amri ya Mola wako Mlezi. Ni yake Yeye yaliyoko mbele yetu na yaliyoko nyuma yetu, na yaliyomo katikati ya hayo. Na Mola wako Mlezi si mwenye kusahau. Maelezo

65. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake. Basi muabudu Yeye tu, na udumu katika ibada yake. Je, mnamjua mwenye jina kama lake? Maelezo

66. Na mwanaadamu husema: Hivyo, nitakapo kufa, ni kweli nitafufuliwa niwe hai tena? Maelezo

67. Je! Hakumbuki mwanaadamu ya kwamba tulimuumba kabla, na hali hakuwa chochote? Maelezo

68. Basi naapa kwa Mola wako Mlezi! Kwa yakini tutawakusanya wao pamoja na mashet'ani; kisha tutawahudhurisha kuizunguka Jahannamu, nao wamepiga magoti! Maelezo

69. Kisha kwa yakini tutawatoa katika kila kundi wale miongoni mwao walio zidi kumuasi Arrahmani, Mwingi wa Rahema.. Maelezo

70. Tena hakika Sisi tunawajua vyema zaidi wanao stahiki kuunguzwa humo. Maelezo

71. Wala hapana yeyote katika nyinyi ila ni mwenye kuifikia. Hiyo ni hukumu ya Mola wako Mlezi ambayo lazima itimizwe. Maelezo

72. Kisha tutawaokoa wale walio mchamngu; na tutawaacha madhaalimu humo wamepiga magoti. Maelezo

73. Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, walio kufuru huwaambia walio amini: Lipi katika makundi mawili lenye cheo kizuri na lilio bora barazani? Maelezo

74. Na kaumu ngapi tuliziangamiza zilizo kuwa na mapambo mazuri zaidi na wazuri zaidi kwa kuwatazama! Maelezo

75. Sema: Walio katika upotofu basi Arrahmani Mwingi wa Rahema atawapururia muda mpaka wayaone waliyo onywa - ama ni adhabu au ni Saa. Hapo ndipo watapo jua ni nani mwenye makao mabaya na mwenye askari dhaifu. Maelezo

76. Na Mwenyezi Mungu huwazidishia uwongofu wenye kushika uwongofu. Na mema yenye kudumu ni bora katika malipo mbele ya Mola wako Mlezi na yana mwisho mwema. Maelezo

77. Je, umemwona aliye zikanya Ishara zetu na akasema: Kwa hakika mimi nitapewa mali na wana! Maelezo

78. Kwani yeye amepata khabari za ghaibu, au amechukua ahadi kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema? Maelezo

79. Hasha! Tutaandika anayo yasema, tutamkunjulia muda wa adhabu. Maelezo

80. Na tutamrithi hayo anayo yasema, na atatufikia mtupu peke yake! Maelezo

81. Na wamechukua miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati iwape nguvu. Maelezo

82. Sivyo kabisa! Wataikataa hiyo ibada yao, na watakuwa ndio dhidi yao. Maelezo

83. Kwani huoni ya kwamba tumewatuma mashet'ani kwa makafiri wawachochee kwa uchochezi? Maelezo

84. Basi usiwafanyie haraka. Sisi tunawahisabia idadi ya siku zao. Maelezo

85. Siku tutayo wakusanya wachamngu kuwapeleka kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema kuwa ni wageni wake. Maelezo

86. Na tukawachunga wakhalifu kuwapeleka Jahannamu hali ya kuwa wana kiu. Maelezo

87. Hawatakuwa na mamlaka ya uombezi ila wale walio chukua ahadi kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema.. Maelezo

88. Na wao ati husema kuwa Arrahmani Mwingi wa Rehema ana mwana! Maelezo

89. Hakika mmeleta jambo la kuchusha mno! Maelezo

90. Zinakaribia mbingu kutatuka kwa hilo, na ardhi kupasuka, na milima kuanguka vipande vipande. Maelezo

91. Kwa kudai kwao kuwa Arrahmani Mwingi wa Rehema ana mwana. Maelezo

92. Wala hahitajii Arrahmani Mwingi wa Rehema kuwa na mwana. Maelezo

93. Hapana yeyote aliomo mbinguni na ardhini ila atafika kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema kuwa ni mtumwa wake. Maelezo

94. Yeye hakika amewadhibiti na amewahisabu sawa sawa. Maelezo

95. Na kila mmoja katika wao atamfikia Siku ya Kiyama peke yake. Maelezo

96. Hakika walio amini na wakatenda mema Arrahmani Mwingi wa Rehema atawajaalia mapenzi. Maelezo

97. Na hakika tumeifanya nyepesi (Qur'ani) kwa ulimi wako, ili uwabashirie kwayo wachamngu, na uwaonye kwayo watu wabishi. Maelezo

98. Na kaumu ngapi tumezihiliki kabla yao. Je! Unawaona hata mmoja katika wao au unasikia hata mchakato wao? Maelezo


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani