Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

53. SURAT ANNAJM

(Imeteremka Makka)

 

Kiapo mwanzo wa Sura hii kinadhihirisha ukweli wa Mtume s.a.w. katika anayo yasimulia ya khabari za Wahyi (Ufunuo) na anayo yafikisha kutokana na huo ufunuo. Hakupoteza kitu katika hayo wala hakukosea. Na Mtume s.a.w. amesema kweli katika aliyo yazungumzia juu ya safari yake ya kwenda mbinguni, katika hayo yaliyo tokea ya Miiraji, jicho lake halikuhangaika wala halikuruka mpaka.
Kisha Sura inaingia kueleza uchache wa akili za makafiri kwenda kuabudu masanamu waliyo yaunda wenyewe kwa mikono yao, wakayaita majina yao wenyewe, kama walivyo waita Malaika kuwa ati ni wanawake, baada ya kumfanya Mwenyezi Mungu ana mabinti, na wao wenyewe wawe na watoto wa kiume.
Kisha Sura inamtaka Mtume s.a.w. awapuuze, na amwachilie mambo yao Mwenyezi Mungu Mwenye kumiliki na kuumba vyote viliomo mbinguni  na kwenye ardhi. Na Yeye ndiye atakaye mlipa muovu kwa uovu wake, na mwema kwa wema wake. Naye ndiye Mjuzi kabisa wa yote yanayo pita kwa viumbe vyake na hali zao. Yakafwatia hayo kulaumiwa anaye kanya kuhisabiwa kila mtu kwa vitendo vyake, kama yalivyo kwisha pita kwa sharia zilio tangulia, na ikasimuliwa na Vitabu vya Musa na Ibrahim. Na Aya hizi zimethibitisha maana haya yaliyo elezwa katika uwezo na Ishara za Mwenyezi Mungu katika mataifa yaliyo kwisha tangulia.
Kisha Sura inakhitimisha kwa kuweka wazi kwamba Qur'ani ni onyo miongoni mwa maonyo walio onywa kwayo kaumu zilizo kwisha tangulia, ili wapate kutahadhari na Siku ya Kiyama ambayo imekaribia wakati wake. Na Sura inawalaumu makafiri wanao ikataa Qur'ani kwa kughafilika kwao huko, na wakawa wanacheka badala ya kulia na kuwaidhika kwa Qur'ani. Na ikawataka Waumini wamsujudie Mwenyezi Mungu aliye iteremsha na wamuabudu Yeye tu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa nyota inapo tua, Maelezo

2. Mwenzenu huyu hakupotea, wala hakukosea. Maelezo

3. Wala hatamki kwa matamanio. Maelezo

4. Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa; Maelezo

5. Amemfundisha aliye mwingi wa nguvu, Maelezo

6. Mwenye kutua, akatulia, Maelezo

7. Naye yuko juu kabisa upeo wa macho. Maelezo

8. Kisha akakaribia na akateremka. Maelezo

9. Akawa ni kama baina ya mipinde miwili, au karibu zaidi. Maelezo

10. Akamfunulia mja wake (Mwenyezi Mungu) alicho mfunulia. Maelezo

11. Moyo haukusema uwongo uliyo yaona. Maelezo

12. Je! Mnabishana naye kwa aliyo yaona? Maelezo

13. Na akamwona mara nyingine, Maelezo

14. Penye Mkunazi wa mwisho. Maelezo

15. Karibu yake ndiyo ipo Bustani inayo kaliwa. Maelezo

16. Kilipo ufunika huo Mkunazi hicho kilicho ufunuika. Maelezo

17. Jicho halikuhangaika wala halikuruka mpaka. Maelezo

18. Kwa yakini aliona katika Ishara kubwa kabisa za Mola wake Mlezi. Maelezo

19. Je! Mmemuona Lata na Uzza? Maelezo

20. Na Manaat, mwingine wa tatu? Maelezo

21. Je! Nyinyi mnao wana wanaume na Yeye ndio awe na wanawake? Maelezo

22. Huo ni mgawanyo wa dhulma! Maelezo

23. Hayo hayakuwa ila ni majina mliyo wapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuleta uthibitisho wowote juu ya hayo. Hawafuati ila dhana tu na kipendacho nafsi. Na kwa yakini uwongofu ulikwisha wafikia kutoka kwa Mola wao Mlezi. Maelezo

24. Ati mtu anakipata kila anacho kitamani? Maelezo

25. Mwenyezi Mungu tu ndiye Mwenye dunia na Akhera. Maelezo

26. Na wako Malaika wangapi mbinguni, ambao uombezi wao hautafaa chochote isipo kuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia. Maelezo

27. Hakika wasio amini Akhera bila ya shaka wao ndio wanawaita Malaika kwa majina ya kike. Maelezo

28. Nao hawana ujuzi wowote kwa hayo isipo kuwa wanafuata dhana tu. Na dhana haisaidii chochote mbele ya haki. Maelezo

29. Basi mwachilie mbali anaye upa kisogo ukumbusho wetu, na wala hataki ila maisha ya dunia. Maelezo

30. Huo ndio mwisho wao wa ujuzi. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi mwenye kuipotea njia yake, na Yeye ndiye anaye mjua zaidi mwenye kuongoka. Maelezo

31. Ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, ili awalipe walio tenda ubaya kwa waliyo yatenda, na walio tenda mema awalipe mema. Maelezo

32. Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vichafu, isipo kuwa makosa khafifu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mkunjufu wa maghfira, naye anakujueni sana tangu alipo kuumbeni kutoka kwenye ardhi, na mlipo kuwa mimba matumboni mwa mama zenu. Basi msijisifu usafi. Yeye anamjua sana mwenye kujikinga na maovu. Maelezo

33. Je! Umemwona yule aliye geuka? Maelezo

34. Na akatoa kidogo, kisha akajizuia? Maelezo

35. Je! Anayo huyo ilimu ya ghaibu, basi ndio anaona? Maelezo

36. Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa? Maelezo

37. Na vya Ibrahimu aliye timiza ahadi? Maelezo

38. Ya kwamba hakika nafsi iliyo beba madhambi haibebi madhambi ya mwengine? Maelezo

39. Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyo yafanya mwenyewe? Maelezo

40. Na kwamba vitendo vyake vitaonekana? Maelezo

41. Kisha ndio atalipwa malipo yake kwa ukamilifu. Maelezo

42. Na kwamba kwao Mola wako Mlezi ndio mwisho. Maelezo

43. Na kwamba Yeye ndiye anaye leta kicheko na kilio. Maelezo

44. Na kwamba Yeye ndiye anaye fisha na kuhuisha. Maelezo

45. Na kwamba Yeye ndiye aliye umba jozi, dume na jike Maelezo

46. Kutokana na mbegu ya uzazi inapo miminwa. Maelezo

47. Na kwamba ni juu yake ufufuo mwengine. Maelezo

48. Na kwamba ni Yeye ndiye anaye tosheleza na kukinaisha. Maelezo

49. Na kwamba hakika Yeye ndiye Mola Mlezi wa nyota ya Shii'ra. Maelezo

50. Na kwamba Yeye ndiye aliye waangamiza A'di wa kwanza, Maelezo

51. Na Thamudi hakuwabakisha, Maelezo

52. Na kabla yao kaumu ya Nuhu. Na hao hakika walikuwa ni madhaalimu zaidi, na waovu zaidi; Maelezo

53. Na miji iliyo pinduliwa, ni Yeye aliye ipindua. Maelezo

54. Vikaifunika vilivyo funika. Maelezo

55. Basi neema gani ya Mola wako Mlezi unayo ifanyia shaka? Maelezo

56. Hili ni Onyo katika maonyo yale yale ya zamani. Maelezo

57. Kiyama kimekaribia! Maelezo

58. Hapana wa kukifichua isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Maelezo

59. Je! Mnayastaajabia maneno haya? Maelezo

60. Na mnacheka, wala hamlii? Maelezo

61. Nanyi mmeghafilika? Maelezo

62. Basi msujudieni Mwenyezi Mungu, na mumuabudu. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani