Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani  (Nani Yeye?)

 

 

51. SURAT ADH-DHAARIYAAT

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanza kwa kiapo cha ukweli wa kufufuliwa na kutokea malipo. Kisha ikafuatisha kwa kiapo kingine juu ya ubabaishi wa wanao kanya katika maneno yao juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na juu ya Qur'ani tukufu. Kisha ikaingia kuwaonya wanao kanya kuwa watapata mwisho muovu katika Akhera. Tena ikaeleza waliyo ahidiwa wachamngu katika malipo ya vitendo vyao vyema walivyo vitanguliza duniani. Kisha ikawazindua watu wazingatie Ishara za Mwenyezi Mungu katika kuumba kwake, na katika nafsi zao, na katika mambo ya ufundi wa ajabu na uzuri wa umbo alio uweka humo.
Na ikasimulia kisa cha Ibrahim na wageni wake Malaika, kisha ikaeleza hali za baadhi ya mataifa na maangamizo yaliyo wasibu kwa kuwakadhibisha Manabii wao. Kisha ikaashiria kwa jumla baadhi ya Ishara za uumbaji, na ikahimiza watu warejee kwa Mwenyezi Mungu, na wamuabudu Yeye peke yake, ambayo hayo ndio makusudi ya kuumbwa majini na watu. Na Sura imekhitimisha kwa kuwaonya wanao mkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. kuwa watapata adhabu iliyo kwisha wapata kaumu za kabla yao.


 

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

 

1. Naapa kwa pepo zinazo tawanya, Maelezo

2. Na zinazo beba mizigo, Maelezo

3. Na zinazo kwenda kwa wepesi. Maelezo

4. Na zinazo gawanya kwa amri, Maelezo

5. Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli, Maelezo

6. Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea. Maelezo

7. Naapa kwa mbingu zenye njia, Maelezo

8. Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana. Maelezo

9. Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa. Maelezo

10. Wazushi wameangamizwa. Maelezo

11. Ambao wameghafilika katika ujinga. Maelezo

12. Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo? Maelezo

13. Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni. Maelezo

14. Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza. Maelezo

15. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem. Maelezo

16. Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema. Maelezo

17. Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. Maelezo

18. Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira. Maelezo

19. Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba. Maelezo

20. Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini. Maelezo

21. Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni? Maelezo

22. Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa. Maelezo

23. Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema. Maelezo

24. Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa? Maelezo

25. Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni. Maelezo

26. Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona. Maelezo

27. Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli? Maelezo

28. Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu. Maelezo

29. Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa! Maelezo

30. Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua. Maelezo

31. AKASEMA: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa? Maelezo

32. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu, Maelezo

33. Tuwatupie mawe ya udongo, Maelezo

34. Yaliyo tiwa alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka. Maelezo

35. Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini. Maelezo

36. Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu! Maelezo

37. Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu. Maelezo

38. Na katika khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi. Maelezo

39. Lakini alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu! Maelezo

40. Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa. Maelezo

41. Na katika khabari za A'di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi. Maelezo

42. Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka. Maelezo

43. Na katika khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu. Maelezo

44. Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona. Maelezo

45. Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea. Maelezo

46. Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu wapotovu. Maelezo

47. Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua. Maelezo

48. Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi! Maelezo

49. Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie. Maelezo

50. Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake. Maelezo

51. Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake. Maelezo

52. Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu. Maelezo

53. Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi. Maelezo

54. Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi. Maelezo

55. Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini. Maelezo

56. Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi. Maelezo

57. Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe. Maelezo

58. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti. Maelezo

59. Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize. Maelezo

60. Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani