Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

20. SURAT T'AHA

(Imeteremka Makka)

 

SURA HII ni ya Makka, isipo kuwa Aya mbili, nazo ni Aya 130 na 131. Hisabu ya Aya zake ni 135. Sura hii imeanza kwa harufi mbili za kuzindua juu ya muujiza wa Qur'ani, na kuwazindua wasikilizaji waisikilize. Baada ya harufi hizo mbili cheo cha Qur'ani kimetajwa, na utukufu wa hii Qur'ani ni utukufu wa Mwenye kuileta, naye ni Mwenyezi Mungu, Subhanahu wa Taa'la, Mmiliki mbingu na ardhi, Mwenye kujua siri, na kilicho fichikana kuliko siri. Kisha kimesimuliwa kisa cha Musa a.s. pamoja na Firauni, na vipi alipo anza kupewa utume Nabii Musa a.s. Na yametajwa maombi yake kutaka nduguye Harun a.s. awe msaidizi wake wa kumpa nguvu, tena vipi walivyo kutana  na Firauni baada ya kitisho cha mkutano wake kwa ajili ya ujeuri wake. Na katika mintarafu ya haya Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha kuzuka kwa Musa a.s.
Katika Sura hii pana majibizano baina ya Musa na Firauni, tena baina ya Musa a.s. na wachawi, na hali ya Musa ya kuogopa kushindwa mbele ya wachawi, na fimbo yake ilipo zimeza kamba zao, na tena mwisho vipi yalivyo ishia mambo ya wachawi na kuamini kwao, na Firauni kuwaadhibu. Kisha ikatajwa vipi Musa alivyo  toka yeye na Wana wa Israili kutokana na Firauni, na vipi alivyo zama Firauni, naye alikuwa kawafuatia baada ya kupasuka bahari; na vipi Musa aliokoka akafika Jabal T'ur akawaacha watu wake ili ende kwenye mlima kuzungumza na Mola wake Mlezi. Na Msamaria akawafitini kwa kuwachochea waliabudu sanamu la ndama lililo undwa kwa dhahabu. Na ilikuwa ukipita upepo ndani yake hutoa sauti. Musa alikasirika kwa yaliyo tokea, akamkamata kichwa nduguye akimvutia kwake.
Kisha katika Sura hii tukufu  yakatokea yaliyo msibu Msamaria. Mwenyezi Mungu Subhanahu amesimulia hadithi ya kuvuka katika hadithi za Musa na nyenginezo. Na mwisho wa Sura pana mausio mema juu ya Subira, na Usamehevu, na Sala. Kisha ikabainishwa kubwatika washirikina katika matakwa yao ya muujiza mwengine usio huu wa Qur'ani; na Subhanahu ameashiria hikima ya kuwatuma Mitume. Tena Sura hii tukufu imekhitimisha kwa kuashiria adhabu watakayo pata makafiri, na malipo mema watakayo pata Waumini.
 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. T'AHA! Maelezo

2. Hatukukuteremshia Qur'ani ili upate mashaka. Maelezo

3. Bali ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea. Maelezo

4. Materemsho yatokayo kwa aliye umba ardhi na mbingu zilizo juu. Maelezo

5. Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliye tawala juu ya Kiti cha Enzi. Maelezo

6. Ni vyake vyote viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na viliomo baina yao, na viliomo chini ya ardhi. Maelezo

7. Na ukinyanyua sauti kwa kusema...basi hakika Yeye anajua siri na duni kuliko siri. Maelezo

8. Mwenyezi Mungu! Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Yeye ana majina mazuri kabisa. Maelezo

9. Na je! Imekufikia hadithi ya Musa? Maelezo

10. Alipo uona moto, akawaambia watu wake: Ngojeni! Mimi nimeuona moto, huenda nikakuleteeni kijinga kutoka huo moto, au nikapata uongofu kwenye moto. Maelezo

11. Basi alipo ufikia akaitwa: Ewe Musa! Maelezo

12. Hakika Mimi ndiye Mola wako Mlezi! Basi vua viatu vyako. Kwani upo katika bonde takatifu la T'uwa. Maelezo

13. Nami nimekuteua wewe; basi sikiliza unayo funuliwa. Maelezo

14. Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi. Maelezo

15. Hakika Saa itakuja bila ya shaka. Nimekaribia kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyo yafanya. Maelezo

16. Kwa hivyo asikukengeushe nayo yule ambaye haiamini na akafuata pumbao lake ukaja kuhiliki. Maelezo

17. Na nini hicho kilichomo mkononi mwako wa kulia, ewe Musa? Maelezo

18. Akasema: Hii ni fimbo yangu; naiegemea na ninawaangushia majani kondoo na mbuzi wangu. Tena inanifaa kwa matumizi mengine. Maelezo

19. Akasema: Itupe, ewe Musa! Maelezo

20. Akaitupa. Mara ikawa nyoka anaye kwenda mbio. Maelezo

21. Akasema: Ikamate, wala usiogope! Tutairudisha hali yake ya kwanza. Maelezo

22. Na uambatishe mkono wako kwenye ubavu. Utatoka mweupe pasipo kuwa na madhara yoyote. Hiyo ni ishara nyengine. Maelezo

23. Ili tukuonyeshe baadhi ya ishara zetu kubwa. Maelezo

24. Nenda kwa Firauni; kwani hakika yeye amepindukia mipaka. Maelezo

25. (Musa) akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nikunjulie kifua changu, Maelezo

26. Na unifanyie nyepesi kazi yangu, Maelezo

27. Na ulifungue fundo lililo katika ulimi wangu, Maelezo

28. Wapate kufahamu maneno yangu. Maelezo

29. Na nipe waziri katika watu wangu, Maelezo

30. Harun, ndugu yangu. Maelezo

31. Kwake yeye niongeze nguvu zangu. Maelezo

32. Na umshirikishe katika kazi yangu. Maelezo

33. Ili tukutakase sana. Maelezo

34. Na tukukumbuke sana. Maelezo

35. Hakika Wewe unatuona. Maelezo

36. Akasema: Hakika Umepewa maombi yako, ewe Musa! Maelezo

37. Na hakika tulikwisha kufanyia hisani mara nyengine... Maelezo

38. Pale tulipo mfunulia mama yako yaliyo funuliwa, Maelezo

39. Ya kuwa mtie katika kisanduku, na kisha kitie mtoni, na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu naye ni adui yake. Na nimekutilia mapenzi yanayo tokana kwangu, na ili ulelewe machoni mwangu. Maelezo

40. Dada yako alipo kwenda na akasema: Je! Nikujuulisheni mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurejesha kwa mama yako ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ulimuuwa mtu, nasi tukakuokoa katika dhiki, na tukakujaribu kwa majaribio mengi. Ukakaa miaka kwa watu wa Madyana. Kisha ukaja kama ilivyo kadiriwa, ewe Musa! Maelezo

41. Na nimekuteuwa kwa ajili ya nafsi yangu. Maelezo

42. Nenda, wewe na ndugu yako, pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka. Maelezo

43. Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka. Maelezo

44. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa. Maelezo

45. Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri. Maelezo

46. Akasema: Msiogope! Hakika Mimi ni pamoja nanyi. Nasikia na ninaona. Maelezo

47. Basi mwendeeni, na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola wako Mlezi! Basi waache Wana wa Israili watoke nasi, wala usiwaadhibu. Sisi tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na amani itakuwa juu ya aliye fuata uwongofu. Maelezo

48. Hakika tumefunuliwa sisi kwamba hapana shaka adhabu itamsibu anaye kadhibisha na akapuuza. Maelezo

49. (Firauni) akasema: Basi Mola wenu Mlezi ni nani, ewe Musa? Maelezo

50. Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoa. Maelezo

51. Akasema: Nini hali ya karne za kwanza? Maelezo

52. Akasema: Ilimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi katika Kitabu. Mola wangu Mlezi hapotei wala hasahau. Maelezo

53. Ambaye amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na akakupitishieni humo njia, na akakuteremshieni kutoka mbinguni maji. Na kwa hayo tukatoa namna mbali mbali za mimema. Maelezo

54. Kuleni, na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili. Maelezo

55. Kutokana nayo (ardhi) tumekuumbeni, na humo tunakurudisheni, na kutoka humo tutakutoeni mara nyengine. Maelezo

56. Na hakika tulimwonyesha ishara zetu zote. Lakini alikadhibisha na akakataa. Maelezo

57. Akasema: Ewe Musa! Hivyo umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako? Maelezo

58. Basi sisi hakika tutakueletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe, ambayo tusiivunje sisi wala wewe, mahali patapo kuwa sawa. Maelezo

59. Akasema: Miadi yenu ni siku ya Sikukuu; na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri. Maelezo

60. Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja. Maelezo

61. Musa akamwambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na mwenye kuzua lazima ashindwe! Maelezo

62. Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe, na wakanong'ona kwa siri. Maelezo

63. Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wao, na waondoe mila zenu zilizo bora kabisa. Maelezo

64. Kwa hivyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu kweli kweli leo atakaye shinda. Maelezo

65. Wakasema: Ewe Musa! Je! Utatupa wewe, au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa? Maelezo

66. Akasema: Bali tupeni nyinyi! Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio. Maelezo

67. Basi Musa akaingia khofu nafsi yake. Maelezo

68. Tukasema: Usikhofu! Hakika wewe ndiye utakaye shinda. Maelezo

69. Na kitupe kilicho katika mkono wako wa kulia; kitavimeza walivyo viunda. Hakika walivyo unda ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo. Maelezo

70. Basi wachawi wakaangushwa wanasujudu. Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa Harun na Musa! Maelezo

71. (Firauni) akasema: Oh! Mnamuamini kabla sijakupeni ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliye kufundisheni uchawi. Basi kwa yakini nitakukateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakutundikeni misalabani katika vigogo vya mitende, na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi aliye mkali wa kuadhibu na kuiendeleza adhabu yake. Maelezo

72. Wakasema: Hatutokukhiari wewe kuliko ishara waziwazi zilizo tujia, na kuliko yule aliye tuumba. Basi hukumu utavyo hukumu; kwani wewe unahukumu haya ya maisha ya duniani tu. Maelezo

73. Hakika sisi tumemuamini Mola wetu Mlezi ili atusamehe makosa yetu na uchawi ulio tulazimisha kuufanya. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na Mwenye kudumu zaidi. Maelezo

74. Hakika ataye mjia Mola wake Mlezi naye ni mkhalifu, basi kwa yakini, yake huyo ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi. Maelezo

75. Na atakaye mjia naye ni Muumini aliye tenda mema, basi hao ndio wenye vyeo vya juu. Maelezo

76. Bustani za milele zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa. Maelezo

77. Na tulimfunulia Musa: Toka usiku na waja wangu, na uwapigie njia kavu baharini. Usikhofu kukamatwa, wala usiogope. Maelezo

78. Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake. Basi kiliwafudikiza humo baharini kilicho wafudikiza. Maelezo

79. Na Firauni aliwapoteza watu wake wala hakuwaongoa. Maelezo

80. Enyi Wana wa Israili! Hakika tulikuokoeni na adui yenu, na tukakuahidini upande wa kulia wa mlima. Na tulikuteremshieni Manna na Salwa. Maelezo

81. Kuleni katika vitu vizuri hivyo tulivyo kuruzukuni, wala msiruke mipaka katika hayo, isije ikakushukieni ghadhabu yangu. Na inaye mshukia ghadhabu yangu basi huyo ameangamia. Maelezo

82. Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anaye tubia, na akaamini, na akatenda mema, tena akaongoka. Maelezo

83. Na nini kilicho kutia haraka ukawaacha watu wako, ewe Musa? Maelezo

84. Akasema: Hao wapo nyuma yangu wananifuatia. Na nimefanya haraka kukujia, Mola wangu Mlezi, ili uridhike. Maelezo

85. (Mwenyezi Mungu) akasema: Sisi tumewatia mtihani watu wako baada yako, na Msamaria amewapoteza. Maelezo

86. Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu Mlezi hakukuahidini ahadi nzuri? Je, umekuwa muda mrefu kwenu au mmetaka ikushukieni ghadhabu ya Mola wenu Mlezi, ndio maana mkavunja miadi yangu? Maelezo

87. Wakasema: Sisi hatukuvunja miadi yako kwa khiari yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya mapambo ya watu, basi tukaitupa. Na hivyo ndivyo alivyo toa shauri Msamaria. Maelezo

88. Na akawaundia ndama, kiwiliwili chenye sauti. Na wakasema: Huyu ndiye mungu wenu, na mungu wa Musa, lakini alisahau. Maelezo

89. Je! Hawakuona kuwa hakuwarudishia neno, wala hakuweza kuwadhuru wala kuwafaa? Maelezo

90. Na hakika Harun alikwisha waambia kabla yake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmetiwa mtihanini tu kwa kitu hiki. Na kwa yakini Mola wenu Mlezi ni Arrahmani, Mwingi wa Rehema. Basi nifuateni mimi, na t'iini amri yangu! Maelezo

91. Wakasema: Hatutaacha kumuabudu mpaka Musa atapo rejea kwetu. Maelezo

92. (Musa) akasema: Ewe Harun! Ni nini kilicho kuzuia, ulipo waona wamepotea, Maelezo

93. Hata usinifuate? Je, umeasi amri yangu? Maelezo

94. Akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu zangu, wala kichwa changu. Kwa hakika naliogopa usije sema: Umewafarikisha Wana wa Israil, na hukungojea kauli yangu. Maelezo

95. (Musa) akasema: Ewe Msamaria! Unataka nini ? Maelezo

96. Akasema: Niliona wasiyo yaona wao, nikashika gao katika unyao wa Mtume. Kisha nikalitupa. Na hivi ndivyo ilivyo nielekeza nafsi yangu. Maelezo

97. (Musa) akasema: Basi ondoka! Na kwa yakini utakuwa katika maisha ukisema: Usiniguse. Na hakika una ahadi kwako isiyo vunjwa. Na mtazame huyo mungu wako uliye endelea kumuabudu - Sisi kwa hakika tutamchoma moto, kisha tutamtawanya baharini atawanyike. Maelezo

98. Hakika Mungu wenu ni Allah, Mwenyezi Mungu, tu. Hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Ujuzi wake umeenea kila kitu. Maelezo

99. Namna hivi tunakuhadithia katika khabari za yaliyo tangulia. Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha ya kukumbukwa. Maelezo

100. Atakaye jitenga nayo, basi kwa yakini Siku ya Kiyama atabeba mzigo. Maelezo

101. Wadumu humo. Na ni mzigo muovu kwao kuubeba Siku ya Kiyama! Maelezo

102. Siku litakapo pulizwa barugumu, na tukawakusanya wakhalifu Siku hiyo, hali macho yao ya kibuluu. Maelezo

103. Watanong'onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku kumi tu. Maelezo

104. Sisi tunajua zaidi watakayo yasema, atakapo sema mbora wao katika mwendo: Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu. Maelezo

105. Na wanakuuliza khabari za milima. Waambie: Mola wangu Mlezi ataivuruga vuruga. Maelezo

106. Na ataiacha tambarare, uwanda. Maelezo

107. Hutaona humo mdidimio wala muinuko. Maelezo

108. Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu. Na sauti zote zitamnyenyekea Arrahmani Mwingi wa Rahema. Basi husikii ila mchakato na mnong'ono. Maelezo

109. Siku hiyo uombezi haufai kitu, ila wa aliye mruhusu Arrahmani Mwingi wa Rehema na akamridhia kusema. Maelezo

110. Yeye anajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao. Wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo. Maelezo

111. Na zitadhalilika nyuso mbele ya Aliye Hai Milele, Mwangalizi Mkuu. Na atakuwa ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma. Maelezo

112. Na anaye tenda mema, naye ni Muumini, basi hatakhofu kudhulumiwa wala kupunjwa. Maelezo

113. Na namna hivi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu, na tumekariri humo maonyo ili wapate kuogopa na kujilinda na iwaletee makumbusho. Maelezo

114. Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki. Wala usiifanyie haraka hii Qur'ani, kabla haujamalizika ufunuo wake. Na sema: Mola wangu Mlezi! Nizidishie ilimu. Maelezo

115. Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau, wala hatukuona kwake azma kubwa. Maelezo

116. Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu, isipo kuwa Iblisi, alikataa. Maelezo

117. Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo. Basi asikutoeni katika Bustani hii, mkaingia mashakani. Maelezo

118. Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi. Maelezo

119. Na hakika hutapata kiu humo wala hutapata joto. Maelezo

120. Lakini Shet'ani alimtia wasiwasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujuulishe mti wa kuishi milele na ufalme usio koma? Maelezo

121. Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake Mlezi, na akapotea njia. Maelezo

122. Kisha Mola wake Mlezi akamteuwa, naye akamkubalia toba yake, naye akamwongoa. Maelezo

123. Akasema: Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukikufikieni uwongofu kutoka kwangu basi atakaye ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika. Maelezo

124. Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu. Maelezo

125. Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona? Maelezo

126. (Mwenyezi Mungu) atasema: Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na kadhaalika leo unasahauliwa. Maelezo

127. Na hivi ndivyo tutakavyo mlipa kila apitaye kiasi, na asiye amini ishara za Mola wake Mlezi. Na hakika adhabu ya Akhera ni kali zaidi, na inadumu zaidi. Maelezo

128. Je! Haikuwabainikia tu; vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao, nao wanatembea katika maskani zao? Hakika katika hayo zimo ishara kwa wenye akili. Maelezo

129. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi na muda ulio wekwa, bila ya shaka inge fika adhabu (hapa hapa). Maelezo

130. Yavumilie haya wayasemayo. Na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha. Maelezo

131. Wala usivikodolee macho tulivyo wastareheshea baadhi ya watu miongoni mwao, kwa ajili ya mapambo ya duniani, ili tuwajaribu. Na riziki ya Mola wako Mlezi ni bora na inadumu zaidi. Maelezo

132. Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchamngu. Maelezo

133. Na walisema: Kwa nini hakutuletea muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Je! Haikuwafikilia dalili wazi ya yaliyomo katika Vitabu vya kale? Maelezo

134. Na lau kuwa tuliwaangamiza kwa adhabu kabla yake, wangeli sema: Ewe Mola wetu Mlezi! Kwa nini usituletee Mtume tukazifuata ishara zako kabla hatujadhilika na kuhizika. Maelezo

135. Sema: Kila mmoja anangoja. Basi ngojeni! Hivi karibuni mtajua nani mwenye njia sawa na nani aliye ongoka. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani