Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani¬  (Nani Yeye?)

29. SURAT AL A'NKABUT

(Imeteremka Makka)

SURA HII NI ya Makka, na idadi ya Aya zake ni 69. Lakini Aya 1 mpaka 11 ziliteremka Madina. Sura hii imeanzia kwa kubainisha kwamba hapana budi ila Imani ya Waumini itiwe mitihanini kwa misukosuko na jihadi kwa ajili ya kulinda dola ya Haki na Imani. Na binaadamu ameusiwa kwa wazazi wake pamoja na amri ya jihadi, ili ukusanyike wema na jihadi, na baina ya watu wa namna mbali mbali na Imani. Na imeelezwa kwamba miongoni mwao yupo anaye sema kwa ulimi wake kwamba ameamini na hali moyo wake haukukubali. Kisha Sura hii imetaja khabari za Nuhu na kaumu yake, na kadhaalika imeeleza kisa cha Ibrahim katika wito wake. Na ikabainisha mafunzo hayo kwa ajili ya Mtume s.a.w. Kisha ikasimulia jawabu ya watu wa Ibrahim. Na ikaeleza khabari za Lut'i na kisa cha kaumu yake, na kuteremka kwa Wajumbe Malaika wa Mwenyezi Mungu kuja kuwahiliki, na wakaokoka ahali zake isipo kuwa mkewe. Kisha Subhanahu akaashiria kisa cha Shuaibu pamoja na Madyana, na cha Hud na A'di, na Saleh na Thamud, na kudanganyikiwa kwa Qaruni na Firauni na Hamani na matokeo ya mwisho wao. Na Yeye Subhanahu amebainisha kwamba kuabudu masanamu kwa washirikina kunategemea hoja iliyo kuwa dhaifu kabisa kuliko jumba la buibui. Na kwamba mifano kama hii hawaielewi ila wale wanao tumia akili zao. Na baada ya hayo Mwenyezi Mungu akamuamrisha Nabii wake asijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia nzuri. Na Yeye Subhanahu akaashiria kwamba Nabii s.a.w. hajui kusoma wala kuandika, na hayo yanazidi kuonyesha Utume wake. Na pia Subhanahu ametaja ukaidi wa washirikina katika kutaka kwao waletewe miujiza ya kuiona, nayo wataikataa kama walivyo ikataa kaumu ya Musa na wengineo. Na akagusia kule kuhimiza kwao kuteremshiwa adhabu. Naye amewabainishia adhabu itakayo wapata. Naye Subhanahu akataja malipo ya Waumini na Makafiri Siku ya Kiyama, na akataka watu watazame baada ya hayo ulimwengu na neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu ziliomo ndani yake. Kisha akataja thamani ya uhai wa duniani ukilinganisha na wa Akhera, na hali ya washirikina katika unyonge wao na kumkimbilia kwao Mwenyezi Mungu wanapo kuwa katika khofu, na wanapo kuwa na nguvu na wakawa katika usalama wanavyo mshirikisha Mwenyezi Mungu. Kisha akaeleza neema zake anazo wapa katika Nyumba Takatifu ya Makka, na wanavyo zikanya neema hizo. Kisha Mwenyezi Mungu akabainisha fadhila za wanao pigana Jihadi.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

 

1. Alif Lam Mim (A.L.M.) Maelezo

2. Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe? Maelezo

3. Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo. Maelezo

4. Au wanadhani wanao tenda maovu kwamba watatushinda? Hukumu mbaya hiyo wanayo hukumu. Maelezo

5. Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu itafika bila ya shaka. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. Maelezo

6. Na anaye fanya juhudi basi bila ya shaka anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake. Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu. Maelezo

7. Na walio amini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa yao, na tutawalipa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

8. Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii. Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

9. Na walio amini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawatia miongoni mwa watu wema. Maelezo

10. Na katika watu wapo wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu. Lakini wanapo pewa maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya mateso ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka kwa Mola wako Mlezi husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliomo vifuani mwa walimwengu? Maelezo

11. Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio amini, na atawatambulisha wanaafiki. Maelezo

12. Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo. Maelezo

13. Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa wakiyazua. Maelezo

14. Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka khamsini. Basi tufani liliwachukua, nao ni madhaalimu. Maelezo

15. Nasi tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na tukaifanya kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote. Maelezo

16. Na Ibrahim pale alipo waambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na mcheni Yeye. Hiyo ndiyo kheri yenu, ikiwa nyinyi mnajua. Maelezo

17. Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa. Maelezo

18. Na mkikadhibisha, basi kaumu kadhaa wa kadhaa za kabla yenu zilikwisha kadhibisha. Na si juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe waziwazi. Maelezo

19. Je! Wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyo anzisha uumbaji, na kisha akarudisha tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. Maelezo

20. Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu. Maelezo

21. Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake Yeye mtapelekwa. Maelezo

22. Na nyinyi si wenye kushinda katika ardhi wala katika mbingu. Wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Maelezo

23. Na walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye, hao ndio wenye kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wenye kupata adhabu chungu. Maelezo

24. Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini. Maelezo

25. Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makaazi yenu ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuruni. Maelezo

26. Lut'i akamuamini, na akasema: Mimi nahamia kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Maelezo

27. Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika dhuriya zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema. Maelezo

28. Na pale Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa hayo. Maelezo

29. Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli. Maelezo

30. Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu mafisadi hawa! Maelezo

31. Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika sisi hapana shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu. Maelezo

32. Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe aliye miongoni mwa watao kaa nyuma. Maelezo

33. Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, alihuzunika kwa ajili yao, na moyo uliona dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usiogope, wala usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni mwa watao kaa nyuma. Maelezo

34. Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya uchafu wanao ufanya. Maelezo

35. Na tumeacha katika mji huo Ishara ilio wazi kwa watu wanao tumia akili zao. Maelezo

36. Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msende katika ardhi mkifisidi. Maelezo

37. Lakini walimkanusha basi ukawatwaa mtikiso wa ardhi, wakapambazukiwa ndani ya nyumba zao nao wamefudikia. Maelezo

38. Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha kubainikieni kutokana na maskani zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia, na hali walikuwa wenye kuona. Maelezo

39. Na pia Qaruni na Firauni na Hamana! Na Musa aliwajia kwa Ishara waziwazi, lakini walijivuna katika nchi, wala hawakuweza kushinda. Maelezo

40. Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Kati yao wapo tulio wapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walio nyakuliwa na ukelele; na kati yao wapo ambao tulio wadidimiza katika ardhi; na kati yao wapo tulio wazamisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu nafsi zao. Maelezo

41. Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua. Maelezo

42. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanacho kiomba badala yake Yeye. Na Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima. Maelezo

43. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaifahamu ila wenye ilimu. Maelezo

44. Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Kwa hakika katika hayo ipo Ishara kwa Waumini. Maelezo

45. SOMA uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda. Maelezo

46. Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake. Maelezo

47. Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri. Maelezo

48. Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka wavunjifu. Maelezo

49. Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya walio pewa ilimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa wenye kudhulumu. Maelezo

50. Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha tu. Maelezo

51. Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki wanacho somewa? Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu wanao amini. Maelezo

52. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi. Anayajua yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu na wakamkataa Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri. Maelezo

53. Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana wakati maalumu ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea kwa ghafla, na hali wao hawana khabari. Maelezo

54. Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali Jahannamu kwa hakika imewazunguka makafiri! Maelezo

55. Siku itapo wafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyatenda! Maelezo

56. Enyi waja wangu mlio amini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu. Maelezo

57. Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu. Maelezo

58. Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao  Maelezo

 

59. Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi. Maelezo

60. Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi Mungu anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua. Maelezo

61. Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akafanya jua na mwezi kuti'ii amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi wanako geuzwa? Maelezo

62. Mwenyezi Mungu humkunjulia, na humdhikishia, riziki amtakaye katika waja wake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. Maelezo

63. Na ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi katika wao hawafahamu. Maelezo

64. Na haya maisha ya dunia si chochote ila ni pumbao na mchezo. Na nyumba ya Akhera ndiyo maisha khasa; laiti wangeli kuwa wanajua! Maelezo

65. Na wanapo panda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia ut'iifu. Lakini anapo wavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha. Maelezo

66. Wapate kuyakanya tuliyo wapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja jua! Maelezo

67. Je! Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wengine wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu, na neema za Mwenyezi Mungu wanazikataa? Maelezo

68. Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu au anaye kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya makafiri? Maelezo

69. Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema. Maelezo ¬ ¬ 


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani