Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

65. SURAT ATT'ALAAQ

(Imeteremka Madina)

 

Sura hii inaeleza baadhi ya hukumu za talaka, na eda, na namna zake, na hukumu zake - tangu kubaki mwenye eda katika nyumba aliyo pewa talaka ndani yake, na waajibu wa kumtazama kwa matumizi, na maskani. Na kati ya hukumu hizi, kama ilivyo mwendo wa Qur'ani, ipo ahadi kwa mwenye kufuata amri za Mwenyezi Mungu, na onyo kwa mwenye kukiuka mipaka yake. Kisha Sura imeashiria malipo ya wenye kutakabari wakakataa kutimiza amri za Mwenyezi Mungu na Watume wake. Na ikakhitimisha Sura kwa kuwahimiza Waumini wamche Mwenyezi Mungu, na kuwakumbusha neema za kuwapelekea Mtume anaye wasomea Aya za Mwenyezi Mungu, ili awatoe kwenye giza wende kwenye mwangaza, na kwa uweza wake Mwenyezi Mungu kuziumba mbingu saba, na katika ardhi mfano wa hizo.
 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ewe Nabii! Mtakapo wapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Mwenyezi Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya. Maelezo

2. Basi wanapo fikia muda wao, ima warejeeni muwaweke kwa wema, au farikianeni nao kwa wema. Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu. Na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo anavyo agizwa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na anaye mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea. Maelezo

3.Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia. Na anaye mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake. Maelezo

4. Na wale walio sita hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayo shaka, basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, pamoja na ambao hawapati hedhi. Na wenye mimba eda yao mpaka watakapo zaa. Na anaye mcha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi. Maelezo

5. Hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu amekuteremshieni. Na anaye mcha Mwenyezi Mungu atamfutia maovu yake, na atampa ujira mkubwa. Maelezo

6. Wawekeni humo humo mnamo kaa nyinyi kwa kadiri ya pato lenu, wala msiwaletee madhara kwa kuwadhiki. Na wakiwa wana mimba, wagharimieni mpaka wajifungue. Na wakikunyonyesheeni, basi wapeni ujira wao, na shaurianeni kwa wema. Na mkiona uzito kati yenu, basi amnyonyeshee mwanamke mwengine. Maelezo

7. Mwenye wasaa atoe kadiri ya wasaa wake, na mwenye dhiki atoe katika alicho mpa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa kadiri ya alicho mpa. Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji. Maelezo

8. Na miji mingapi iliyo vunja amri ya Mola wake Mlezi na Mitume wake, basi tuliihisabia hisabu ngumu na tukaiadhibu kwa adhabu kali. Maelezo

9. Basi ikauonja ubaya wa mambo yake; na mwisho wa mambo yao ilikuwa khasara. Maelezo

10. Mwenyezi Mungu aliwaandalia adhabu kali. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili, mlio amini! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Ukumbusho, Maelezo

11. Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zinazo bainisha, ili kuwatoa walio amini na wakatenda mema kutoka gizani kuwapeleka kwenye nuru. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na akatenda mema, atamwingiza katika Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Mwenyezi Mungu amekwisha mpa riziki nzuri. Maelezo

12. Mwenyezi Mungu ni yule ambaye ameziumba mbingu saba, na ardhi kwa mfano wa hizo. Amri zake zinashuka baina yao, ili mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu kukijua vilivyo kwa ilimu yake. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani