Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

55. SURAT ARRAH'MAN

(Imeteremka Madina)

 

Sura hii imeingia kuzihisabu fadhila na neema za Mwenyezi Mungu, kwa kuanzia baada ya kumtaja Arrah'man, Mwingi wa Rehema, kwa kutaja neema yake tukufu kabisa, nayo ni Kufunza Qur'ani Tukufu. Tena Aya zikaendelea kuzieleza hizo neema kwa namna ya kuweka wazi utukufu wa Mwenye kuziumba, aliye tukuka shani yake; na inadhihirisha uweza wake na ufalme wake juu ya wanaadamu na majini katika mbingu na ardhi.
Na inaeleza adhabu za wakosefu na wanao kadhibisha katika Jahannamu, na ikafafanua neema za wachamngu Peponi.
Na Sura ikakhitimisha kwa kumtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kumsifu.
Na Sura imeikariri Aya isemayo "Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha?" mara thalathini na moja, katika mpango wa ki- Qur'ani kukariri kunako pendeza kama inavyo wafikiana na haja. Kila moja katika hizo Aya inawagonga hao wakanushaji kwa kuzikadhibisha kwao neema za Mwenyezi Mungu katika Aya iliyo kabla yake.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Arrah'man, Mwingi wa Rehema Maelezo

2. Amefundisha Qur'ani. Maelezo

3. Amemuumba mwanaadamu, Maelezo

4. Akamfundisha kubaini. Maelezo

5. Jua na mwezi huenda kwa hisabu. Maelezo

6. Na mimea yenye kutambaa, na miti, inanyenyekea. Maelezo

7. Na mbingu ameziinua, na ameweka mizani, Maelezo

8. Ili msidhulumu katika mizani. Maelezo

9. Na wekeni mizani kwa haki, wala msipunje katika mizani. Maelezo

10. Na ardhi ameiweka kwa ajili ya viumbe. Maelezo

11. Humo yamo matunda na mitende yenye mafumba. Maelezo

12. Na nafaka zenye makapi, na rehani. Maelezo

13. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha Maelezo

14. Amemuumba mtu kwa udongo wa kinamo.. Maelezo

15. Na akawaumba majini kwa ulimi wa moto. Maelezo

16. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha Maelezo

17. Mola Mlezi wa mashariki mbili na wa magharibi mbili. Maelezo

18. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

19. Anaziendesha bahari mbili zikutane; Maelezo

20. Baina yao kipo kizuizi, zisiingiliane. Maelezo

21. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

22. Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani. Maelezo

23. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

24. Na ni vyake Yeye hivi viendavyo baharini vilivyo undwa kama vilima. Maelezo

25. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

26. Kila kilioko juu yake kitatoweka. Maelezo

27. Na atabakia Mwenyewe Mola wako Mlezi Mwenye utukufu na ukarimu. Maelezo

28. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

29. Vinamwomba Yeye vilivyomo katika mbingu na ardhi. Kila siku Yeye yumo katika mambo. Maelezo

30. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

31. Tutakuhisabuni enyi makundi mawili. Maelezo

32. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

33. Enyi makundi ya majini na watu! Mkiweza kupenya kwenye mbingu na ardhi, basi penyeni! Hamtapenya ila kwa kupewa madaraka. Maelezo

34. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

35. Mtapelekewa muwako wa moto na shaba; wala hamtashinda. Maelezo

36. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

37. Itakapo pasuka mbingu ikawa nyekundu kama mafuta. Maelezo

38. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

39. Siku hiyo hataulizwa dhambi zake mtu wala jini. Maelezo

40. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

41. Watajuulikana wakosefu kwa alama zao, basi watashikwa kwa nywele zao za utosini na kwa miguu. Maelezo

42. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

43. Hii ndiyo Jahannamu ambayo wakosefu wakiikanusha. Maelezo

44. Watakuwa wakizunguka baina ya hiyo na maji ya moto yanayo chemka. Maelezo

45. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

46. Na mwenye kuogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi atapata Bustani mbili. Maelezo

47. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

48. Bustani zenye matawi yaliyo tanda. Maelezo

49. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

50. Ndani yake zimo chemchem mbili zinazo pita. Maelezo

51. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

52. Humo katika kila matunda zimo namna mbili. Maelezo

53. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

54. Wawe wameegemea matandiko yenye bit'ana ya hariri nzito; na matunda ya Bustani hizo yapo karibu. Maelezo

55. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

56. Humo watakuwamo wanawake watulizao macho yao; hajawagusa mtu kabla yao wala jini. Maelezo

57. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

58. Kama kwamba wao ni yakuti na marijani. Maelezo

59. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha. Maelezo

60. Ati yaweza kuwa malipo ya ihsani ila ihsani? Maelezo

61. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

62. Na zaidi ya hizo zipo Bustani nyengine mbili. Maelezo

63. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

64. Za kijani kibivu. Maelezo

65. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

66. Na chemchem mbili zinazo furika. Maelezo

67. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

68. Imo humo miti ya matunda, na mitende na mikomamanga. Maelezo

69. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

70. Humo wamo wanawake wema wazuri. Maelezo

71. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

72. Wanawake wazuri wanao tawishwa katika makhema. Maelezo

73. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

74. Hajawagusa mtu wala jini kabla yao. Maelezo

75. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

76. Wameegemea juu ya matakia ya kijani na mazulia mazuri. Maelezo

77. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha? Maelezo

78. Limetukuka jina la Mola wako Mlezi Mwenye utukufu na ukarimu.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani