Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

63. SURAT AL-MUNAAFIQUN

(Imeteremka Madina)

 

Sura hii imekusanya kikundi cha sifa za wanaafiki; ikataja kwamba hao hutangaza imani yao kwa ndimi zao bila ya kuwa wanasema kweli.  Na ikabainisha kwamba wanafanya yamini zao za uwongo kuwa ni kinga wasiambiwe kuwa ni makafiri, ambao kwa hakika ndivyo walivyo na ndivyo watakavyo lipwa hivyo. Pia imebainisha kuwa hao wanaafiki wana umbo zuri la kumpendeza anao waona, na wana ufasihi mzuri wa kusikilizwa. Na juu ya hivyo, nyoyo zao zi tupu, hazina Imani ndani yake. Wao ni kama magogo yaliyo egemezwa, yasiyo na uhai.
Na Sura inaelezea kuwa wakiitwa ili Mtume wa Mwenyezi Mungu awaombee maghfira, hali yao hubainika kwa kuwa hutakabari, na hudhihirisha kukataa kwao kuitikia,  nao wanajivuna.
Kisha Sura ikaingia kutaja madai ya wanaafiki kwamba wao ati ndio watukufu wenye nguvu, na Waumini ni madhalili; na ahadi walio waahidi Waumini kuwa watawatoa mji wakisha rejea Madina. Sura imebainisha wepi katika makundi mawili hayo walio watukufu na wenye nguvu.
Na khatimaye Sura inaelekeza kuwasemeza Waumini watoe kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, wafanye haraka kwa hayo kabla mauti hayajamfikia mmoja wao, akajuta, na akatamani laiti inge akhirishwa ajali yake. Na wala Mwenyezi Mungu hamuakhirishi yeyote ikisha fika ajali yake.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Wanapo kujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo. Maelezo

2. Wamevifanya viapo vyao ni kinga, na wao wakajizuia kuifuata Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika ni mabaya kabisa waliyo kuwa wakiyafanya. Maelezo

3. Hayo ni kwa sababu ya kuwa waliamini, kisha wakakufuru; kwa hivyo umepigwa muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawafahamu lolote. Maelezo

4. Na unapo waona, miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao. Lakini wao ni kama magogo yaliyo egemezwa. Wao hudhania kila ukelele unao pigwa ni kwa ajili yao. Hao ni maadui; tahadhari nao. Mwenyezi Mungu awaangamizilie mbali! Vipi wanapotoka na haki? Maelezo

5. Na wanapo ambiwa: Njooni ili Mtume wa Mwenyezi Mungu akuombeeni maghfira, huvigeuza vichwa vyao, na unawaona wanageuka nao wamejaa kiburi. Maelezo

6. Sawa sawa kwao, ukiwatakia maghfira au hukuwatakia maghfira, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu. Maelezo

7. Hao ndio wanao sema: Msitoe mali kwa ajili ya walioko kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ili waondokelee mbali! Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye khazina za mbingu na ardhi, lakini wanaafiki hawafahamu. Maelezo

8. Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui. Maelezo

9. Enyi mlio amini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio khasiri. Maelezo

10. Na toeni katika tulicho kupeni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti, tena hapo akasema: Mola wangu Mlezi! Huniakhirishi muda kidogo nipate kutoa sadaka, na niwe katika watu wema? Maelezo

11. Wala Mwenyezi Mungu hataiakhirisha nafsi yoyote inapo fika ajali yake; na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani