Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

67. SURAT AL-MULK

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii inaitwa Surat Al-Mulk kwa kutokana na neno Al-Mulk, yaani Ufalme,  linalo tokea katika Aya ya kwanza katika Sura. Na muhimu ya makusudio ya Sura hii tukufu ni kuelekeza fikra na nadhari zizingatie athari ya uweza wa Mwenyezi Mungu ulio zagaa katika nafsi za watu na katika viumbe vya Mwenyezi Mungu mnavyo viona katika ardhi na mbinguni upeo wa macho yenu, ili hayo yawe ndiyo njia ya kupelekea kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na pia Sura hii inabainisha hali ya makafiri ambao watatupwa katika Jahannamu, na watasikilizana mikoromo yao, na wataungua katika Moto wake, na wataungama madhambi yao, na watajuta kwa  watavyo ishia, watapo wauliza Malaika kwa kuto mwitikia Mtume alipo waita na akawahadharisha.
Na ama walio mkhofu Mola wao Mlezi, na wakamuamini, hao watapata maghfira na msamaha kwa makosa yaliyo waporonyoka, na ujira mkubwa kwa mema waliyo yatanguliza na wakayatenda.
 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. AMETUKUKA ambaye mkononi mwake umo Ufalme wote; na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Maelezo

2. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha. Maelezo

3. Aliye umba mbingu saba kwa matabaka. Huoni tafauti yoyote katika uumbaji wa Mwingi wa Rehema. Hebu rudisha nadhari! Unaona kosa lolote? Maelezo

4. Tena rudisha nadhari mara mbili, nadhari yako itakurejea mwenyewe hali ya kuwa imehizika nayo imechoka. Maelezo

5. Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapigia mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa nguvu. Maelezo

6. Na kwa walio mkufuru Mola wao Mlezi ipo adhabu ya Jahannamu. Na ni marejeo maovu yalioje hayo! Maelezo

7. Watakapo tupwa humo watausikia mngurumo wake na huku inafoka. Maelezo

8. Inakaribia kupasuka kwa hasira. Kila mara likitupwa kundi humo walinzi wake huwauliza: Kwani hakukujieni mwonyaji? Maelezo

9. Watasema: Kwani! Ametujia mwonyaji, lakini tulimkadhibisha, na tukasema: Mwenyezi Mungu hakuteremsha chochote. Nyinyi hamumo ila katika upotovu mkubwa! Maelezo

10. Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni! Maelezo

11. Wakakiri dhambi zao. Basi kuangamia ni kwa watu wa Motoni! Maelezo

12. Hakika wanao mwogopa Mola wao Mlezi kwa ghaibu, watapata maghfira na ujira mkubwa. Maelezo

13. Na ficheni kauli zenu, au zitangazeni; hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani. Maelezo

14. Asijue aliye umba, naye ndiye Mjua siri, Mwenye khabari? Maelezo

15. Yeye ndiye aliye idhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa. Maelezo

16. Mnadhani mko salama kwa alioko juu kuwa hatakudidimizeni kwenye ardhi, na tahamaki hiyo inatikisika! Maelezo

17. Au mnadhani mko salama kwa alioko juu ya kuwa Yeye hakupelekeeni kimbunga chenye changarawe? Mtajua vipi maonyo yangu? Maelezo

18. Na bila ya shaka walikwisha kanusha walio kuwa kabla yao; basi kulikuwaje kukasirika kwangu? Maelezo

19. Kwani hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyo zikunjua mbawa zao, na kuzikunja? Hawawashikilii ila Mwingi wa rehema. Hakika Yeye ni Mwenye kuona kila kitu. Maelezo

20. Au ni lipi hilo jeshi lenu la kukunusuruni badala ya Mwingi wa Rehema? Hakika makafiri hawamo ila katika udanganyifu. Maelezo

21. Au ni nani huyo ambaye atakupeni riziki kama Yeye akizuia riziki yake? Bali wao wanakakamia tu katika jeuri na chuki. Maelezo

22. Je! Anaye kwenda akisinukia juu ya uso wake ni mwongofu zaidi, au yule anaye kwenda sawasawa katika Njia Iliyo Nyooka? Maelezo

23. Sema: Yeye ndiye aliye kuumbeni tangu mwanzo, na akakupeni masikio na macho, na nyoyo. Ni kidogo kabisa shukrani zenu. Maelezo

24. Sema: Yeye ndiye aliye kutawanyeni katika ardhi, na kwake mtakusanywa. Maelezo

25. Na wanasema: Lini ahadi hii, ikiwa mnasema kweli? Maelezo

26. Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu; na hakika mimi ni mwonyaji tu mwenye kubainisha. Maelezo

27. Lakini watakapo iona karibu, nyuso za walio kufuru zitahuzunishwa, na itasemwa: Hayo ndiyo mliyo kuwa mkiyaomba. Maelezo

28. Sema: Mwaonaje, ikiwa Mwenyezi Mungu atanihiliki mimi na walio pamoja nami, au akiturehemu, ni nani atakaye walinda makafiri na adhabu chungu? Maelezo

29. Sema: Yeye ndiye Mwingi wa Rehema; tunamuamini Yeye, na juu yake tunategemea. Mtakuja jua ni nani aliye katika upotovu ulio dhaahiri. Maelezo

30. Sema: Mwaonaje, yakiwa maji yenu yamedidimia chini, nani atakueleteeni maji yanayo miminika? Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani