Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

43. SURAT AZZUKHRUF

(Imeteremka Makka)

 

Imeanzia Sura hii kwa harufi mbili za alifbete, na ikafuatia kwa kuitaja Qur'ani na kueleza cheo chake kwa Mwenyezi Mungu. Kisha Sura ikaingia kubainisha msimamo wa wale wanao zifanyia maskhara Risala za Mitume wao, na ikazileta dalili nyingi za kuthibitisha Imani ya Mwenyezi Mungu pekee. Na juu ya hoja hizo wao wakamzulia Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika, na wakamfanya kuwa ana watoto wa kike, na wao wanao wa kiume. Na walipo ishiwa na hoja wakashikilia mila za baba zao.
Kisha Sura ikasimulia kisa cha Ibrahim, na ikafuatiliza kule kuyaona makuu makafiri wa Makka ya kwamba Qur'ani iliteremka juu ya Muhammad, wala isiteremke juu ya mmoja katika wakuu wa miji yao miwili. Hayo ni kama kwamba wao ndio wanao zigawanya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu alikwisha wagawia maisha yao ya duniani, kwa kuwa wao wenyewe wameshindwa hayo. Kisha Sura ikathibitisha kwamba lau kuwa si kuchukia wasije watu wote wakakufuru basi bila ya shaka angeli mpa kafiri starehe na mapambo na uzuri wote wa duniani. Kadhaalika Sura imebainisha kwamba mwenye kupuuza Haki Mwenyezi Mungu humsalitisha na Shet'ani amwongoze kwenye maangamio. Kisha Sura inasimulia kisa cha Musa na Firauni, na alivyo ghurika Firauni na ufalme wake, na yaliyo mteremkia Firauni na kaumu yake ya mateso ya Mwenyezi Mungu. Na hayo akafuatiwa  kutajwa Bin Maryamu, na kwamba yeye ni mja aliye neemeshwa na Mwenyezi Mungu, na akawaita watu wende kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na baada ya kuonya  kwa adhabu ya Siku ya Kiyama itayo wapata walio dhulumu, na kubashiriwa Waumini kuwa watapata Pepo ambayo ndani yake macho yao yatatua, Sura inakhitimisha kueleza kuwa Ufalme wa Mwenyezi Mungu umeenea kote, na hao walio washirikisha naye hawanalo wawezalo. Basi, ewe Muhammad! Wapuuzilie mbali, na useme: Salamu! Watakuja jua!


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. H'a Mim Maelezo

2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha. Maelezo

3. Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu. Maelezo

4. Na hakika hiyo imo katika Asili ya Maandiko yalioko kwetu, ni tukufu na yenye hikima. Maelezo

5. Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka kwa ukafiri? Maelezo

6. Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani! Maelezo

7. Na hawajii Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli. Maelezo

8. Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita. Maelezo

9. Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi, Maelezo

10. Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka. Maelezo

11. Na ambaye ndiye aliye teremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na kwa hayo tukaifufua nchi iliyo kufa. Na namna hivi ndivyo mtakavyo tolewa. Maelezo

12. Na ambaye ndiye aliye umba katika kila kitu jike na dume, na akakufanyieni marikebu na wanyama mnao wapanda. Maelezo

13. Ili mkae vizuri migongoni mwao, kisha mkumbuke neema za Mola wenu Mlezi mnapokaa sawa sawa juu yao na mseme: Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe. Maelezo

14. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi. Maelezo

15. Na wanamfanyia katika waja wake fungu. Kwa hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila aliye dhaahiri. Maelezo

16. Au amejichukulia watoto wanawake katika vile alivyo viumba, na akakuteulieni nyinyi watoto wanaume? Maelezo

17. Na anapo bashiriwa mmoja wao kwa yale aliyo mpigia mfano Mwenyezi Mungu, uso wake husawijika na hujaa hasira. Maelezo

18. Ati aliye lelewa katika mapambo, na katika mabishano hawezi kusema kwa bayana...? Maelezo

19. Na wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa Rehema, ni wanawake! Kwani wameshuhudia kuumbwa kwao? Ushahidi wao utaandikwa na wao watahojiwa! Maelezo

20. Nao husema: Angeli penda Mwingi wa Rehema tusingeli waabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu! Maelezo

21. Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hichi, na ikawa wao wanakishikilia hicho? Maelezo

22. Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunaongoza nyayo zao. Maelezo

23. Na kadhaalika hatukumtuma mwonyaji kwenye mji wowote ila watu wake walio deka kwa starehe walisema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, na sisi tunafuata nyayo zao. Maelezo

24. Akasema (Mwonyaji): Hata nikikuleteeni yenye uwongofu bora kuliko mlio wakuta nao baba zenu? Wakasema: Sisi tunayakataa tu hayo mliyo tumwa. Maelezo

25. Basi tukawalipizia. Angalia ulikuwaje mwisho wa walio kadhibisha! Maelezo

26. Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Hakika mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yaabudu, Maelezo

27. Isipo kuwa yule aliye niumba, kwani Yeye ataniongoa. Maelezo

28. Na akalifanya hili liwe neno lenye kubaki katika vizazi vyake ili warejee. Maelezo

29. Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka ikawafikia Haki na Mtume aliye bainisha. Maelezo

30. Na ilipo wafikia Haki wakasema: Huu ni uchawi, na sisi hakika tunaukataa. Maelezo

31. Na walisema: Kwa nini Qur'ani hii haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili hii? Maelezo

32. Kwani wao ndio wanao gawa rehema za Mola wako Mlezi? Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wenginewe wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya. Maelezo

33. Na lau isinge kuwa watu watakuwa kundi moja tungeli wajaalia wanao mkufuru Rahmani wana nyumba zao zina dari ya fedha, na ngazi zao pia wanazo pandia, Maelezo

34. Na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyo egemea juu yake, Maelezo

35. Na mapambo. Lakini hayo si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia tu, na Akhera iliyoko kwa Mola wako Mlezi ni ya wenye kumchamngu. Maelezo

36. Anaye yafanyia upofu maneno ya Rahmani tunamwekea Shet'ani kuwa ndiye rafiki yake. Maelezo

37. Na hakika wao wanawazuilia Njia na wenyewe wanadhani kuwa wameongoka. Maelezo

38. Hata atakapo tujia atasema: Laiti ungeli kuwako baina yangu na wewe kama umbali baina ya mashariki na magharibi. Rafiki mwovu mno wewe! Maelezo

39. Na kwa kuwa mlidhulumu, haitakufaeni kitu leo kwamba nyinyi mnashirikiana katika adhabu. Maelezo

40. Je! Unaweza kuwasikilizisha viziwi, au unaweza kuwaongoa vipofu na waliomo katika upotofu ulio wazi? Maelezo

41. Na hata tukikuondoa, Sisi tutalipiza kisasi chetu kwao. Maelezo

42. Au tutakuonyesha tulio waahidi. Nasi bila ya shaka tuna uweza juu yao. Maelezo

43. Basi wewe yashike yaliyo funuliwa kwako. Hakika wewe uko kwenye Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

44. Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa. Maelezo

45. Na waulize Mitume wetu tulio watuma kabla yako: Je! Tulifanya miungu mingine iabudiwe badala ya Rah'mani? Maelezo

46, Na bila ya shaka tulimtuma Musa kwa Ishara zetu ende kwa Firauni na waheshimiwa wake, na akasema: Hakika mimi ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote! Maelezo

47. Lakini alipo wajia na Ishara zetu wakaingia kuzicheka. Maelezo

48. Na hatukuwaonyesha Ishara yoyote ila hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuliko nyenginewe. Na tukawakamata kwa adhabu ili warejee. Maelezo

49. Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka. Maelezo

50. Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi. Maelezo

51. Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je! Hamwoni? Maelezo

52. Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi? Maelezo

53. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama? Maelezo

54. Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu wapotovu. Maelezo

55. Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawazamisha wote! Maelezo

56. Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye. Maelezo

57. Na alipo pigiwa mfano Mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele. Maelezo

58. Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi! Maelezo

59. Hakuwa yeye (Isa) ila ni Mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili. Maelezo

60. Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika ardhi wakifuatana. Maelezo

61. Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

62. Wala asikuzuilieni Shet'ani. Hakika yeye ni adui yenu wa dhaahiri. Maelezo

63. Na alipo kuja Isa na dalili zilizo wazi, alisema: Nimekujieni na hikima, na ili nikuelezeni baadhi ya yale mliyo khitalifiana. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na mnit'ii mimi. Maelezo

64. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na ni Mola wenu Mlezi. Basi Muabuduni Yeye tu. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka. Maelezo

65. Lakini makundi kwa makundi yao yalikhitalifiana wao kwa wao. Ole wao walio dhulumu kwa adhabu ya siku chungu. Maelezo

66. Je! Nini wanangojea ila Saa iwajie kwa ghafla na wala wao hawatambui? Maelezo

67. Siku hiyo marafiki watakuwa ni maadui, wao kwa wao, isipo kuwa wachamngu. Maelezo

68. Enyi waja wangu! Hamtakuwa na khofu siku hiyo, wala hamtahuzunika. Maelezo

 

69. Ambao waliziamini Ishara zangu na walikuwa Waislamu. Maelezo

70. Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; mtafurahishwa humo. Maelezo

71. Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele. Maelezo

72. Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya. Maelezo

73. Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala. Maelezo

74. Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannamu. Maelezo

75. Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa. Maelezo

76. Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu. Maelezo

77. Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Naye aseme: Hakika nyinyi mtakaa humo humo! Maelezo

78. Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki. Maelezo

79. Au waliweza kupitisha amri yao? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha. Maelezo

80. Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika. Maelezo

81. Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu. Maelezo

82. Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia. Maelezo

83. Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao waliyo ahidiwa. Maelezo

84. Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi. Maelezo

85. Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa. Maelezo

86. Wala hao mnao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa kumwombea mtu, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua. Maelezo

87. Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa? Maelezo

88. Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini. Maelezo

89. Basi wasamehe, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani