Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani¬  (Nani Yeye?)

24. SURATUN NUR

(Imeteremka Madina)

Sura hii ni ya Madina, na Aya zake ni 64. Mwenyezi Mungu amebainisha ndani yake waajibu wa kusafisha umma na uchafu wa zina na kutangaza fedheha kwa vitendo na maneno kati ya Waumini. Na akaleta sharia ya adhabu kuzuia hayo, kama alivyo leta sharia makhsusi katika uzinzi wa mume au mke ili kujenga imani baina ya mtu na mkewe. Kutoka uzinzi masimulizi yakaingilia kutaja hukumu ya uwongo katika hali hizi, na yawapasayo Waumini kwa min tarafu ya neno ovu lisio kuwa na dalili. Tena yakafuatia masimulizi ya adabu za kuingia majumbani.¬  Na nani mwenye haki ya kuona pambo la mwanamke. Na baada ya wito wa jumla ikafuatiliza kutakiwa mwendo safi usio na towa. Kisha imekuja Nuru ya Mwenyezi Mungu, na inatajwa misikiti, na vinatangazwa vitendo vya makafiri na hali za wenye inadi. Na upande mwengine zinaelezwa hali za Waumini. Baada ya hayo Sura inaeleza adabu za watu wa nyumbani, watu walio khusiana, watoto na wakubwa, katika hali ya kuingiliana na kuchanganyika. Na nani mwenye haki ya kula naye mtu. Na khatimaye zimetajwa sifa za Waumini wanapo itwa na Mtume kwa jambo lilio wakhusu wote, na Sura ikambainisha Mwenye Ukuu wa Ufalme wake ulio tukuka, na Mwenye kuenea ujuzi wake.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

 

1. HII NI SURA Tuliyo iteremsha na tukailazimisha; tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke. Maelezo

 

2. Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini. Maelezo

 

3. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo yameharimishwa kwa Waumini. Maelezo

 

4. Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu. Maelezo

 

5. Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu. Maelezo

 

6. Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli. Maelezo

 

7. Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo. Maelezo

 

8. Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba huyu mume ni miongoni mwa waongo. Maelezo

 

9. Na mara ya tano ya kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake kama mumewe yu miongoni mwa wanao sema kweli. Maelezo

 

10. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpokeaji toba.... Maelezo

 

11. Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyo yachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa. Maelezo

 

12. Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri? Maelezo

 

13. Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo. Maelezo

 

14. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyo jiingiza. Maelezo

 

15. Mlipo yapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyo yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa. Maelezo

 

16. Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa! Maelezo

 

17. Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini! Maelezo

 

18. Na Mwenyezi Mungu anakubainisheni Aya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. Maelezo

 

19. Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui. Maelezo

 

20. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu.... Maelezo

 

21. Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakaye fuata nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. Maelezo

 

22. Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa jamaa zao na masikini na walio hama kwa Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. Maelezo

 

23. Hakika wanao wasingizia wanawake, wanao jihishimu, walio ghafilika, Waumini, wamelaaniwa duniani na Akhera, nao watapata adhabu kubwa. Maelezo

 

24. Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

 

25. Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki, na watajua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki Iliyo Wazi. Maelezo

 

26. Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Hao wameepushwa na hayo wanayo yasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu. Maelezo

 

27. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka. Maelezo

 

28. Na msip o mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yatenda. Maelezo

 

29. Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisio kaliwa ambazo ndani yake yamo manufaa yenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yadhihirisha na mnayo yaficha. Maelezo

 

30. Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za wanayo yafanya. Maelezo

 

31. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa. Maelezo

 

32. Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua. Maelezo

 

33. Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa uhuru katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo

 

34. Na kwa yakini tumekuteremshieni Ishara zilizo wazi na mifano kutokana na walio tangulia kabla yenu na mawaidha kwa wachamngu. Maelezo

 

35. Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. Maelezo

 

36. Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni Maelezo

 

37. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka. Maelezo

 

38. Ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo yatenda, na awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu. Maelezo

 

39. Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu. Maelezo

 

40. Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na nuru. Maelezo

 

41. Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua Sala yake na namna ya kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua wayatendayo. Maelezo

 

42. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya wote. Maelezo

 

43. Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua macho. Maelezo

 

44. Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa wenye kuona. Maelezo

 

45. Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. Maelezo

 

46. Kwa yakini tumeteremsha Ishara zinazo bainisha. Na Mwenyezi Mungu hummwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

 

47. Na wanasema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tumet'ii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala hao si wenye kuamini. Maelezo

 

48. Na wanapo itwa kumuendea Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, kipo kikundi katika wao kinakataa. Maelezo

 

49. Na ikiwa haki ni yao, wanamjia kwa kut'ii. Maelezo

 

50. Je! Wana maradhi katika nyoyo zao, au wanaona shaka, au wanaogopa ya kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu? Bali hao ndio madhaalimu. Maelezo

 

51. Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufanikiwa. Maelezo

 

52. Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu. Maelezo

 

53. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kiapo chao ya kwamba ukiwaamrisha kwa yakini watatoka. Sema: Msiape! Ut'iifu unajuulikana. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. Maelezo

 

54. Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Na mkigeuka, basi yaliyo juu yake ni aliyo bebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyo bebshwa nyinyi. Na mkimt'ii yeye mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe wazi wazi. Maelezo

 

55. Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu. Maelezo

 

56. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mtume, ili mpate kurehemewa. Maelezo

 

57. Msiwadhanie walio kufuru kwamba watashinda katika nchi. Na makaazi yao ni Motoni, na hakika ni maovu kweli marejeo yao. Maelezo

 

58. Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. Maelezo

 

59. Na watoto wanapo fikilia umri wa kubaalighi basi nawatake ruhusa, kama walivyo taka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyo kubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima. Maelezo

 

60. Na wanawake wazee wasio taraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao, bila ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijihishimu ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. Maelezo

 

61. Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba zenu, au nyumba za mama zenu, au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada wa mama zenu, au za mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu. Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, kuwa ni maamkio yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka na mema. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Aya zake mpate kuelewa. Maelezo

 

62. Hakika Waumini wa kweli ni walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na wanapo kuwa pamoja naye kwa jambo la kuwakhusu wote hawaondoki mpaka wamtake ruhusa. Kwa hakika wale wanao kuomba ruhusa, hao ndio wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya kazi zao, mruhusu umtakaye miongoni mwao, uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemmu. Maelezo

 

63. Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanao ondoka kwa uficho. Basi nawatahadhari wanao khalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu. Maelezo

 

64. Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika Yeye anajua mlio nayo. Na siku mtapo rudishwa kwake atawaeleza waliyo yafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. Maelezo ¬ ¬ 


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani