Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

61. SURAT ASS'AF

(Imeteremka Madina)

 

Sura hii imefunguka kwa kutoa khabari kwamba viliomo katika mbingu na katika ardhi vinamsabihi Mwenyezi Mungu. Na kwamba haiwaelekei Waumini kusema wasiyo yatenda. Na hakika Mwenyezi Mungu anapenda wawe mkono mmoja. Kisha Sura imewashutumu Wana wa Israili kuwa ni wenye inda na ukafiri kwa kauli za Mitume wawili watukufu, nao ni Musa na Isa s.a.w. Na kwamba wao wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuitimiza nuru yake. Na ndani ya hii Sura ipo ahadi ya Mwenyezi Mungu - na ahadi yake ni ya kweli - kuwa ataifanya Dini hii ishinde dini zote nyenginezo, hata walau washirikina wakichukia. Na ikakhitimishia kwa kuhimiza Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa hali na mali, na kuwaahidi wenye kupigana Jihadi, Mujahidina, kupata msamaha na Pepo, na mengineyo wayapendayo Waumini, nayo ni msaada utokao kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi wa karibu. Na wanahimizwa Waumini wawe wenye kumsaidia Mwenyezi Mungu, kama walivyo kuwa wanafunzi wa Isa bin Mariamu. Na kwamba Mwenyezi Mungu atawaunga mkono Waumini kwa msaada wake, na Yeye ni Mwenye kushinda katika kila kitu, Mwenye hikima ya ukomo.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Maelezo

2. Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda? Maelezo

3. Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa mnasema msiyo yatenda. Maelezo

4. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigana katika Njia yake kwa safu kama jengo lilio kamatana. Maelezo

5. Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa nini mnaniudhi, nanyi mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu niliye tumwa kwenu? Walipo potoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu. Maelezo

6. Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri! Maelezo

7. Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu. Maelezo

8. Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia. Maelezo

9. Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki ili ipate kuzishinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia. Maelezo

10. Enyi mlio amini! Nikuonyesheni biashara itakayo kuokoeni na adhabu iliyo chungu? Maelezo

11. Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganeni Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua. Maelezo

12. Atakusameheni dhambi zenu, na atakutieni katika Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za milele. Huko ndio kufuzu kukubwa. Maelezo

13. Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini! Maelezo

14. Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyo sema Isa bin Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu! Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walio amini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani