Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

30. SURAT AR-RUM

(Imeteremka Makka)

SURA hii imeanza kutaja kushindwa kwa dola ya Rumi, na ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa Waumini kwamba atawapa ushindi kuwashinda Waajemi, na ikawataka watu wafikiri juu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu, na watembee katika ardhi wapate kuujua mwisho wa makafiri walio iamirisha ardhi zaidi kuliko walivyo iamirisha wao Makureshi. Na Sura hii imeeleza hali ya watu Siku ya Kiyama, na ikasifu kutakasa kwa Waumini kumtakasa Mwenyezi Mungu, na wanavyo muabudu Yeye asubuhi mapema na jioni, na adhuhuri na alasiri. Na ikanabihisha dalili za Upweke wake Mwenyezi Mungu kwa kupishana zamu usiku na mchana, na kukhitalifiana lugha, na mambo yanayo onekana ya ulimwengu katika mbingu na ardhi. Na ikapiga mifano ambayo inayo onyesha upotovu wa shirki, na ikawakumbusha watu vipi Mwenyezi Mungu alivyo waumba wao na akawaneemesha, na kuvitia nguvu viungo vya ukoo, na kushikamana kwa ujamaa, na ikashughulikia mambo ya sharia, ikaharimisha riba, na ikalazimisha Zaka, na ikahimiza kuwafanyia wema jamaa.
Kisha Mwenyezi Mungu Subhanahu akawaneemesha waja wake na akawataka washike Dini na ut'iifu, na akawataka waangalie katika ulimwengu yale maajabu yake yanayo onyesha ukomo wa nguvu na uweza. Na akabainisha mabadiliko ya binaadamu anavyo geuka mpaka akafikia umri wa ukongwe kabisa.
    Na Aya za mwisho zimegusia Siku ya Kiyama na jinsi washirikina wanavyo ikanya. Na Sura ikakhitimishia kwa kumnasihi Mtume s.a.w. athibiti juu ya Haki, na avumilie kwa yanayo mfika, kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu inakuja tu bila ya muhali wowote.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alif Lam Mim (A.L.M.) Maelezo

2. Warumi wameshindwa,  Maelezo

3. Katika nchi iliyo karibu. Nao baada ya kushindwa kwao watashinda Maelezo

 

4. Katika miaka michache. Amri ni ya Mwenyezi Mungu kabla yake na baada yake. Na siku hiyo Waumini watafurahi.  Maelezo

5. Kwa nusura ya Mwenyezi Mungu humnusuru amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu. Maelezo

 

6. Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini watu wengi hawajui. Maelezo

7. Wanajua hali ya dhaahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na Akhera. Maelezo

8. Je! Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake ila kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu wengi bila ya shaka ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao Mlezi. Maelezo

9. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao, na wakaitimbua ardhi na wakaistawisha zaidi kuliko walivyo istawisha wao. Na Mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao. Maelezo

10. Kisha ulikuwa mwisho wa walio fanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia maskhara. Maelezo

11. Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili, na kisha mtarejeshwa kwake. Maelezo

12. Na itapo simama Saa wakosefu watakata tamaa. Maelezo

13. Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa walio kuwa wakiwashirikisha na Mungu; na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa wao. Maelezo

14. Na siku itapo simama Saa, siku hiyo watagawanyika. Maelezo

15. Ama walio amini na wakatenda mema watafurahishwa katika Bustani. Maelezo

16. Na ama walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu na mkutano wa Akhera, hao basi watahudhurishwa katika adhabu. Maelezo

17. Basi Subhanallah! Mtakaseni Mwenyezi Mungu jioni na asubuhi, Maelezo

18. Na sifa zote njema ni zake katika mbingu na ardhi, na alasiri na adhuhuri. Maelezo

19. Hukitoa kilicho hai kutokana na kilicho kufa, na hukitoa kilicho kufa kutokana na kilicho hai. Na huihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Na kama hivyo ndivyo mtavyo fufuliwa. Maelezo

20. Na katika Ishara zake ni kuwa kakuumbeni kwa udongo. Kisha mmekuwa watu mlio tawanyika kote kote. Maelezo

21. Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri. Maelezo

22. Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na kutafautiana ndimi zenu na rangi zenu. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa wajuzi. Maelezo

23. Na katika Ishara zake ni kulala kwenu usiku na mchana, na kutafuta kwenu fadhila zake. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao sikia. Maelezo

24. Na katika Ishara zake hukuonyesheni umeme kwa kukutieni khofu na tamaa. Na hukuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao zingatia. Maelezo

25. Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri yake. Kisha atakapo kuiteni mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi. Maelezo

26. Na vyake Yeye vilivyo mbinguni na katika ardhi. Vyote vinamt'ii Yeye. Maelezo

27. Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Maelezo

28. Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika hao iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyo kuruzukuni, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyo ogopana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili. Maelezo

29. Bali walio dhulumu wamefuata mapendo ya nafsi zao pasina kujua. Basi nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha apotee? Wala hao hawatakuwa na wa kuwanusuru. Maelezo

30. Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui. Maelezo

31. Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na shikeni Sala, na wala msiwe katika washirikina. Maelezo

32. Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho. Maelezo

33. Yakiwapata watu madhara humwomba Mola wao Mlezi nao wametubu kwake. Kisha akiwaonjesha rehema itokayo kwake, mara kikundi miongoni mwao humshirikisha Mola wao Mlezi, Maelezo

34. Kwa kuyakataa tuliyo wapa. Basi stareheni. Mtakuja jua! Maelezo

35. Au tumewateremshia hoja ambayo kwayo ndio wanafanya ushirikina? Maelezo

36. Na watu tunapo waonjesha rehema huifurahia, na ukiwasibu uovu kwa iliyo yatanguliza mikono yao wenyewe, mara wanakata tamaa. Maelezo

37. Kwani hawaoni kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humdhikisha amtakaye? Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini. Maelezo

38. Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na msafiri. Hayo ni kheri kwa watakao radhi ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufanikiwa. Maelezo

39. Na mnacho kitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnacho kitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watao zidishiwa. Maelezo

40. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni, kisha akakuruzukuni, kisha anakufisheni, na kisha anakufufueni. Je! Yupo yeyote katika hao mnao washirikisha na Mwenyezi Mungu afanyae lolote katika hayo? Yeye ametakasika, na ametukuka na hayo mnayo mshirikisha naye. Maelezo

41. Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu. Maelezo

42. Sema: Safirini duniani muangalie ulikuwaje mwisho wa walio tangulia. Wengi wao walikuwa washirikina. Maelezo

43. Basi uelekeze uso wako kwenye Dini Iliyo Nyooka kabla ya kufika Siku hiyo isiyo zuilika, inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watatengana. Maelezo

44. Anaye kufuru basi ukafiri wake utakuwa juu yake mwenyewe, na anaye tenda mema, basi wanazitengezea nafsi zao. Maelezo

45. Ili awalipe walio amini na wakatenda mema kutokana na fadhila yake. Hakika Yeye hawapendi makafiri. Maelezo

46. Na katika Ishara zake ni kuzituma pepo ziletazo bishara njema, na ili kukuonjesheni baadhi ya rehema zake, na ili majahazi yende kwa amri yake; na mtafute kutokana na fadhila yake, na ili mumshukuru. Maelezo

47. Na hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao, na wakawajia kwa hoja zilizo wazi. Tukawaadhibu wale walio fanya ukosefu. Na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini. Maelezo

48. Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma pepo zikayatimua mawingu, kisha akayatandaza mbinguni kama apendavyo. Na akayafanya mapande mapande, basi ukaiona mvua inatoka ndani yake. Anapo wafikishia awatakao katika waja wake, mara hao huwa na furaha. Maelezo

49. Na ingawa kabla ya kuteremshiwa walikuwa wenye kukata tamaa. Maelezo

50. Basi ziangalie athari za rehema ya Mwenyezi Mungu, jinsi anavyo ihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Basi hakika huyo ndiye bila ya shaka Mwenye kuhuisha wafu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu. Maelezo

51. Na tunge utuma upepo na wakauona umekuwa rangi ya manjano, juu ya hayo wange endelea kukufuru. Maelezo

52. Kwani wewe hakika huwafanyi maiti wakasikia, wala viziwi wakasikia wito wakisha geuka kukupa mgongo. Maelezo

53. Wala wewe huwaongoi vipofu na upotovu wao. Huwasikilizishi ila wanao ziamini Aya zetu. Hao ndio Waislamu, walio nyenyekea. Maelezo

54. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na udhaifu kisha akajaalia nguvu baada ya unyonge, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge tena na ukongwe. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza. Maelezo

55. Na siku itapo simama Saa wakosefu wataapa kwamba hawakukaa duniani ila saa moja tu. Hivyo ndivyo walivyo kuwa wakipotozwa. Maelezo

56. Na walio pewa ilimu na Imani watasema: Hakika nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu ya Mwenyezi Mungu mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo Siku ya kufufuliwa! Lakini nyinyi mlikuwa hamuijui. Maelezo

57. Basi Siku hiyo hautawafaa walio dhulumu udhuru wao, wala haitotakiwa toba yao. Maelezo

58. Na hakika tulikwisha wapigia watu kila mfano katika hii Qur'ani. Na ukiwaletea Ishara yoyote hapana shaka walio kufuru watasema: Nyinyi si chochote ila ni waongo. Maelezo

59. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga muhuri kwenye nyoyo za wasio jua. Maelezo

60. Basi subiri. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Wala wasikupaparishe hao wasio kuwa na yakini. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani