Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

25. SURAT AL FURQAN

(Imeteremka Makka)

 

Idadi ya Aya za Sura hii ni 77. Zote ni za Makka  isipo kuwa Aya 68, 69 na 70.
Sura imeanzia kwa kubainisha cheo cha Qur'ani, na ukubwa wa ufalme wa  Mwenye kuiteremsha ambaye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na juu ya utukufu wa utawala wake, washirikina bado badala yake wanaabudu masanamu, na wanaikadhibisha Qur'ani,  na wanaukataa  Utume wa Mtume s.a.w. kwa hoja ya kuwa ati yeye ni binaadamu, anakula chakula, na anatembea masokoni, na kwa ubishi wanataka Malaika ndio wawaletee Ujumbe.  Na lau kuwa Mwenyezi Mungu amewafanya Mitume wake Malaika angeli wafanya ni watu ili wapate kufahamiana na watu. Ubabaishi unge baki. Na wakapinga kwa nini Qur'ani ikawa inateremka vipande vipande. Wakajibiwa hikima ya hayo. Na inda hii ikafuatilizwa kwa mifano yenye kueleza khabari za Mitume waliyo pita na kaumu zao. Lakini hizo kaumu zikafuata matamanio yao. Wakawa kama wanyama au wapotovu zaidi katika mwendo wao. Na zikaja Aya za uumbaji zenye kuonyesha ukamilifu wa kudra yake Mtukufu, yenye kufahamisha uangalizi na maarifa. Na Sura  ikakhitimisha kwa kutaja sifa za Waumini zitazo warithisha vyumba vya Peponi vya juu, watapo pokewa kwa maamkio na kusalimiwa.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote. Maelezo

2. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo. Maelezo

3. Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka. Maelezo

4. Na wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na uwongo. Maelezo

5. Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni. Maelezo

6. Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. Maelezo

7. Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye? Maelezo

8. Au akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa. Maelezo

9. Tazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea, wala hawataiweza Njia. Maelezo

10. Ametukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya fakhari. Maelezo

11. Bali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa.. Maelezo

12. Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yake na mngurumo wake. Maelezo

13. Na watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa, wataomba wafe. Maelezo

14. Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi! Maelezo

15. Sema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo? Maelezo

16. Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayo ombwa. Maelezo

17. Na siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na akasema: Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia? Maelezo

18. Watasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia. Maelezo

19. Basi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha adhabu kubwa. Maelezo

20. Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuona. Maelezo

21. NA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa wamejiona bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno! Maelezo

22. Siku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu. Na watasema: Mungu apishe mbali! Maelezo

23. Na tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika. Maelezo

24. Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora na mahali penye starehe nzuri. Maelezo

25. Na siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na wateremshwe Malaika kwa wingi, Maelezo

26. Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri. Maelezo

27. Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume! Maelezo

28. Ee Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki! Maelezo

29. Amenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shet'ani ni khaini kwa mwanaadamu. Maelezo

30. Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur'ani ni kihame. Maelezo

31. Na vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru. Maelezo

32. Na wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur'ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu. Maelezo

33. Wala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora. Maelezo

34. Wale ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana njia. Maelezo

35. Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri. Maelezo

36. Tukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa. Maelezo

37. Na watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume, tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye kudhulumu adhabu chungu. Maelezo

38. Na tuliwaangamiza kina A'di na Thamudi na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyo kuwa kati yao. Maelezo

39. Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa. Maelezo

40. Na kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio teremshiwa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiiona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa. Maelezo

41. Na wanapo kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na (wanasema): Ati ndiye huyu Mwenyezi Mungu aliye mtuma kuwa Mtume? Maelezo

42. Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu yetu, ingeli kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapo iona adhabu, ni nani aliye potea njia. Maelezo

43. Je! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake? Maelezo

44. Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia. Maelezo

45. Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake. Maelezo

46. Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo. Maelezo

47. Naye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akakufanyieni mchana ni kufufuka. Maelezo

48. Naye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi. Maelezo

49. Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba. Maelezo

50. Na kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini watu wengi wanakataa ila kukufuru. Maelezo

51. Na tungeli taka tungeli peleka katika kila mji Mwonyaji. Maelezo

52. Basi usiwat'ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa Jihadi kubwa. Maelezo

53. Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho. Maelezo

54. Naye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza. Maelezo

55. Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi. Maelezo

56. Nasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji. Maelezo

57. Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi. Maelezo

58. Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake. Maelezo

59. Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Uliza khabari zake kwa wamjuaye. Maelezo

60. Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki. Maelezo

61. Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng'ara. Maelezo

62. Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru. Maelezo

63. Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama! Maelezo

64. Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama. Maelezo

65. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi. Maelezo

66. Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya. Maelezo

67. Na wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo. Maelezo

68. Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara, Maelezo

69. Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka. Maelezo

70. Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo

71. Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu. Maelezo

72. Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao. Maelezo

73. Na wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu. Maelezo

74. Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu. Maelezo

75. Hao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu. Maelezo

76. Wadumu humo - kituo na makao mazuri kabisa. Maelezo

77. Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani