Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

69. SURAT AL-H'AAQQAH

(Imeteremka Makka)

 

 Sura hii tukufu inaeleza hali za Kiyama, na imetaja yaliyo wasibu watu wa mataifa yaliyo tangulia, ya kuteketezwa, na kuchukuliwa kwa nguvu na shida walipo kadhibisha. Na imetaja namna litavyo pulizwa baragumu, na mageuzi na kuondoka yatakayo zisibu ardhi na milima na mbingu. Na yatakayo tokea baada ya hayo ya kuletwa watu kwa ajili ya hisabu, na kubashiriwa watu wa mkono wa kulia kwa malipo ya ukarimu na neema za daima watakazo zipata, na maonyo ya watu wa kushoto na adhabu chungu. Tena Sura ikakhitimisha kwa kutaja ukweli wa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. katika Ujumbe alio ufikisha, na ukweli wa Qur'ani ambao ndio ni Haki iliyo yakini.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Tukio la haki. Maelezo

2. Nini hilo Tukio la haki? Maelezo

3. Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki? Maelezo

4. Thamudi na A'di waliukadhibisha Msiba unao situsha. Maelezo

5. Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno. Maelezo

6. Na ama A'di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika. Maelezo

7. Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani. Maelezo

8. Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki? Maelezo

9. Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia. Maelezo

10. Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu. Maelezo

11. Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina, Maelezo

12. Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi. Maelezo

13. Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu, Maelezo

14. Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja, Maelezo

15. Siku hiyo ndio Tukio litatukia. Maelezo

16. Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa. Maelezo

17. Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi. Maelezo

18. Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yoyote yenu. Maelezo

19. Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu! Maelezo

20. Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu. Maelezo

21. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza, Maelezo

22. Katika Bustani ya juu, Maelezo

23. Matunda yake yakaribu. Maelezo

24. Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita. Maelezo

25. Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu! Maelezo

26. Wala nisingeli jua nini hisabu yangu. Maelezo

27. Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa. Maelezo

28. Mali yangu hayakunifaa kitu. Maelezo

29. Madaraka yangu yamenipotea. Maelezo

30. (Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu! Maelezo

31. Kisha mtupeni Motoni! Maelezo

32. Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini! Maelezo

33. Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Maelezo

34. Wala hahimizi kulisha masikini. Maelezo

35. Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu, Maelezo

36. Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni. Maelezo

37. Chakula hicho hawakili ila wakosefu. Maelezo

38. Basi naapa kwa mnavyo viona, Maelezo

39. Na msivyo viona, Maelezo

40. Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima. Maelezo

41. Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini. Maelezo

42. Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka. Maelezo

43. Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote. Maelezo

44. Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu, Maelezo

45. Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia, Maelezo

46. Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo! Maelezo

47. Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia. Maelezo

48. Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu. Maelezo

49. Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha. Maelezo

50. Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa. Maelezo

51. Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini. Maelezo

52. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani