Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

56. SURAT AL-WAAQIA'H

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanzia kwa kusimulia Tukio la Kiyama, na matokeo yatayo ambatana na Tukio hilo. Kisha ikasimulia kuwa viumbe Siku hiyo watakuwa namna tatu. Ikafuatia hayo kwa kufafanua kwa kutosha walio andaliwa kila fungu katika hao, ikiwa ni neema zinazo wafikiana na cheo chao, au ni adhabu inayo nasibiana na ukafiri wao na uasi wao.
Kisha Aya zikaweka wazi baada ya hayo yanayo onekana katika neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na athari za uweza wake katika viumbe, na makulima, na maji, na moto; na yanayo hitajika kutokana na athari hizi kumsabihi Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumtakasa.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Litakapo tukia hilo Tukio Maelezo

2. Hapana cha kukanusha kutukia kwake. Maelezo

3. Literemshalo linyanyualo, Maelezo

4. Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso, Maelezo

5. Na milima itapo sagwasagwa, Maelezo

6. Iwe mavumbi yanayo peperushwa, Maelezo

7. Na nyinyi mtakuwa namna tatu:- Maelezo

8. Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani? Maelezo

9. Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni? Maelezo

10. Na wa mbele watakuwa mbele. Maelezo

11. Hao ndio watakao karibishwa Maelezo

12. Katika Bustani zenye neema. Maelezo

13. Fungu kubwa katika wa mwanzo, Maelezo

14. Na wachache katika wa mwisho. Maelezo

15. Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa. Maelezo

16. Wakiviegemea wakielekeana. Maelezo

17. Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele, Maelezo

18. Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi. Maelezo

19. Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa. Maelezo

20. Na matunda wayapendayo, Maelezo

21. Na nyama za ndege kama wanavyo tamani. Maelezo

22. Na Mahurulaini, Maelezo

23. Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa. Maelezo

24. Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda. Maelezo

25. Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi, Maelezo

26. Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama. Maelezo

27. Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani? Maelezo

28. Katika mikunazi isiyo na miba,

29. Na migomba iliyo pangiliwa, Maelezo

30. Na kivuli kilicho tanda,

31. Na maji yanayo miminika, Maelezo

32. Na matunda mengi, Maelezo

33. Hayatindikii wala hayakatazwi, Maelezo

34. Na matandiko yaliyo nyanyuliwa. Maelezo

35. Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya, Maelezo

36. Na tutawafanya vijana, Maelezo

37. Wanapendana na waume zao, hirimu moja. Maelezo

38. Kwa ajili ya watu wa kuliani. Maelezo

39. Fungu kubwa katika wa mwanzo, Maelezo

40. Na fungu kubwa katika wa mwisho. 3 Maelezo

41. Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni? Maelezo

42. Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka, Maelezo

43. Na kivuli cha moshi mweusi, Maelezo

44. Si cha kuburudisha wala kustarehesha. Maelezo

45. Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa. Maelezo

46. Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa,

47. Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa? Maelezo

48. Au baba zetu wa zamani? Maelezo

49. Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho Maelezo

50. Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu. Maelezo

51. Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha, Maelezo

52. Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu. Maelezo

53. Na kwa mti huo mtajaza matumbo. Maelezo

54. Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka. Maelezo

55. Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu. Maelezo

56. Hiyo ndiyo karamu yao Siku ya Malipo. Maelezo

57. Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki? Maelezo

58. Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza? Maelezo

59. Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji? Maelezo

60. Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi

61. Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua. Maelezo

62. Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki? Maelezo

63. Je! Mnaona makulima mnayo yapanda? Maelezo

64. Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha? Maelezo

65. Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu, Maelezo

66. Mkisema: Hakika sisi tumegharimika; Maelezo

67. Bali sisi tumenyimwa. Maelezo

68. Je! Mnayaona maji mnayo yanywa? Maelezo

69. Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha? Maelezo

70. Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru? Maelezo

71. Je! Mnauona moto mnao uwasha? Maelezo

72. Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji? Maelezo

73. Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani. Maelezo

74. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu. Maelezo

75. Basi naapa kwa maanguko ya nyota, Maelezo

76. Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua! Maelezo

77. Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani Tukufu, Maelezo

78. Katika Kitabu kilicho hifadhiwa. Maelezo

79. Hapana akigusaye ila walio takaswa. Maelezo

80. Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

81. Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza? Maelezo

82. Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha? Maelezo

83. Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo, Maelezo

84. Na nyinyi wakati huo mnatazama! Maelezo

85. Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi. Maelezo

86. Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu, Maelezo

87. Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli? Maelezo

88. Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa, Maelezo

89. Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema. Maelezo

90. Na akiwa katika watu wa upande wa kulia, Maelezo

91. Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia. Maelezo

92. Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu, Maelezo

93. Basi karamu yake ni maji yanayo chemka, Maelezo

94. Na kutiwa Motoni. Maelezo

95. Hakika hii ndiyo haki yenye yakini. Maelezo

96. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani