Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

44. SURAT ADDUKHAN

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanza kwa kusimulia khabari za Qur'ani, ya kwamba imeteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika usiku wa Lailatul Qadri ulio barikiwa, kwa ajili ya kuonya na Tawhid, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Na kwamba hii Qur'ani ni Haki, Kweli tupu. Hali kadhaalika Sura imesimulia khabari za kufufuliwa, na kwamba hayo hayana shaka ndani yake, na imezibisha hoja za wanao yakanya hayo, na ikawarudi washirikina. Ikalinganisha baina ya washirikina wa Makka na wenzao walio watangulia, nao ni kaumu ya Firauni. Ikaeleza mapatilizo ya Mwenyezi Mungu yaliyo washukia hao. Tena ikatilia mkazo kwamba Siku ya Kiyama ndiyo siku iliyo pangwa ya kuutenga ukafiri na upotovu wote. Na ikasimulia malipo ya wakosefu kwa siku hiyo na malipo ya walio ongoka. Na ikamalizika kama ilivyo anzia kwa mazungumzo juu ya Qur'ani, na kwa kuwaonya wanao kadhibisha Ujumbe wa Mtume s.a.w. kuwa nao wangojee balaa na masaibu yatakayo washukia.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. H'a Mim Maelezo

2. Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha, Maelezo

3. Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji. Maelezo

4. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima, Maelezo

5. Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma. Maelezo

6. Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. Maelezo

7. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini. Maelezo

8. Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo. Maelezo

9. Lakini wao wanacheza katika shaka. Maelezo

10. Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri, Maelezo

11. Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu! Maelezo

12. Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini. Maelezo

13. Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha. Maelezo

14. Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu. Maelezo

15. Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile! Maelezo

16. Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa. Maelezo

17. Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu. Maelezo

18. Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu. Maelezo

19. Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi. Maelezo

20. Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe. Maelezo

21. Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami. Maelezo

22. Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi: Hakika watu hawa ni wakosefu. Maelezo

23. Mwenyezi Mungu akasema: Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa. Maelezo

24. Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalo zamishwa. Maelezo

25. Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha! Maelezo

26. Na mimea na vyeo vitukufu! Maelezo

27. Na neema walizo kuwa wakijistareheshea! Maelezo

28. Ndio hivyo! Na tukawarithisha haya watu wenginewe. Maelezo

29. La mbingu wala ardhi hazikuwalilia, wala hawakupewa muhula. Maelezo

30. Na bila ya shaka tuliwaokoa Wana wa Israili katika adhabu ya kuwadhalilisha, Maelezo

31. Ya Firauni. Hakika yeye alikuwa jeuri katika wenye kupindukia mipaka. Maelezo

32. Na tuliwakhiari kwa ujuzi wetu kuliko walimwengu wenginewe. Maelezo

33. Na tukawapa katika ishara zenye majaribio yaliyo wazi. Maelezo

34. Hakika hawa wanasema: Maelezo

35. Hapana ila kufa kwetu mara ya kwanza tu, wala sisi hatufufuliwi. Maelezo

36. Basi warudisheni baba zetu, ikiwa nyinyi mnasema kweli. Maelezo

37. Je! Ni wao bora au watu wa Tubbaa' na walio kuwa kabla yao? Tuliwaangamiza. Hakika hao walikuwa wakosefu. Maelezo

38. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo. Maelezo

39. Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui. Maelezo

40. Hakika siku ya Uamuzi ni wakati ulio wekwa kwa wao wote. Maelezo

41. Siku ambayo rafiki hatamfaa rafiki yake kwa chochote, wala hawatanusuriwa. Maelezo

42. Isipo kuwa atakaye mrehemu Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. Maelezo

43. Hakika Mti wa Zaqqum, Maelezo

44. Ni chakula cha mwenye dhambi. Maelezo

45. Kama shaba iliyo yayushwa, hutokota matumboni Maelezo

46. Kama kutokota kwa maji ya moto. Maelezo

47. (Itasemwa:) Mkamateni na mtupeni katikati ya Jahannamu! Maelezo

48. Kisha mmwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yanayo chemka. Maelezo

49. Onja! Ati wewe ndiye mwenye nguvu, mtukufu! Maelezo

50. Hakika haya ndiyo mliyo kuwa mkiyatilia shaka. Maelezo

51. Hakika wachamngu watakuwa katika mahali pa amani, Maelezo

52. Katika mabustani na chemchem, Maelezo

53. Watavaa hariri nyepesi na hariri nzito wakikabiliana, Maelezo

54. Hivi ndivyo itakavyo kuwa, na tutawaoza mahurilaini. Maelezo

55. Humo watataka kila aina ya matunda, na wakae kwa amani. Maelezo

56. Humo hawataonja mauti ila mauti yale ya kwanza, na (Mwenyezi Mungu) atawalinda na adhabu ya Jahannamu, Maelezo

57. Kuwa ni fadhila zitokazo kwa Mola wako Mlezi. Huko ndiko kufuzu kukubwa. Maelezo

58. Basi tumeifanya nyepesi hii Qur'ani kwa ulimi wako, ili wapate kukumbuka. Maelezo

59. Ngoja tu, na wao wangoje pia. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani