Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

 

37. SURAT ASS'AFFAT

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanza kwa kiapo kwa mataifa miongoni mwa viumbe vya Mwenyezi Mungu ambayo yana sifa ya kujipanga kwa safu, na kuzuia, na kusoma. Kiapo hicho ni kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mmoja. Na Ishara zinashuhudia kwa hayo. Kwani Yeye ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, na  Yeye ni Mola Mlezi wa mashariki na magharibi, ambaye aliye ipamba mbingu ya dunia kwa nyota, na akaifanya ihifadhike na muasi aliye acha ut'iifu wa Mwenyezi Mungu. Na baada ya kuthibitisha itikadi ya Tawhidi, Sura imeendelea kuthibitisha itikadi ya kufufuliwa. Na ikawahadharisha wenye kutia shaka kuwa huko kufufuliwa kutawazukia ghafla nao wanaona. Na ikazileta dalili za kumkinika huko, bali wepesi wa kutokea kwake, na hali wao wanayaona hayo na wanasema: Hii ndiyo Siku ya Hisabu! Na wataambiwa: Hii ndiyo Siku ya mpambanuo mlio kuwa mkiikanusha. Na watakusanywa madhaalimu na walivyo kuwa wakiviabudu.  Na watasailiwa na watahojiwa. Na watakuwa wakisingiziana wao kwa wao madhambi walio yapata, na hali wote watakuwa wanashirikiana pamoja katika adhabu. Kwani walijivuna wakakataa kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, na wakamsingizia Mtume wao kuwa ana kichaa na wazimu; na hali kuwa hapana shaka kuwa kawajia na Haki. Na Mitume wamesema kweli katika waliyo kuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Waumini wenye ikhlasi watastareheshwa kwa kila namna ya neema. Na watazikumbuka neema za Mwenyezi Mungu. Watawatokea watu waovu, na watawaona katikati ya Moto wa Jahim. Watamhimidi Mwenyezi Mungu kwa alivyo walinda, na walivyo okoka wasifuate wito wa wale waovu. Baada ya hayo Sura ikaingia ikieleza mashukio ya walio dhulumu na mashukio ya Waumini. Tena ikafuatiliza kwa kueleza khabari za Mitume wengine ili kumpoza Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kuwapa mawaidha watu wake wanao pinga. Na baada ya hadithi mbali mbali za zama mbali mbali na watu mbali mbali, zilizo eleza cheo cha Ujumbe na Wajumbe wenyewe, Sura imetengua madai ya washirikina kwamba Mwenyezi Mungu ana mabinti na wao wana watoto wanaume. Na kwamba Yeye amewafanya Malaika ni wanawake. Na kwamba ipo nasaba ya kukhusiana baina yake na majini. Mwenyezi Mungu Ametakasika na hayo wanayo yazua. Na waja wake ndio watanusuriwa, na jeshi lake ndilo litakalo shinda. Na adhabu yake itaifanya ovu asubuhi ya wanao onywa. Na Sura ikakhitimisha kwa kumtakasa Mola Mlezi wa Utukufu na hayo wanayo mzulia. Na amani ishuke kwa Mitume wote, na Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa wanao jipanga kwa safu. Maelezo

2. Na kwa wenye kukataza mabaya. Maelezo

3. Na kwa wenye kusoma Ukumbusho. Maelezo

4. Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja. Maelezo

5. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote. Maelezo

6. Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota. Maelezo

7. Na kulinda na kila shet'ani a'si. Maelezo

8. Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande. Maelezo

9. Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu. Maelezo

10. Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng'ara. Maelezo

11. Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata. Maelezo

12. Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara. Maelezo

13. Na wanapo kumbushwa hawakumbuki. Maelezo

14. Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara. Maelezo

15. Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri. Maelezo

16. Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa? Maelezo

17. Hata baba zetu wa zamani? Maelezo

18. Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili. Maelezo

19. Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona! Maelezo

20. Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo. Maelezo

21. Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha. Maelezo

22. Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu - Maelezo

23. Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu! Maelezo

24. Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa: Maelezo

25. Mna nini? Mbona hamsaidiani? Maelezo

26. Bali hii leo, watasalimu amri. Maelezo

27. Watakabiliana wao kwa wao kuulizana. Maelezo

28. Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia. Maelezo

29. Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini. Maelezo

30. Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu. Maelezo

31. Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu. Maelezo

32. Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu. Maelezo

33. Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja. Maelezo

34. Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu. Maelezo

35. Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa 'Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna. Maelezo

36. Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu? Maelezo

37. Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume. Maelezo

38. Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu. Maelezo

39. Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya. Maelezo

40. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. Maelezo

41. Hao ndio watakao pata riziki maalumu, Maelezo

42. Matunda, nao watahishimiwa. Maelezo

43. Katika Bustani za neema. Maelezo

44. Wako juu ya viti wamekabiliana. Maelezo

45. Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem Maelezo

46. Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao. Maelezo

47. Hakina madhara, wala hakiwaleweshi. Maelezo

48. Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri. Maelezo

49. Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika. Maelezo

50. Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe. Maelezo

51. Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki Maelezo

52. Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki Maelezo

53. Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa? Maelezo

54. Atasema: Je! Nyie mnawaona? Maelezo

55. Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu. Maelezo

56. Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza. Maelezo

57. Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa. Maelezo

58. Je! Sisi hatutakufa, Maelezo

59. Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa. Maelezo

60. Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa. Maelezo

61. Kwa mfano wa haya nawatende watendao. Maelezo

62. Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum? Maelezo

63. Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu. Maelezo

64. Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu. Maelezo

65. Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet'ani. Maelezo

66. Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo. Maelezo

67. Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka. Maelezo

68. Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu. Maelezo

69. Hakika waliwakuta baba zao wamepotea. Maelezo

70. Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao. Maelezo

71. Na bila ya shaka walikwisha potea kabla yao wengi wa watu wa zamani. Maelezo

72. Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji. Maelezo

73. Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa walio onywa. Maelezo

74. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa. Maelezo

75. Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji. Maelezo

76. Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa. Maelezo

77. Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia. Maelezo

78. Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye. Maelezo

79. Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote! Maelezo

80. Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. Maelezo

81. Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. Maelezo

82. Kisha tukawazamisha wale wengine. Maelezo

83. Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake, Maelezo

84. Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima. Maelezo

85. Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini? Maelezo

86. Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu? Maelezo

87. Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote? Maelezo

88. Kisha akapiga jicho kutazama nyota. Maelezo

89. Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa! Maelezo

90. Nao wakamwacha, wakampa kisogo. Maelezo

91. Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli? Maelezo

92. Mna nini hata hamsemi? Maelezo

93. Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia. Maelezo

94. Basi wakamjia upesi upesi. Maelezo

95. Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe? Maelezo

96. Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya! Maelezo

97. Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo! Maelezo

98. Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini. Maelezo

99. Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa. Maelezo

100. Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema. Maelezo

101. Basi tukambashiria mwana aliye mpole. Maelezo

102. Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri. Maelezo

103. Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji. Maelezo

104. Tulimwita: Ewe Ibrahim! Maelezo

105. Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema. Maelezo

106. Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri. Maelezo

107. Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu. Maelezo

108. Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye. Maelezo

109. Iwe salama kwa Ibrahim! Maelezo

110. Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema. Maelezo

111. Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. Maelezo

112. Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema. Maelezo

113. Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi. Maelezo

114. Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni. Maelezo

115. Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa. Maelezo

116. Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda. Maelezo

117. Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha. Maelezo

118. Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

119. Na tukawaachia (sifa njema) katika watu walio kuja baadaye. Maelezo

120. Iwe salama kwa Musa na Haruni! Maelezo

121. Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. Maelezo

122. Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini. Maelezo

123. Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume. Maelezo

124. Alipo waambia watu wake: Hamwogopi? Maelezo

125. Mnamwomba Baa'li na mnamwacha Mbora wa waumbaji, Maelezo

126. Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani? Maelezo

127. Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa; Maelezo

128. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. Maelezo

129. Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye. Maelezo

130. Iwe salama kwa Ilyas. Maelezo

131. Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema. Maelezo

132. Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini. Maelezo

133. Na hakika Lut'i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume. Maelezo

134. Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote, Maelezo

135. Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma. Maelezo

136. Kisha tukawaangamiza wale wengineo. Maelezo

137. Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi, Maelezo

138. Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini? Maelezo

139. Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume. Maelezo

140. Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni. Maelezo

141. Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa. Maelezo

142. Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa. Maelezo

143. Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu, Maelezo

144. Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa. Maelezo

145. Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa. Maelezo

146. Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung'unye. Maelezo

147. Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi. Maelezo

148. Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda. Maelezo

149. Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume? Maelezo

 

150. Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia? Maelezo

151. Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema: Maelezo

152. Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo! Maelezo

153. Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume? Maelezo

154. Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi? Maelezo

155. Hamkumbuki? Maelezo

156. Au mnayo hoja iliyo wazi? Maelezo

157. Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli. Maelezo

158. Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa. Maelezo

159. Subhana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia. Maelezo

160. Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. Maelezo

161. Basi hakika nyinyi na mnao waabudu Maelezo

162. Hamwezi kuwapoteza Maelezo

163. Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni. Maelezo

164. Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu. Maelezo

165. Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu. Maelezo

166. Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa. Maelezo

167. Na walikuwapo walio kuwa wakisema: Maelezo

168. Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani, Maelezo

169. Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi. Maelezo

170. Lakini waliukataa. Basi watakuja jua. Maelezo

171. Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa. Maelezo

172. Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa. Maelezo

173. Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda. Maelezo

174. Basi waachilie mbali kwa muda. Maelezo

175. Na watazame, nao wataona. Maelezo

176. Je! Wanaihimiza adhabu yetu? Maelezo

177. Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa. Maelezo

178. Na waache kwa muda. Maelezo

179. Na tazama, na wao wataona. Maelezo

180. Subhana Rabbi'l'Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia. Maelezo

181. Na Salamu juu ya Mitume. Maelezo

182. Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani