Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

52. SURAT ATT'UR

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanza kwa kiapo cha watano katika bora wa viumbe kuwa adhabu itawateremkia hao wanao kanusha. Kisha ikafikia kusimulia kuwateremkia hiyo adhabu, na namna zake mbali mbali siku ya kufufuliwa na kulipwa. Na ikaingia kutaja mazungumzo juu ya neema za wachamngu na watakayo stareheshwa nayo katika Mabustani ya milele, na namna ya ukarimu watakao upata, na kisha yatakavyo tua macho yao kwa kuwa dhuriya zao watavyo wafuata, na kunyanyuliwa vyeo vyao wawafikie wao. Na baada ya hayo Sura inamuamrisha Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. adumishe kukumbusha bila ya kujali wanayo mzulia makafiri kumpinga yeye, au kushughulika na wayasemayo juu ya Qur'ani tukufu, kwa vile inavyo onyesha kuwa wameshindwa kuleta maneno mfano wa Qur'ani.
Sura hii pia imekashifu maoni yao makafiri ya ufisadi ya kutangaza upotovu wao, na uovu wa kupima kwao. Kisha ikakhitimishia kwa kumuelekea Nabii s.a.w. na kumwambia awaachilie mbali mpaka watakapo ikuta siku yao watapo situshwa, naye akaamrishwa aistahamilie hukumu ya Mola wake Mlezi ya kuwapa muhula hao, kwani hayo hayatamdhuru kitu yeye kwa sababu yumo katika uhifadhi wa Mola wake Mlezi na ulinzi wake. Kadhaalika imemtaka amtakase Mwenyezi Mungu na katika nyakati zote, na katika kila msimamo atakao kuwamo kwa jambo lolote, na usiku zinapo tua nyota.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa mlima wa T'ur, Maelezo

2. Na Kitabu kilicho andikwa Maelezo

3. Katika ngozi iliyo kunjuliwa, Maelezo

4. Na kwa Nyumba iliyo jengwa, Maelezo

5. Na kwa dari iliyo nyanyuliwa, Maelezo

6. Na kwa bahari iliyo jazwa, Maelezo

7. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea. Maelezo

8. Hapana wa kuizuia. Maelezo

9. Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso, Maelezo

10. Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa. Maelezo

11. Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha, Maelezo

12. Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi. Maelezo

13. Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu, Maelezo

14. (Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha! Maelezo

15. Je! Huu ni uchawi, au hamwoni tu? Maelezo

16. Uingieni, mkistahamili au msistahamili - ni mamoja kwenu. Hakika mnalipwa kwa mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

17. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na neema, Maelezo

18. Wakifurahi kwa yale aliyo wapa Mola wao Mlezi. Na Mola wao Mlezi atawalinda na adhabu ya Motoni. Maelezo

19. Kuleni na kunyweni kwa raha kabisa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

20. Watakuwa wameegemea juu ya viti vya enzi vilivyo pangwa kwa safu. Na tutawaoza mahuru-l-aini. Maelezo

21. Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa Imani tutawakutanisha nao dhuriya zao, na wala hatutawapunja hata kidogo katika vitendo vyao. Kila mtu lazima atapata alicho kichuma. Maelezo

22. Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyo penda. Maelezo

23. Watapeana humo bilauri zisio na vinywaji vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi. Maelezo

24. Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza. Maelezo

25. Wataelekeana wakiulizana. Maelezo

26. Waseme: Tulikuwa zamani pamoja na ahali zetu tukiogopa; Maelezo

27. Basi Mwenyezi Mungu akatufanyia hisani na akatulinda na adhabu ya upepo wa Moto. Maelezo

28. Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu. Maelezo

29. Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu. Maelezo

30. Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari. Maelezo

31. Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia. Maelezo

32. Au hizo akili zao ndio zinawaamrisha haya, au wao basi ni watu majeuri tu? Maelezo

33. Au ndio wanasema: Ameitunga hii! Bali basi tu hawaamini! Maelezo

34. Basi nawalete masimulizi kama haya ikiwa wao wanasema kweli. Maelezo

35. Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji? Maelezo

36. Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana na yakini. Maelezo

37. Au wanazo khazina za Mola wako Mlezi au wao ndio wenye madaraka? Maelezo

38. Au wanazo ngazi za kusikilizia? Basi huyo msikilizaji wao na alete hoja ilio wazi! Maelezo

39. Au Yeye Mwenyezi Mungu ana wasichana, na nyinyi ndio mna wavulana? Maelezo

40. Au wewe unawaomba ujira, na kwa hivyo ndio wanaelemewa na uzito wa gharama? Maelezo

41. Au wanayo ilimu ya ghaibu, nao wameandika? Maelezo

42. Au wanataka kufanya vitimbi tu? Lakini hao walio kufuru ndio watakao tegeka. Maelezo

43. Au wanae mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu? Subhanallah! Ametaksika Mwenyezi Mungu na hao wanao washirikisha naye. Maelezo

44. Na hata wange ona pande linatoka mbinguni linaanguka wange sema: Ni mawingu yaliyo bebana. Maelezo

45. Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa. Maelezo

46. Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa. Maelezo

47. Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyengine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui. Maelezo

48. Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi. Kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama, Maelezo

49. Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani