Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

 

33. SURAT AL-AH'ZAB

(Imeteremka Madina)

 

Sura  hii imeanza kwa kumtaka Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. amche Mwenyezi Mungu na amtegemee Yeye. Tena ikaingia kuzungumza juu ya mas-ala ya watoto wa kupanga, na ikakataa kuwa hao wana wanao walea kuwa ni watoto wao khasa. Na ikataja mapenzi na ut'iifu wa Mwenyezi Mungu alio wajibisha kwa ajili ya Mtume wake, na hishima na kuwatukuza Mamama wa Waumini, yaani wake za Mtume. Na Sura imeeleza ahadi aliyo ichukua Mwenyezi Mungu kwa Manabii kuwa wafikishe ujumbe; na ikafafanua khabari za Vita vya Ah'zab (Makundi) na khofu na misukosuko iliyo kuwako, na vipi mwishoe Waumini wakashinda na ahadi ya Mwenyezi Mungu ikatimia. Na Sura hii ikashughulikia kutaja adabu ambazo zinawapasa wake za Mtume kuzifuata, na wajilazimishe nafsi zao kuzishika. Tena ikaangukia kuzungumza juu ya watoto wa kupanga, na ikavunja ada ya siku za kijahiliya, za ujinga, ilipo kuwa kuharimisha mtu kuoana na mwana wa kupanga ambaye kwa hakika ni halali yake. Na Sura ikamsifu Mtume s.a.w. na ikamthibitishia aliyo kuwa anastahiki. Na ikausia kustareheshwa na kumwacha kwa wema mwanamke anaye pewa talaka kabla ya kuingia harusi. Na ikamkhusisha Mtume s.a.w. kuwa imemhalalishia mwanamke aliye jitolea kuolewa naye, na ikasema wazi kuwa si halali kwake kuzidisha kuowa wanawake wengine baada ya hao tisa alio kuwa nao. Kisha Sura tukufu ikabainisha yanayo wajibikia Waumini kuyafuata wanapo ingia nyumba za Nabii kwa ajili ya kula, na kuwa wakisha wende zao, na juu ya kuwauliza wake zake nyuma ya pazia. Na Sura ikawataka Mamama wa Waumini (wake za Mtume s.a.w.) wateremshe mitandio yao juu ya vifua vyao. Na Sura ikazungumza juu ya Saa na vitisho vya Kiyama, na ikatoa nasaha ya kumcha Mwenyezi Mungu, na kusema maneno yaliyo sawa, na ikakhitimishia kwa kutaja jukumu la Mwenyezi Mungu alilo libeba mwanaadamu, hali mbingu na ardhi na milima ilishindwa kulibeba.
Kutokana na hayo inaonekana kuwa makusudio  muhimu kabisa ya Sura hii ni: Maneno juu ya watoto wa kupanga, na kuivunja ada iliyo kuwa imeenea wakati ule kuharimisha kuwaoa wana wa kupanga ambao ni halali kwao; na ihsani ya Mwenyezi Mungu kuwafanyia Waumini kwa ushindi kuwashinda washirikina kama alivyo waahidi; na kufafanua sharia aliyo wawekea Mwenyezi Mungu Waumini wanapo ingia nyumba za Nabii s.a.w. na kuwaharimishia kuwaoa wake zake baada yake, na kuzipanga adabu makhsusi zilizo wakhusu Mamama wa Waumini, yaani wake za Mtume s.a.w.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ewe Nabii! Mche Mwenyezi Mungu wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima. Maelezo

2. Na fuata uliyo funuliwa kwa wahyi kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda. Maelezo

3. Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa. Maelezo

4. Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake. Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoa Njia. Maelezo

5. Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo

6. Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko Waumini wengine na Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu. Haya yamekwisha andikwa Kitabuni. Maelezo

7. Na tulipo chukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu, Maelezo

8. Ili (Mwenyezi Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri adhabu chungu. Maelezo

9. Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu. Pale yalipo kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda. Maelezo

10. Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho yalipo kodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali. Maelezo

11. Hapo ndipo Waumini walipo jaribiwa, na wakatikiswa mtikiso mkali. Maelezo

12. Na walipo sema wanaafiki na wale wenye maradhi katika nyoyo zao: Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu. Maelezo

13. Na kundi moja katika miongoni mwao lilipo sema: Enyi watu wa Yathrib! Hapana kukaa nyinyi! Rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa tupu; hawakutaka ila kukimbia tu. Maelezo

14. Na lau kuwa wangeli ingiliwa kwa pande zote, kisha wakatakiwa kufanya khiana, wangeli fanya, na wasingeli sita ila kidogo tu. Maelezo

15. Na hakika walikwisha muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kwamba hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa. Maelezo

16. Sema: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa mnakimbia mauti au kuuwawa, na hata hivyo hamtastareheshwa ila kidogo tu. Maelezo

17. Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi akikutakieni uovu, au akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Maelezo

18. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanao zuilia, na wanao waambia ndugu zao: Njooni kwetu! Wala hawaingii vitani ila kidogo tu. Maelezo

19. Wana choyo juu yenu. Ikifika khofu utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka, kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na khofu ikiondoka wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibat'ilisha vitendo vyao. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. Maelezo

20. Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo makundi watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza khabari zenu. Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani ila kidogo tu. Maelezo

21. Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana. Maelezo

22. Na Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu. Maelezo

23. Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo. Maelezo

24. Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao, na awaadhibu wanaafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo

25. Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya ghadhabu yao; hawakupata kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini katika vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na uweza. Maelezo

26. Na akawateremsha wale walio wasaidia (maadui) katika Watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao. Baadhi yao mkawa mnawauwa, na wengine mnawateka. Maelezo

27. Na akakurithisheni ardhi zao na nyumba zao na mali zao, na ardhi msiyo pata kuikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Maelezo

28. Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri. Maelezo

29. Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa. Maelezo

30. Enyi wake wa Nabii! Atakaye fanya uchafu dhaahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. Maelezo

31. NA MIONGONI mwenu atakeye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akatenda mema, tutampa malipo yake mara mbili, na tutamwandalia riziki ya ukarimu. Maelezo

32. Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema. Maelezo

33. Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni baarabara. Maelezo

34. Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Mwenyezi Mungu na hikima. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri, na Mwenye khabari. Maelezo

35. Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa. Maelezo

36. Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi. Maelezo

37. Na ulipo mwambia yule Mwenyezi Mungu aliye mneemesha, nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako aliyo taka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja naye tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapo kuwa wamekwisha timiza nao shuruti za t'alaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa. Maelezo

38. Hapana ubaya kwa Nabii kufanya aliyo mhalalishia Mwenyezi Mungu. Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa walio pita zamani. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni kudura iliyo kwisha kadiriwa. Maelezo

39. (Hao wa zamani) walio kuwa wakifikisha risala za Mwenyezi Mungu na wanamwogopa Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhisabu. Maelezo

40. Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. Maelezo

41. Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru. . Maelezo

42. Na mtakaseni asubuhi na jioni. Maelezo

43. Yeye na Malaika wake ndio wanakurehemuni ili kukutoeni gizani mwende kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini. Maelezo

44. Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa: Salama! Na amewaandalia malipo ya ukarimu. Maelezo

45. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na mwonyaji, Maelezo

46. Na mwitaji kumwendea Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa yenye kutoa nuru. Maelezo

47. Na wabashirie Waumini ya kwamba wana fadhila kubwa inayo toka kwa Mwenyezi Mungu. Maelezo

48. Wala usiwat'ii makafiri na wanaafiki, na usijali udhia wao. Nawe mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa. Maelezo

49. Enyi mlio amini! Mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha mkawapa t'alaka kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayo ihisabu. Basi wapeni cha kuwaliwaza, na muwawache kwa kuwachana kwa wema. Maelezo

50. Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari yao, na ulio wamiliki kwa mkono wako wa kulia katika alio kupa Mwenyezi Mungu, na mabinti ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada za mama yako walio hama pamoja nawe; na mwanamke Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, kama mwenyewe Nabii akitaka kumwoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Sisi tunajua tuliyo wafaridhia wao katika wake zao na wanawake ilio wamiliki mikono yao ya kulia. Ili isiwe dhiki kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo

51. Unaweza kuakhirisha zamu kwa umtakaye katika wao, na umsogeze umtakaye. Na kama ukimtaka yule uliye mtenga, basi si vibaya kwako. Kufanya hivi kutapelekea yaburudike macho yao, wala wasihuzunike, na wawe radhi juu ya kile unacho wapa wao wote. Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima. Maelezo

52. Baada ya hawa hawakuhalalikii wewe wanawake wengine, wala kuwabadilisha kwa wake wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza; isipo kuwa yule uliye mmiliki kwa mkono wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu. Maelezo

53. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapo itwa basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapo wauliza wakeze haja waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haikufalieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Maelezo

54. Mkidhihirisha chochote kile, au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. Maelezo

55. Hapana ubaya kwao (wake za Mtume) kuonana na baba zao, wala watoto wao, wala ndugu zao, wala watoto wa ndugu zao wanaume, wala watoto wa ndugu zao wanawake, wala wanawake wenzao, wala wale iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Na enyi wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu. Maelezo

56. Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu. Maelezo

57. Hakika wanao muudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehi. Maelezo

58. Na wale wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilio dhaahiri. Maelezo

59. Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo

60. Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitna katika Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu. Maelezo

61. Wamelaanika! Popote watakapo onekana watakamatwa na watauliwa kabisa. Maelezo

62. Hii ni ada ya Mwenyezi Mungu iliyo kuwa kwa wale walio pita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Mwenyezi Mungu. Maelezo

63. Watu wanakuuliza khabari ya Saa (ya Kiyama). Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu. Na nini kitakujuvya? Pengine hiyo Saa iko karibu. Maelezo

64. Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto unao waka kwa nguvu. Maelezo

65. Watadumu humo milele. Hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru. Maelezo

66. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungeli mt'ii Mwenyezi Mungu, na tungeli mt'ii Mtume! Maelezo

67. Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwat'ii bwana zetu na wakubwa wetu; nao ndio walio tupoteza njia. Maelezo

68. Mola wetu Mlezi! Wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana kubwa. Maelezo

69. Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio mtaabisha Musa, lakini Mwenyezi Mungu akamtakasa na waliyo yasema, naye alikuwa mwenye hishima mbele ya Mwenyezi Mungu. Maelezo

70. Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawasawa. Maelezo

71. Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na akusameheni madhambi yenu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa. Maelezo

72. Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima; na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu akaichukua. Hakika yeye amekuwa dhaalimu mjinga. Maelezo

73. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu anawaadhibu wanaafiki wanaume, na wanaafiki wanawake, na washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na anawapokelea toba Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani