Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

21. SURATUL ANBIYAA

(Imeteremka Makka)

 

HII NI SURA iliyo teremka Makka baada ya Surat Ibrahim. Aya zake ni 112. Inabainisha kukaribia Kiyama na hali washirikina wameghafilika nacho. Nao walidai kuwa Mtume hatokuwa binaadamu, na pengine wakisema kuwa hii Qur'ani ni uchawi, na pengine kuwa ni mashairi, na pengine ni ndoto za ovyo ovyo. Na maonyo yapo mbele yao. Na Mitume wote hawakuwa ila ni wanaadamu tu kama Muhammad s.a.w., na walio watangulia kabla yao walisema uwongo kama walivyo sema uwongo Makureshi.  Mwenyezi Mungu aliwajaalia ajali yao, kwani Yeye ni Mweza wa kuteketeza na kubakisha, na ni vyake Yeye vyote viliomo katika mbingu na ardhi.  Na Malaika kila walipo wanamtakasa kwa kumsabihi Mwenyezi Mungu Mtukufu wala hawasiti. Na hakika kwenda sawa mbingu na ardhi ni dalili kuwa Muumba wake ni Mmoja, kwani lau kuwa wangeli shirikiana waumbaji mambo yangeli fisidika. Na Mitume wote wamekuja na amri ya kuabudiwa Mwenyezi Mungu peke yake. Wala hana mwana, wala asiseme yeyote kuwa yeye ni mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Wasemao hivyo malipo yao ni Jahannamu. Na Subhanahu kabainisha utukufu wa viumbe vyake, na ajabu za uumbaji wake wa mbingu na ardhi. Na akabainisha hali ya washirikina na makafiri. Naye Subhanahu wa Taa'la amenabihisha vipi Mwenyezi Mungu Mtukufu anavyo wahifadhi watu, na akaashiria Subhanahu nini malipo ya makafiri Siku ya Kiyama. Na akataja hadithi ya Musa na Harun pamoja na Firauni, na hadithi ya Ibrahim pamoja na kaumu yake, na alivyo mneemesha kwa dhuriya wema. Naye Subhanahu wa Taa'la ametaja hadithi ya Luut' na kaumu yake, na walivyo angamizwa, na hadithi ya Nuhu a.s. na ukafiri wa kaumu yake, na walivyo teketezwa isipo kuwa walio amini. Kisha Subhanahu wa Taa'la  akaashiria hadithi za Sulaiman, na Daud, na Ayub, na Ismail, na Idris, na Dhulkifli, na Dhunnuun, na Maryamu. Na akataja khabari za Juj na Maajuj. Naye Subhanahu amebainisha vitendo vyema na matunda yake, na malipo watayo lipwa wenye kumchamngu na wakatenda mema, na hali yao Siku ya Kiyama, na rehema ya Mwenyezi Mungu katika Ujumbe wa Muhammad, na maonyo ya Mwenyezi Mungu kwa washirikina. Na kwamba hakika amri yote ni yake Yeye anavyo hukumu, na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. IMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza. Maelezo

2. Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo. Maelezo

3. Zimeghafilika nyoyo zao. Na wale walio dhulumu hunong'onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binaadamu tu kama nyinyi! Mnauwendea uchawi hali nanyi mnaona? Maelezo

4. Alisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo mbinguni na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. Maelezo

5. Lakini wao walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza kama walivyo tumwa wale wa mwanzo. Maelezo

6. Hawakuamini kabla yao watu wa mji tulio uangamiza. Basi, je, wataamini hawa? Maelezo

7. Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui. Maelezo

8. Wala hatukuwafanya miili isiyo kula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele. Maelezo

9. Kisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na tulio wataka, na tukawateketeza walio pita mipaka. Maelezo

10. Na hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani yake yamo makumbusho yenu. Je! Hamzingatii? Maelezo

11. Na mingapi katika miji iliyo kuwa ikidhulumu tumeiteketeza, na tukawasimamisha baada yao watu wengine. Maelezo

12. Basi walipo ihisi adhabu yetu, mara wakaanza kukimbia. Maelezo

13. Msikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu, na maskani zenu, mpate kusailiwa! Maelezo

14. Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhaalimu. Maelezo

15. Hakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya kama walio fyekwa, wamezimika. Maelezo

16. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yao kwa mchezo. Maelezo

17. Kama tungeli taka kufanya mchezo tunge jifanyia Sisi wenyewe, lau kwamba tungeli kuwa ni wafanyao mchezo. Maelezo

18. Bali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na mara ukatoweka. Na ole wenu kwa mnayo yazua. Maelezo

19. Na ni vyake Yeye tu Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki. Maelezo

20. Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei. Maelezo

21. Au wamepata miungu katika ardhi inayo fufua? Maelezo

22. Lau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua. Maelezo

23. Yeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao hojiwa kwa wayatendayo. Maelezo

24. Au wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza. Maelezo

25. Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu. Maelezo

26. Na wanasema: Arrahman, Mwingi wa Rehema, ana mwana! Subhanahu, Ametakasika na hayo! Bali hao (wanao waita wana) ni watumwa walio tukuzwa. Maelezo

27. Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake. Maelezo

28. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamwombei yeyote ila yule anaye mridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea. Maelezo

29. Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu. Maelezo

30. Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini? Maelezo

31. Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka. Maelezo

32. Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa, lakini wanazipuuza Ishara zake. Maelezo

33. Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea. Maelezo

34. Nasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako kuwa na maisha ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele? Maelezo

35. Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa. Maelezo

36. Na wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni kitu cha maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na hali wao wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema! Maelezo

37. Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize. Maelezo

38. Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli? Maelezo

39. Lau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa! Maelezo

40. Bali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula! Maelezo

41. Na Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa. Kwa hivyo wale walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia dhihaka. Maelezo

42. Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi. Maelezo

43. Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi! Maelezo

44. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda? Maelezo

45. Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo onywa. Maelezo

46. Na wanapo guswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu itokayo kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa wenye kudhulumu. Maelezo

47. Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu. Maelezo

48. Na kwa yakini tuliwapa Musa na Haaruni kipambanuzi, na mwangaza, na makumbusho kwa wachamngu, Maelezo

49. Ambao wanamkhofu Mola wao Mlezi faraghani, na wanaiogopa Saa ya Kiyama. Maelezo

50. Na haya ni makumbusho yaliyo barikiwa, tuliyo yateremsha. Basi je! Mnayakataa? Maelezo

51. Na hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake zamani, na tulikuwa tunamjua. Maelezo

52. Alipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu? Maelezo

53. Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu. Maelezo

54. Akasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika upotofu ulio dhaahiri. Maelezo

55. Wakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika wachezao tu? Maelezo

56. Akasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo. Maelezo

57. Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya mkisha geuka kwenda zenu. Maelezo

58. Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao walirudie. Maelezo

59. Wakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni katika walio dhulumu. Maelezo

60. Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim. Maelezo

61. Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia! Maelezo

62. Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibrahim? Maelezo

63. Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka. Maelezo

64. Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu! Maelezo

65. Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi. Maelezo

66. Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni? Maelezo

67. Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini? Maelezo

68. Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo! Maelezo

69. Sisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim! Maelezo

70. Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri. Maelezo

71. Na tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye nchi tulio ibariki kwa ajili ya walimwengu wote. Maelezo

72. Naye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote tukawajaalia wawe watu wema. Maelezo

73. Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu. Maelezo

74. Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu. Maelezo

75. Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa watenda mema. Maelezo

76. Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa. Maelezo

77. Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote. Maelezo

78. Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao hiyo. Maelezo

79. Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo. Maelezo

80. Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru? Maelezo

81. Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu. Maelezo

82. Na pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya kazi nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao. Maelezo

83. Na Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu. Maelezo

84. Basi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo kuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo toka kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada. Maelezo

85. Na Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa miongoni mwa wanao subiri. Maelezo

86. Na tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa katika watu wema. Maelezo

87. Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu. Maelezo

88. Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyo waokoa Waumini. Maelezo

89. Na Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi. Maelezo

90. Basi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na khofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea. Maelezo

91. Na mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu. Maelezo

92. Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi. Maelezo

93. Nao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote watarudi kwetu. Maelezo

94. Na atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia. Maelezo

95.Na haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba hawatarejea, Maelezo

96. Mpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa wanateremka kutoka kila mlima; Maelezo

97. Na miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo kodoka macho ya walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu. Maelezo

98. Hakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu. Maelezo

99. Lau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote watadumu humo. Maelezo

100. Lao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia (jenginelo). Maelezo

101. Ama wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na hayo. Maelezo

102. Hawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale zinayo yatamani nafsi zao. Maelezo

103. Hicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa! Maelezo

104. Siku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao. Maelezo

105. Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema. Maelezo

106. Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada. Maelezo

107. Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote. Maelezo

108. Sema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Je! Mmesilimu? Maelezo

109. Na kama wakigeuka, basi sema: Nimekutangazieni sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyo ahidiwa. Maelezo

110. Hakika Yeye anajua kauli ya dhaahiri na anajua myafichayo. Maelezo

111. Wala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo. Maelezo

112. Sema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa Rehema, aombwaye msaada juu ya mnayo yazua. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani