Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

45. SURAT AL-JAATHIYA

(Imeteremka Makka)

 

Imeanzia Sura hii kwa harufi mbili katika harufi za Alifbete, na ikafuatiliza kwa kubainisha kuwa kuteremshwa Qur'ani kumetokana na Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu Mwenye hikima. Kisha ikazitaja dalili za uumbaji na za kiakili kuthibitisha itikadi ya Imani na kuitia watu waifuate. Hali kadhaalika imekusanya wito kwa wenye kukadhibisha Ishara. Kisha ikaingia kuzihisabu neema za Mwenyezi Mungu na fadhila zake kwa waja wake; na ikawataka Waumini wawasamehe makafiri wanao kanya. Kwani Mwenyezi Mungu peke yake ndiye wa kumlipa kila mtu kwa alilo litenda. Kisha Sura baada ya hayo ikazungumzia vipi Mwenyezi Mungu alivyo wafadhili Wana wa Israili kwa kuwapa neema nyingi, na khitilafu zilizo zuka baina yao ambazo Mwenyezi Mungu atazitolea hukumu Siku ya Kiyama. Kisha ikaingia kufarikisha baina ya walio fuata Haki na walio fuata matamanio, wakakanya kufufuliwa, na wakapinga Ishara  za uweza kwa kutaka wafufuliwe baba zao! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuhuisha, na ndiye Mwenye kufisha. Yeye ana ufalme wa kila kitu. Na siku watakapo kusanywa wapotovu kila nafsi itaitwa ikapokee kitabu chake. Hapo watafuzu Waumini na watakemewa walio takabari. Sura tena inarejea hadithi ya kule kuikataa kwao Saa ya Kiyama, na kuzikadhibisha Ishara zinazo ionyesha; na vile Mwenyezi Mungu atavyo wasahau wao kama wao walivyo isahau hii Siku. Na ikabainisha kuwa makaazi yao ni Motoni kwa kule kuzikejeli kwao Ishara za Mwenyezi Mungu na kudanganyika kwao na dunia. Na Sura imekhitimisha kwa kumsifu Muumba mbingu na ardhi, Mwenye utukufu kote humo, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. H'a Mim Maelezo

2. Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Maelezo

3. Hakika katika mbingu na ardhi ziko Ishara kwa Waumini. Maelezo

4. Na katika umbo lenu na katika wanyama alio watawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini. Maelezo

5. Na kupishana usiku na mchana, na riziki anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na mabadiliko ya upepo, ni Ishara kwa watu wenye akili. Maelezo

6. Hizi Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki; basi hadithi gani watakayo iamini baada ya Mwenyezi Mungu na Aya zake? Maelezo

7. Ole wake kila mzushi mwenye dhambi! Maelezo

8. Anaye sikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, kisha anashikilia yale yale aliyo katazwa, na anajivuna, kama kwamba hakuzisikia. Basi mbashirie adhabu chungu! Maelezo

9. Na anapo kijua kitu kidogo katika Aya zetu hukifanyia mzaha. Watu hao ndio watakao kuwa na adhabu ya kufedhehesha. Maelezo

10. Na nyuma yao ipo Jahannamu. Na walio yachuma hayatawafaa hata kidogo, wala walinzi walio washika badala ya Mwenyezi Mungu. Na watapata adhabu kubwa. Maelezo

11. Huu ni uwongofu. Na wale wale walio zikataa Ishara za Mola wao Mlezi watapata adhabu inayo tokana na ghadhabu iliyo chungu. Maelezo

12. Mwenyezi Mungu ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili humo zipite marikebu kwa amri yake, na ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru. Maelezo

13. Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, vyote vimetoka kwake. Hakika katika hayo zimo Ishara kwa watu wanao fikiri. Maelezo

14. Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji siku za Mwenyezi Mungu, ili awalipe kwa waliyo kuwa wakiyachuma. Maelezo

15. Mwenye kutenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye kutenda uovu ni juu yake mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Mola wenu Mlezi. Maelezo

16. Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu wote. Maelezo

17. Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliyo kuwa baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa wakikhitalifiana. Maelezo

18. Kisha tukakuweka wewe juu ya Njia ya haya mambo, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wasio jua kitu. Maelezo

19. Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni rafiki wa wamchao. Maelezo

20. Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni uwongofu, na rehema kwa watu wanao yakinisha. Maelezo

21. Je! Wanadhani wanao tenda maovu kuwa tutawafanya kama walio amini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu mbaya wanayo ihukumu! Maelezo

22. Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na ili kila nafsi ilipwe yale iliyo yachuma. Nao hawatadhulumiwa. Maelezo

23. Je! Umemwona aliye fanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake, na Mwenyezi Mungu akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga machoni mwake? Basi nani atamwongoa huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki? Maelezo

24. Na walisema: Hapana ila huu uhai wetu wa duniani - twafa na twaishi, na hapana kinacho tuhiliki isipo kuwa dahari. Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu. Maelezo

25. Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi hawana hoja ila kusema: Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasemao kweli. Maelezo

26. Sema: Mwenyezi Mungu anakuhuisheni, kisha anakufisheni, kisha anakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo na shaka. Lakini watu wengi hawajui. Maelezo

27. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Na siku itapo simama Saa ya Kiyama, siku hiyo wataangamia wenye kushikamana na upotovu. Maelezo

28. Na utauona kila umma umepiga magoti, na kila umma utaitwa kwenda soma kitabu chake: Leo mtalipwa mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

29. Hichi kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki. Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

30. Ama walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi atawatia katika rehema yake. Huko ndiko kufuzu kulio wazi. Maelezo

31. Na ama walio kufuru, wataambiwa: Kwani hamkuwa mkisomewa Aya zangu nanyi mkapanda kichwa, na mkawa watu wakosefu? Maelezo

32. Na ikisemwa: Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, na Saa haina shaka, nyinyi mkisema: Hatuijui hiyo Saa, tunadhania dhana tu, wala hatuna yakini. Maelezo

33. Basi ubaya wa waliyo yatenda utawadhihirikia, na yatawazunguka waliyo yafanyia maskhara. Maelezo

34. Na itasemwa: Leo tunakusahauni kama nyinyi mlivyo sahau mkutano wa siku yenu hii; na mahali penu ni Motoni, wala hamna wa kukunusuruni. Maelezo

35. Hayo ni kwa sababu nyinyi mlizifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu; na maisha ya dunia yakakudanganyeni. Basi leo hawatatolewa humo wala hao hawatakubaliwa udhuru wao. Maelezo

36. Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mbingu, na Mola Mlezi wa ardhi, na Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

37. Na ukubwa ni wake Yeye tu, mbinguni na katika ardhi, naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani