Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

26. SURAT ASH-SHUA'RAA

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanzia kwa kuisifu Qur'ani yenyewe, ikaingia kuwaonya makafiri kwa uweza wa Mwenyezi Mungu kuwateremshia adhabu juu yao, na kumliwaza Nabii s.a.w. kwa anayo yapata ya kukanushwa na watu wake, kwa kutajiwa yalio wapata Mitume wa kabla yake ya kukadhibishwa na kaumu zao. Ikasimulia mkutano wa Musa na Harun walipo kutana na Firauni, na alivyo wakadhibisha yeye. Kisha Subhanahu akataja kisa cha Ibrahim, baba wa Manabii, na khabari za Nuhu pamoja na kaumu yake, na mambo ya A'adi, na Saleh pamoja na Thamud. Kisha ikaelezea Sura wito wa Lut'i na kisa cha Shuaib na watu wa Vichakani (Al-Aykat).
Na mwenye kuzingatia  visa vya hawa Manabii saba ataona asili ya wito wao ni mmoja. Na njia ya makafiri katika kupinga ujumbe wao ni moja. Kama ilivyo anzia Sura basi ilikhitimishia mazumgumzo kwa kuvunja wazo la kuwa Mtume ni mtunga mashairi, na kuwa Qur'ani ni mashairi.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. T'aa Siin Miim. (T'.S.M.) Maelezo

2. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha. Maelezo

3. Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini. Maelezo

4. Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao. Maelezo

5. Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao. Maelezo

6. Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha. Maelezo

7. Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri? Maelezo

8. Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. Maelezo

9. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

10. Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu, Maelezo

11. Watu wa Firauni. Hawaogopi? Maelezo

12. Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe. Maelezo

13. Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun. Maelezo

14. Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa. Maelezo

15. Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza. Maelezo

16. Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

17. Waachilie Wana wa Israili wende nasi. Maelezo

18. (Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi? Maelezo

19. Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani? Maelezo

20. (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea. Maelezo

21. Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume. Maelezo

22. Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili? Maelezo

23. Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote? Maelezo

24. Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini. Maelezo

25. (Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi? Maelezo

26. (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza. Maelezo

27. (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu. Maelezo

28. (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini. Maelezo

29. (Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani. Maelezo

30. Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi? Maelezo

31. Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli. Maelezo

32. Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri. Maelezo

33. Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao. Maelezo

34. (Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu. Maelezo

35. Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani? Maelezo

36. Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo. Maelezo

37. Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu. Maelezo

38. Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu. Maelezo

39. Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika? Maelezo

40. Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda. Maelezo

41. Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda? Maelezo

42. Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele. Maelezo

43. Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa. Maelezo

44. Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda. Maelezo

45. Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua. Maelezo

46. Hapo wachawi walipinduka wakasujudu. Maelezo

47. Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

48. Mola Mlezi wa Musa na Harun. Maelezo

49. (Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote. Maelezo

50. Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. Maelezo

51. Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini. Maelezo

52. Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa. Maelezo

53. Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo. Maelezo

54. (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo. Maelezo

55. Nao wanatuudhi. Maelezo

56. Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari. Maelezo

57. Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem, Maelezo

58. Na makhazina, na vyeo vya hishima, Maelezo

59. Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili. Maelezo

60. Basi wakawafuata lilipo chomoza jua. Maelezo

61. Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana! Maelezo

62. (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa! Maelezo

63. Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa. Maelezo

64. Na tukawajongeza hapo wale wengine. Maelezo

65. Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote. Maelezo

66. Kisha tukawazamisha hao wengine. Maelezo

67. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini. Maelezo

68. Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

69. Na wasomee khabari za Ibrahim. Maelezo

70. Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini? Maelezo

71. Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea. Maelezo

72. Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita? Maelezo

73. Au yanakufaeni, au yanakudhuruni? Maelezo

74. Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo. Maelezo

75. Je! Mmewaona hawa mnao waabudu- Maelezo

76. Nyinyi na baba zenu wa zamani? Maelezo

77. Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

78. Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa, Maelezo

79. Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha. Maelezo

80. Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha. Maelezo

81. Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha. Maelezo

82. Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo. Maelezo

83, Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema. Maelezo

84. Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye. Maelezo

85. Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema. Maelezo

86. Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu. Maelezo

87. Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa. Maelezo

88. Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana. Maelezo

89. Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi. Maelezo

90. Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu. Maelezo

91. Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu. Maelezo

92. Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu Maelezo

93. Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe? Maelezo

94. Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu, Maelezo

95. Na majeshi ya Ibilisi yote. Maelezo

96. Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo: Maelezo

97. Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri, Maelezo

98. Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

99. Na hawakutupoteza ila wale wakosefu. Maelezo

100. Basi hatuna waombezi. Maelezo

101. Wala rafiki wa dhati. Maelezo

102. Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini. Maelezo

103. Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini. Maelezo

104. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

105. Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume. Maelezo

106. Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu? Maelezo

107. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. Maelezo

108. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. Maelezo

109. Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

110. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. Maelezo

111. Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini? Maelezo

112. Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya? Maelezo

113. Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua! Maelezo

114. Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini. Maelezo

115. Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri. Maelezo

116. Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe. Maelezo

117. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha. Maelezo

118. Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini. Maelezo

119. Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni. Maelezo

120. Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia. Maelezo

121. Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao walio kuwa Waumini. Maelezo

122. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

123. Kina A'd waliwakanusha Mitume. Maelezo

124. Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu? Maelezo

125. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. Maelezo

126. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. Maelezo

127. Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

128. Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi? Maelezo

129. Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele! Maelezo

130. Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari. Maelezo

131. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. Maelezo

132. Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua. Maelezo

133. Amekupeni wanyama wa kufuga na wana. Maelezo

134. Na mabustani na chemchem. Maelezo

135. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa. Maelezo

136. Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha. Maelezo

137. Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani. Maelezo

138. Wala sisi hatutaadhibiwa. Maelezo

139. Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. Maelezo

140. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

141. Kina Thamud waliwakanusha Mitume. Maelezo

142. Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu? Maelezo

143. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. Maelezo

144. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini. Maelezo

145. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

146. Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa? Maelezo

147. Katika mabustani, na chemchem? Maelezo

148. Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva. Maelezo

149. Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi. Maelezo

150. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. Maelezo

151, Wala msit'ii amri za walio pindukia mipaka, Maelezo

152. Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi. Maelezo

153. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa. Maelezo

154. Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. Maelezo

155. Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu. Maelezo

156. Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa. Maelezo

157. Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta. Maelezo

158. Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. Maelezo

159. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

160. Watu wa Lut'i waliwakanusha Mitume. Maelezo

161. Alipo waambia ndugu yao, Lut'i: Je! Hamumchimngu? Maelezo

162. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu. Maelezo

163. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi. Maelezo

164. Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

165. Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume? Maelezo

166. Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka! Maelezo

167. Wakasema: Ewe Lut'i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji! Maelezo

168. Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu. Maelezo

169. Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo. Maelezo

170. Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote, Maelezo

171. Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma. Maelezo

172. Kisha tukawaangamiza wale wengine. Maelezo

173. Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa. Maelezo

174. Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini. Maelezo

175. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. Maelezo

176. Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume. Maelezo

177. Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu? Maelezo

178. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu. Maelezo

179. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi. Maelezo

180. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

181. Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja. Maelezo

182. Na pimeni kwa haki iliyo nyooka; Maelezo

183. Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi. Maelezo

184. Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia. Maelezo

185. Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa. Maelezo

186. Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo. Maelezo

187. Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli. Maelezo

188. Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda. Maelezo

189. Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa. Maelezo

190. Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini. Maelezo

191. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

192. Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

193. Ameuteremsha Roho muaminifu, Maelezo

194. Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji, Maelezo

195. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi. Maelezo

196. Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale. Maelezo

197. Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili? Maelezo

198. Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu, Maelezo

199. Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini. Maelezo

200. Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu. Maelezo

201. Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu. Maelezo

202. Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari. Maelezo

203. Na watasema: Je, tutapewa muhula? Maelezo

204. Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu? Maelezo

205. Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka, Maelezo

206. Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa, Maelezo

207. Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa? Maelezo

208. Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji - Maelezo

209. Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu. Maelezo

210. Wala Mashet'ani hawakuteremka nayo, Maelezo

211. Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi. Maelezo

212. Hakika hao wametengwa na kusikia. Maelezo

213. Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa. Maelezo

214. Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe. Maelezo

215. Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini. Maelezo

216. Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda. Maelezo

217. Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

218. Ambaye anakuona unapo simama, Maelezo

219. Na mageuko yako kati ya wanao sujudu. Maelezo

220. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. Maelezo

221. Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet'ani? Maelezo

222. Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi. Maelezo

223. Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo. Maelezo

224. Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata. Maelezo

225. Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde? Maelezo

226. Na kwamba wao husema wasiyo yatenda? Maelezo

227. Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani