Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

68. SURAT AL-QALAM

(Imeteremka Makka)

 

    Sura hii tukufu imekusanya kumtetea Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. na kuipelekea hima yake na azma yake hata abakie mwenye kushikilia Haki bila ya kumlegezea yeyote, na kushabihisha adhabu iliyo wapata watu wa Makka na adhabu iliyo wapata watu wenye shamba ambao kisa chao kimesimuliwa katika Sura. Na Waumini wanabashiriwa watayo yapata kutoka kwa Mola wao Mlezi; na hapana usawa baina yao na makafiri.  Wanao kadhibisha wanakanywa madai yao wanao jidaia nafsi zao bila ya haki, na wanatiwa khofu kwa kuelezwa hali yao itakavyo kuwa Akhera, na wanatishwa. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. ananasihiwa asubiri na astahamili. Mwishoe Sura inakhitimisha kwa kuitukuza Qur'ani tukufu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo, Maelezo

2. Kwa neema ya Mola wako Mlezi wewe si mwendawazimu. Maelezo

3. Na kwa hakika wewe una malipo yasiyo katika. Maelezo

4. Na hakika wewe una tabia tukufu. Maelezo

5. Karibu utaona, na wao wataona, Maelezo

6. Ni nani kati yenu aliye pandwa na wazimu. Maelezo

7. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye ajuaye zaidi nani aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka. Maelezo

8. Basi usiwat'ii wanao kadhibisha. Maelezo

9. Wanatamani lau unge lainisha ili nao wakulainishie. Maelezo

10. Wala usimt'ii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa, Maelezo

11. Mtapitapi, apitaye akifitini, Maelezo

12. Mwenye kuzuia kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi, Maelezo

13. Mkavu, na juu ya hayo, mshari, amejipachika tu. Maelezo

14. Ati kwa kuwa ana mali na watoto! Maelezo

15. Anapo somewa Aya zetu, husema: Hizi ni simulizi za uwongo za watu wa zamani! Maelezo

16. Tutamtia kovu juu ya pua yake. Maelezo

17. Hakika tumewajaribu hawa kama tulivyo wajaribu wale wenye shamba, walipo apa kwamba watayavuna mazao yake itakapo kuwa asubuhi. Maelezo

18. Wala hawakusema: Mungu akipenda! Maelezo

19. Basi lilitokea tukio juu yake kutoka kwa Mola wako Mlezi, nao wamelala! Maelezo

20. Likawa kama usiku wa giza. Maelezo

21. Asubuhi wakaitana. Maelezo

22. Ya kwamba nendeni kondeni mwenu ikiwa mnataka kuvuna. Maelezo

23. Basi walikwenda na huku wakinong'onezana, Maelezo

24. Ya kuwa leo hata masikini mmoja asikuingilieni. Maelezo

25. Na walikwenda asubuhi, nao wameshikilia azimio hilo. Maelezo

26. Basi walipo liona, wakasema: Hakika tumepotea! Maelezo

27. Bali tumenyimwa! Maelezo

28. Mbora wao akasema: Sikukwambieni, kwa nini hamumtakasi Mwenyezi Mungu? Maelezo

29. Wakasema: Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tulikuwa wenye kudhulumu. Maelezo

30. Basi wakakabiliana kulaumiana wao kwa wao. Maelezo

31. Wakasema: Ole wetu! Tulikuwa tumeikiuka mipaka! Maelezo

32. Asaa Mola wetu Mlezi akatubadilishia lilio bora kuliko hili. Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi. Maelezo

33. Namna hivi yanakuwa mateso, na bila ya shaka mateso ya Akhera ni makubwa zaidi, laiti wangeli jua! Maelezo

34. Hakika wachamngu watakuwa na Bustani za neema kwa Mola wao Mlezi. Maelezo

35. Kwani tutawafanya Waislamu kama wakosefu? Maelezo

36. Mna nini? Mnahukumu vipi? Maelezo

37. Au mnacho kitabu ambacho ndani yake mnasoma? Maelezo

38. Kuwa mtapata humo mnayo yapenda? Maelezo

39. Au mnazo ahadi za viapo juu yetu za kufika Siku ya Kiyama ya kuwa hakika mtapata kila mnayo jihukumia? Maelezo

40. Waulize: Ni nani miongoni mwao dhamini wa haya? Maelezo

41. Au wanao washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wanasema kweli. Maelezo

42. Siku utakapo wekwa wazi mundi, na wataitwa kusujudu, lakini hawataweza, Maelezo

43. Macho yao yatainama chini, fedheha itawafunika. Na hakika walikuwa wakiitwa wasujudu walipo kuwa wazima - Maelezo

44. Basi niache na wanao kadhibisha maneno haya! Tutawavutia kidogo kidogo kwa mahali wasipo pajua. Maelezo

45. Na ninawapururia muhula; hakika hila zangu ni imara. Maelezo

46. Au unawaomba ujira, na wao wanaemewa na gharama hiyo? Maelezo

47. Au iko kwao siri, basi wao wanaiandika? Maelezo

48. Basi ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, wala usiwe kama mmezwa na samaki, alipo nadi naye kazongwa. Maelezo

49. Kama isingeli mfikia neema kutoka kwa Mola wake Mlezi, bila ya shaka angeli tupwa ufukweni naye ni mwenye kulaumiwa. Maelezo

50. Lakini Mola wake Mlezi alimteua na akamfanya miongoni mwa watu wema. Maelezo

51. Na walio kufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao, wanapo sikia mawaidha, na wanasema: Hakika yeye ni mwendawazimu. Maelezo

52. Na hayakuwa haya, ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani