Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

23. SURATUL MUUMINUN

(Imeteremka Makka)

 

HII NI SURA iliyo teremka Makka. Aya zake ni mia na kumi na nane. Imeanza kwa kuthibitisha mafanikio ya Waumini, na ikafuatia kueleza sifa zao. Kisha ikataja asli ya kuumbwa mwanaadamu, na kubadilika kwake kwa kukua, na kuzalikana vizazi vyake, na baadhi ya mambo yanayo dhihirisha uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Tena  zikafuatia hadithi za Manabii zinazo fanana kwa umoja wa ujumbe na umoja wa binaadamu, ijapo kuwa watu wanga khitalifiana baina ya wanao kubali na wanao kengeuka. Na sura hii imeeleza khabari za mwenye kutaka uwongofu, na mwenye kupotoka, na msimamo wa washirikina mbele ya Nabii s.a.w. Tena ikaingia kueleza yanayo onekana ya uwezo wa Mwenyezi Mungu katika hukumu za kumuumba mwanaadamu. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu kaingia kuwauliza watu wamjibu kwa kutumia akili zao za maumbile kwa yanayo thibitisha kuwepo kwake, na kuthibitisha Ungu wake. Kisha Sura hii ikaeleza hali za watu itavyo kuwa Siku ya Kiyama, na kwamba wao watahisabiwa, na watafanyiwa uadilifu. Tena Sura inakhitimisha kubainisha Utukufu wake Subhanahu wa Taa'la, na kumnabihisha Nabii wake aombe maghfira na rehema kutokana na Mbora wa wenye kurehemu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. HAKIKA wamefanikiwa Waumini, Maelezo

2. Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao, Maelezo

3. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi, Maelezo

4. Na ambao wanatoa Zaka, Maelezo

5.Na ambao wanazilinda tupu zao, Maelezo

6. Isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Maelezo

7. Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka. Maelezo

8. Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao, Maelezo

9. Na ambao Sala zao wanazihifadhi - Maelezo

10. Hao ndio warithi, Maelezo

11. Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo. Maelezo

12. Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo. Maelezo

13. Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti. Maelezo

14. Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji. Maelezo

15. Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa. Maelezo

16. Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa. Maelezo

17. Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye kughafilika na viumbe. Maelezo

18. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa. Maelezo

19. Kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula; Maelezo

20. Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa kitoweo kwa walao. Maelezo

21. Na hakika mnayo mazingatio makubwa katika nyama hoa - tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, na nyinyi mnapata katika hao manufaa mengi, na pia mnawala. Maelezo

22. Na juu yao na juu ya marikebu mnabebwa. Maelezo

23. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiye kuwa Yeye. Basi je! Hamwogopi? Maelezo

24. Walisema wale wakuu walio kufuru katika watu wake: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Anataka kujipa ubora juu yenu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu amependa basi yakini angeli teremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa baba zetu wa zamani. Maelezo

25. Huyu si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeeni tu kwa muda. Maelezo

26. Akasema (Nuhu): Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa kuwa wamenikanusha. Maelezo

27. Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa. Maelezo

28. Basi utakapo tulia wewe na walio pamoja nawe humo marikebuni, sema: Alhamdulillahi Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, aliye tuokoa na watu madhaalimu! Maelezo

29. Na sema: Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye baraka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji. Maelezo

30. Hakika katika hayo yapo mazingatio. Na kwa yakini Sisi ni wenye kuwafanyia mtihani. Maelezo

31. Kisha baada yao tukaanzisha kizazi kingine. Maelezo

32. Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu! Hamna mungu asiye kuwa Yeye. Jee, hamwogopi? Maelezo

33. Na wakubwa katika watu wake walio kufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera, na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binaadamu kama nyinyi; anakula mlacho, na anakunywa mnywacho. Maelezo

34. Na nyinyi mkimt'ii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa khasarani. Maelezo

35. Hivyo anakuahidini ati ya kwamba mtakapo kufa na mkawa udongo na mifupa kuwa mtatolewa? Maelezo

36. Hayawi! Hayawi hayo mnayo ahidiwa. Maelezo

37. Hapana ila uhai wetu wa duniani tu, tunakufa na kuishi basi. Wala sisi hatutafufuliwa. Maelezo

38. Huyu si lolote ila ni mtu anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, wala sisi sio wa kumuamini. Maelezo

39. Akasema: Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa sababu wananikanusha. Maelezo

40. (Mwenyezi Mungu) akasema: Baada ya muda mchache watakuwa wenye kujuta. Maelezo

41. Basi ukawanyakua ukelele kwa haki, na tukawafanya kama takataka zinazo elea juu ya maji. Ikapotelea mbali kaumu ya madhaalimu! Maelezo

42. Kisha tukaleta baada yao vizazi vingine. Maelezo

43. Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala kuikawiza. Maelezo

44. Kisha tukawatuma Mitume wetu, mmoja baada ya mmoja. Kila umma alipo wafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatanisha hawa baada ya hawa, na tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Wakapotelea mbali watu wasio amini. Maelezo

45. Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, pamoja na ishara zetu na hoja zilizo wazi. Maelezo

46. Kumwendea Firauni na wakuu wake. Lakini walijivuna, nao walikuwa watu majeuri. Maelezo

47. Wakasema: Je, tuwaamini wanaadamu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu? Maelezo

48. Basi wakawakanusha, na wakawa miongoni mwa walio angamizwa. Maelezo

49. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka. Maelezo

50. Na tukamfanya mwana wa Mariamu na mama yake kuwa ni Ishara, na tukawapa makimbilio kwenda mahali palipo inuka penye utulivu na chemchem za maji. Maelezo

51. Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayo yatenda. Maelezo

52. Na kwa yakini huu Umma wenu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi. Maelezo

53. Lakini walikatiana jambo lao mapande mbali mbali. Kila kundi likifurahia kwa waliyo nayo. Maelezo

54. Basi waache katika ghafla yao kwa muda. Maelezo  

55. Je! Wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyo wapa mali na watoto Maelezo

56. Ndio tunawahimizia kheri? Lakini wenyewe hawatambui. Maelezo

57. Kwa hakika hao ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi wananyenyekea, Maelezo

58. Na wale ambao Ishara za Mola wao Mlezi wanaziamini, Maelezo

59. Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi, Maelezo

60. Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi, Maelezo

61. Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia. Maelezo

62. Na hatuilazimishi nafsi ila kwa kadri ya uwezo wake. Na tunacho kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa. Maelezo

63. Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo vitendo vinginevyo wanavyo vifanya. Maelezo

64. Hata tutakapo watia katika adhabu wale walio dekezwa kwa starehe kati yao, hapo ndipo watapo yayatika. Maelezo

65. Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi. Maelezo

66. Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa, nanyi mkirudi nyuma juu ya visigino vyenu, Maelezo

67. Na huku mkitakabari na usiku mkiizungumza (Qur'ani) kwa dharau. Maelezo

68. Je, hawakuifikiri kauli, au yamewajia yasiyo wafikia baba zao wa zamani? Maelezo

69. Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa? Maelezo

70. Au wanasema: Ana wazimu? Bali amewajia kwa Haki, na wengi wao wanaichukia Haki. Maelezo

71. Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao. Maelezo

72. Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako Mlezi ni bora, na Yeye ndiye Mbora wa wanao ruzuku. Maelezo

73. Na kwa yakini wewe unawaita kwenye Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

74. Na hakika wale wasio iamini Akhera wanajitenga na Njia hiyo. Maelezo

75. Na lau tungeli warehemu na tukawaondolea shida waliyo nayo bila ya shaka wangeli endelea katika upotofu wao vile vile, wakitangatanga. Maelezo

76. Na hakika tuliwatia adhabu kali; lakini hawakuelekea kwa Mola wao Mlezi wala hawakunyenyekea. Maelezo

77. Mpaka tulipo wafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa wenye kukata tamaa. Maelezo

78. Na Yeye ndiye aliye kuumbieni kusikia na kuona na nyoyo za kufahamu. Ni kuchache mno kushukuru kwenu. Maelezo

79. Na Yeye ndiye aliye kuenezeni katika ardhi, na kwake Yeye mtakusanywa. Maelezo

80. Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu? Maelezo

81. Bali wanasema kama walivyo sema watu wa kwanza. Maelezo

82. Walisema: Je! Tukisha kufa tukawa udongo na mifupa ndio tutafufuliwa? Maelezo

83. Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni visa vya uwongo vya watu wa zamani. Maelezo

84. Sema: Ni ya nani ardhi na viliomo ndani yake, kama nyinyi mnajua? Maelezo

85. Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu! Sema: Basi, je, hamkumbuki? Maelezo

86. Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa A'rshi Kuu? Maelezo

87. Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, hamwogopi? Maelezo

88. Sema: Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu, naye ndiye anaye linda, wala hakilindwi asicho taka, kama mnajua? Maelezo

89. Watasema: (Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu. Sema: Basi vipi mnadanganyika? Maelezo

90. Bali tumewaletea Haki, na kwa yakini hao ni waongo. Maelezo

91. Mwenyezi Mungu hana mwana yeyote, wala hanaye mungu mwengine. Inge kuwa hivyo basi kila mungu angeli chukua alivyo umba, na baadhi yao wangeli washinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazo msifu. Maelezo

92. Mjuzi wa siri na dhaahiri, na ametukuka juu ya hayo wanayo mshirikisha nayo. Maelezo

93. Sema: Mola wangu Mlezi! Ukinionyesha adhabu waliyo ahidiwa, Maelezo

94. Mola wangu Mlezi! Usinijaalie katika watu madhaalimu hao. Maelezo

95. Na hakika Sisi ni waweza wa kukuonyeshsa tuliyo waahidi. Maelezo

96. Kinga maovu kwa kutenda yaliyo mema zaidi. Sisi tunajua wayasemayo. Maelezo

97. Na sema: Mola wangu Mlezi! Najikinga kwako na wasiwasi wa mashet'ani. Maelezo

98. Na najikinga kwako, Mola wangu Mlezi, wasinikaribie. Maelezo

99. Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe. Maelezo

100. Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa. Maelezo

101. Basi litapo pulizwa baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana. Maelezo

102. Ama wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufanikiwa. Maelezo

103. Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio walio zitia khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu watadumu. Maelezo

104. Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizo kunjana. Maelezo

105. Je! Hazikuwa Aya zangu mkisomewa, na nyinyi mkizikanusha? Maelezo

106. Mola wetu Mlezi! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tulio potea. Maelezo

107. Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni. Na tufanyapo tena basi kweli sisi ni wenye kudhulumu. Maelezo

108. Atasema Mwenyezi Mungu: Tokomeeni humo, wala msinisemeze. Maelezo

109. Bila ya shaka lilikuwapo kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini; basi tusamehe na uturehemu, nawe ndiwe Mbora wa wanao rehemu. Maelezo

110. Lakini nyinyi mliwakejeli hata wakakusahaulisheni kunikumbuka, na mlikuwa mkiwacheka. Maelezo

111. Hakika Mimi leo nimewalipa kwa vile walivyo subiri. Bila ya shaka hao ndio wenye kufuzu. Maelezo

112. Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka? Maelezo

113. Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanao weka hisabu. Maelezo

114. Atasema: Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua. Maelezo

115. Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? Maelezo

116. Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu. Maelezo

117. Na anaye muomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwenginewe hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka hisabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi. Maelezo

118. Nawe sema: Mola wangu Mlezi! Samehe na urehemu nawe ni Mbora wa wanao rehemu. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani