Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

71. SURAT NUH'

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii tukufu imefafanua kisa cha Nuh'u a.s. pamoja na kaumu yake. Ikasimulia khabari za wito wake kwa dhaahiri, kisha kwa siri na kwa dhaahiri. Na ikaeleza mashtaka yake kumshtakia Mwenyezi Mungu juu ya walivyo mpuuza, na inda walio mfanyia, na ikasajili kukakamia kwao kuyaabudu masanamu mpaka wakastahiki kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu. Nuh'u alipo kata tamaa nao kuukubali wito wake, aliwaapiza wahiliki na waangamie, na akajiombea nafsi yake, na wanawe, Waumini wanaume, na Waumini wanawake, wapate msamaha.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Hakika Sisi tulimtuma Nuh'u kwa watu wake: Uwaonye kaumu yako kabla ya kuwafikia adhabu chungu. Maelezo

2. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika mimi ni mwonyaji wa dhaahiri kwenu, Maelezo

3. Ya kwamba mumuabudu Mwenyezi Mungu, na mumche Yeye, na mumt'ii. Maelezo

4. Atakughufirieni madhambi yenu, na atakuakhirisheni mpaka muda ulio wekwa. Hakika muda wa Mwenyezi Mungu utapo fika haucheleweshwi. Laiti mngejua! Maelezo

5. Akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimewaita watu wangu usiku na mchana, Maelezo

6. Lakini wito wangu haukuwazidisha ila kukimbia. Maelezo

7. Na hakika mimi kila nilipo waita ili upate kuwaghufiria, walijiziba masikio yao kwa vidole vyao, na wakajigubika nguo zao, na wakakamia, na wakatakabari vikubwa mno! Maelezo

8. Tena niliwaita kwa uwazi, Maelezo

9. Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa siri. Maelezo

10. Nikasema: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe. Maelezo

11. Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo. Maelezo

12. Na atakupeni mali na wana, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito. Maelezo

13. Mna nini hamweki heshima ya Mwenyezi Mungu? Maelezo

14. Na hali Yeye kakuumbeni daraja baada ya daraja? Maelezo

15. Kwani hamwoni jinsi Mwenyezi Mungu alivyo ziumba mbingu saba kwa matabaka? Maelezo

16. Na akaufanya mwezi ndani yake uwe nuru, na akalifanya jua kuwa taa? Maelezo

17. Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi kama mimea. Maelezo

18. Kisha atakurudsheni humo na atakutoeni tena. Maelezo

19. Na Mwenyezi Mungu amekukunjulieni ardhi kama busati. Maelezo

20. Ili mtembee humo katika njia zilizo pana. Maelezo

21. Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika hao wameniasi, na wamemfuata yule ambaye mali yake na wanawe hawakumzidishia ila khasara. Maelezo

22. Na wakapanga vitimbi vikubwa. Maelezo

23. Na wakasema: Msiwaache miungu yenu, wala msimwache Wadda wala Suwaa' wala Yaghutha, wala Yau'qa, wala Nasra. Maelezo

24. Na hao walikwisha wapoteza wengi, wala usiwazidishie walio dhulumu ila kupotea. Maelezo

25. Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa wakaingizwa Motoni, wala hawakuwapata wa kuwanusuru badala ya Mwenyezi Mungu. Maelezo

26. Na Nuh'u akasema: Mola wangu Mlezi! Usimwache juu ya ardhi mkaazi wake yeyote katika makafiri! Maelezo

27. Hakika ukiwaacha watawapoteza waja wako, wala wao hawatazaa ila waovu makafiri. Maelezo

28. Mola wangu Mlezi! Nighufirie mimi na wazazi wangu, na kila aliye ingia nyumbani mwangu kuwa ni mwenye kuamini, na Waumini wote wanaume, na Waumini wanawake. Na wala usiwazidishie walio dhulumu ila kupotea. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani