Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

 

38. SURAT S'AAD

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii ni ya thalathini na nane katika Sura za Qur'ani Tukufu. Nayo ni Sura ya Makka, na Aya zake ni 88.
Sura hii inatueleza namna ya inda ya washirikina waliyo kuwa wakiufanyia Wito wa Nabii Muhammad s.a.w. na uhasidi wao kwa vile Mwenyezi Mungu alivyo mkirimu kwa kumpa utukufu wa Utume, na kumteremshia Qur'ani. Basi inawajibu kwa yale mawazo ya uwongo walio mnasibishia nayo. Na imebainisha kwamba yaliyo wapelekea kuupiga vita Wito wake kama wafanyavyo si lolote ila ni dharau ya uwongo, na kupenda kuleta khitilafu na mgawanyo. Na lau kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu inge wateremkia, msimamo wao kwa Mtume s.a.w. usingeli kuwa hivyo ulivyo. Kisha Mwenyezi Mungu amewapigia mifano ya kaumu zilizo kwisha tangulia, ili wapate kuacha inadi na kuleta dhiki, na ili kumpa moyo Mtume wake s.a.w. kufikisha Wito, na hata ange pata taabu zozote na vitimbi vyovyote vya washirikina kwa ajili yake. Na apate kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema alizo mpa, kama walivyo fanya ndugu zake Manabii na Mitume wengine. Na kutokea na haya anataja marejeo mema aliyo waandalia Mwenyezi Mungu wachamngu, na maangukio maovu aliyo waandalia wenye kuasi. Kisha akawakumbusha yaliyo kuwa baina ya baba yao Adam a.s. na adui yake Iblisi, ili wajue kuwa anayo waitia Iblisi kufanya kiburi kwa kupinga kufwata haki ni tabia katika tabia zake Iblisi. Na kupanda kiburi huku ndiko kulikuwa sababu ya kufukuzwa kwake kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu.
Sura imekhitimisha kwa kueleza vilivyo kazi muhimu ya Mtume s.a.w., nayo ni kufikisha Wito, na kwamba yeye hawataki ujira kwa hayo, na yeye hakujileta nafsi yake. Na Qur'ani si chochote ila ni Ukumbusho kwa walimwengu wote. Na bila ya shaka watakuja jua ukweli wa khabari zake baadae.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. S'ad, Naapa kwa Qur'ani yenye mawaidha. Maelezo

2. Lakini walio kufuru wamo katika majivuno na upinzani Maelezo

3. Mataifa mangapi tumeyaangamiza kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwisha pita. Maelezo

4. Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anaye tokana nao wenyewe, na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo. Maelezo

5. Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu. Maelezo

6. Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililo pangwa. Maelezo

7. Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu. Maelezo

8. Ati yeye tu ndiye aliye teremshiwa mawaidha peke yake katika sisi? Lakini hao wana shaka na mawaidha yangu, bali hawajaionja adhabu yangu. Maelezo

9. Au wanazo wao khazina za rehema za Mola wako Mlezi, Mwenye nguvu, Mpaji? Maelezo

10. Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo kati yao? Basi nawazipande njia za kwendea huko! Maelezo

11. Hao ni askari watao shindwa miongoni mwa makundi yatayo shindwa. Maelezo

12. Walikanusha kabla yao kaumu ya Nuhu, na kina A'adi na Firauni mwenye majengo. Maelezo

13. Na Thamud na kaumu Lut'i na watu wa Machakani. Hayo ndiyo makundi. Maelezo

14. Hao wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahiki adhabu yangu. Maelezo

15. Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na muda. Maelezo

16. Na wao husema: Mola wetu Mlezi! Tuletee upesi sehemu yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Hisabu. Maelezo

17. Subiri kwa hayo wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daudi, mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia. Maelezo

18. Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye. Maelezo

19. Na pia ndege walio kusanywa makundi kwa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake. Maelezo

20. Na tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa hikima, na kukata hukumu. Maelezo

21. Na je! Imekufikia khabari ya wagombanao walipo pindukia ukuta kuingia chumbani? Maelezo

22. Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Sisi ni wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoe kwenye njia iliyo sawa. Maelezo

23. Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisiini na tisa; na mimi ninaye kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo nikufugie! Na amenishinda kwa maneno. Maelezo

24. Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa walio amini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daudi akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba msamaha Mola wake Mlezi, na akaanguka kusujudu na kutubia. Maelezo

25. Basi tukamsamehe kwa hayo. Naye kwa hakika anao mkaribisho mkubwa na marejeo mazuri kwetu. Maelezo

26. Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika nchi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanao ipotea Njia ya Mwenyezi Mungu wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu. Maelezo

27. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yao bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata. Maelezo

28. Je! Tuwafanye walio amini na wakatenda mema kama wafanyao uharibifu katika nchi? Au tuwafanye wachamngu kama waovu? Maelezo

29. Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili. Maelezo

30. Na Daudi tukamtunukia Suleiman. Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia. Maelezo

31. Alipo pelekewa jioni farasi wasimamao kidete, tayari kutoka shoti; Maelezo

32. Basi akasema: Navipenda vitu vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Kisha wakafichikana nyuma ya boma. Maelezo

33. (Akasema:) Nirudishieni! Akaanza kuwapapasa miguu na shingo. Maelezo

34. Na tulimtia mtihanini Suleiman, na tukauweka mwili juu ya kiti chake, kisha akarejea kwa kutubu. Maelezo

35. Akasema: Mola wangu Mlezi! Nisamehe na unipe ufalme usio mwelekea yeyote baada yangu. Hakika Wewe ndiye Mpaji. Maelezo

36. Basi tukaufanya upepo umtumikie, ukenda kwa amri yake, popote alipo taka kufika. Maelezo

37. Na tukayafanya mashet'ani yamtumikie, wote wajenzi na wapiga mbizi. Maelezo

38. Na wengine wafungwao kwa minyororo. Maelezo

39. Hichi ndicho kipawa chetu. Basi toa au zuia, bila ya hisabu. Maelezo

40. Na hakika yeye kwetu Sisi ana cheo cha kukaribishwa kwetu, na pahala pazuri pa kurejea. Maelezo

41. Na mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwita Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika Shet'ani amenifikishia udhia na adhabu. Maelezo

42. (Akaambiwa:) Piga-piga ardhi kwa mguu wako! Basi haya maji baridi ya kuogea na ya kunywa. Maelezo

43. Na tukampa ahali zake na wengine kama wao pamoja nao, kuwa ni rehema itokayo kwetu, na iwe kumbusho kwa watu wenye akili. Maelezo

44. Na shika kicha cha vijiti tu mkononi mwako, kisha ndio upigie nacho, wala usivunje kiapo. Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu. Maelezo

45. Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na Yaa'qubu walio kuwa na nguvu na busara. Maelezo

46. Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa Akhera. Maelezo

47. Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora. Maelezo

48. Na mkumbuke Ismail na Alyasaa na Dhulkifli, na wote hao ni katika walio bora. Maelezo

49. Huu ni ukumbusho. Na hakika wachamngu wana marudio mazuri. Maelezo

50. Bustani za milele zitazo funguliwa milango yao kwa ajili yao. Maelezo

51. Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji. Maelezo

52. Na pamoja nao wake zao wenye kutuliza macho, hirimu zao. Maelezo

53. Haya ndiyo mliyo ahidiwa kwa Siku ya Hisabu. Maelezo

54. Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyo malizika. Maelezo

55. Ndio hivi! Na hakika wenye kuasi bila ya shaka watapata marudio maovu kabisa; Maelezo

56. Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nacho hicho ni kitanda kiovu mno cha kulalia. Maelezo

57. Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha! Maelezo

58. Na adhabu nyenginezo za namna hii. Maelezo

59. Hili ndilo kundi litakalo ingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho mema kwao. Hakika hao wanaingia Motoni. Maelezo

60. Waseme: Lakini nyinyi! Hamna mapokezi mazuri! Nyinyi ndio mlio tusabibisha haya, napo ni pahala paovu kabisa! Maelezo

61. Waseme: Mola wetu Mlezi! Aliye tusabibisha haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni. Maelezo

62. Watasema: Tuna nini hata hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ndio katika waovu? Maelezo

63. Tulikosea tulipo wafanyia maskhara, au macho yetu tu hayawaoni ? Maelezo

64. Hakika hayo bila ya shaka ndiyo makhasimiano ya watu wa Motoni. Maelezo

65. Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana mungu ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda nguvu, Maelezo

66. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na viliomo baina yake, Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe. Maelezo

67. Sema: Hii ni khabari kubwa kabisa. Maelezo

68. Ambayo nyinyi mnaipuuza. Maelezo

69. Sikuwa na ilimu ya mambo ya viumbe wakuu watukufu walipo kuwa wakishindana. Maelezo

70. Haikufunuliwa kwangu isipo kuwa ya kwamba hakika mimi ni mwonyaji dhaahiri. Maelezo

71. Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo. Maelezo

72. Na nitakapo mkamilisha na kumpulizia roho inayo tokana nami, basi muangukieni kwa kumt'ii. Maelezo

73. Basi Malaika wakat'ii wote pamoja. Maelezo

74. Isipo kuwa Iblisi; alijivuna na akawa katika makafiri. Maelezo

75. Mwenyezi Mungu akamwambia: Ewe Iblisi! Kipi kilicho kuzuia kumt'ii yule niliye muumba kwa mikono yangu? Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli? Maelezo

76. Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye umemuumba kwa udongo. Maelezo

77. Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe umelaanika. Maelezo

78. Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo. Maelezo

79. Akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watayo fufuliwa viumbe. Maelezo

80. Mwenyezi Mungu akasema: Basi umekwisha kuwa miongoni mwa walio pewa muhula, Maelezo

81. Mpaka siku ya wakati maalumu. Maelezo

82. Akasema (Iblisi): Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote, Maelezo

83. Isipo kuwa wale waja wako miongoni mwao walio khitariwa. Maelezo

84. Akasema: Haki! Na haki ninaisema. Maelezo

85. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa hao wote wenye kukufuata miongoni mwao. Maelezo

86. Sema (Ewe Mtume) : Sikuombeni ujira juu ya haya, wala mimi si katika wadanganyifu. Maelezo

87. Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote. Maelezo

88. Na bila ya shaka mtajua khabari zake baada ya muda. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani