Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

74. SURAT AL-MUDDATHTHIR

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii tukufu inamhimiza Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. awaonye watu wake, na amtukuze Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ayaache yasiyo faa kutokana naye, na imesimulia khabari za kupulizwa barugumu na shida za adhabu zitazo washukia makafiri. Na inamuamrisha Mtume s.a.w. amwachilie mbali anaye pinga fadhila alizo fanyiwa na kisha anatumai bado azidishiwe bila ya kutambua wala shukrani. Na Sura imebainisha vipi kulikuwa kufikiri kwa huyo mwenye kupinga na kuikataa Qur'ani, na ikafafanua vipi itakuwa adhabu yake katika Moto wa Saqar ambao unaelezwa kwa njia ya kutisha na kukhofisha. Na ikataja khabari za nafsi kwa zinavyo chuma kheri au shari, na ikaeleza hali ya watu wa mkono wa kulia na wanavyo wakejeli wakosefu kwa kuwauliza nini kilicho wasukumiza Motoni. Na Sura imekhitimisha kwa kusimulia kuwa Qur'ani ni ya mwenye kutaka kuwaidhika, na wenye kuwaidhika ndio watu wachamngu na ndio wenye kupata msamaha.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ewe uliye jigubika! Maelezo

2. Simama uonye! Maelezo

3. Na Mola wako Mlezi mtukuze! Maelezo

4. Na nguo zako, zisafishe. Maelezo

5. Na yaliyo machafu yahame! Maelezo

6. Wala usitoe kwa kutaraji kuzidishiwa. Maelezo

7. Na kwa ajili ya Mola wako Mlezi, subiri! Maelezo

8. Basi litapo pulizwa barugumu, Maelezo

9. Siku hiyo, basi, itakuwa siku ngumu. Maelezo

10. Kwa makafiri haitakuwa nyepesi. Maelezo

11. Niache peke yangu na niliye muumba; Maelezo

12. Na nikamjaalia awe na mali mengi, Maelezo

13. Na wana wanao onekana, Maelezo

14. Na nikamtgenezea mambo vizuri kabisa. Maelezo

15. Kisha anatumai nimzidishie! Maelezo

16. Hasha! Kwani hakika yeye alikuwa akizifanyia inadi Aya zetu! Maelezo

17. Nitamtesa kwa mateso yasio wezekana. Maelezo

18. Kwani hakika yeye alifikiri na akapima. Maelezo

19. Basi ameangamia! Vipi alivyo pima! Maelezo

20. Tena ameangamia! Vipi alivyo pima! Maelezo

21. Kisha akatazama, Maelezo

22. Kisha akakunja kipaji, na akanuna. Maelezo

23. Kisha akaipa kisogo haki, na akatakabari. Maelezo

24. Na akasema: Haya si chochote ila ni uchawi ulio nukuliwa. Maelezo

25. Haya si chochote ila kauli ya binaadamu. Maelezo

26. Nitakuja mtia kwenye Moto wa Saqar. Maelezo

27. Na nini kitakujuulisha ni nini huo Moto wa Saqar? Maelezo

28. Haubakishi wala hausazi. Maelezo

29. Unababua ngozi iwe nyeusi. Maelezo

30. Juu yake wapo kumi na tisa. Maelezo

31. Na hatukuwafanya walinzi wa Motoni ila ni Malaika, wala hatukuifanya idadi yao hiyo ila kuwatatanisha walio kufuru, wapate kuwa na yakini walio pewa Kitabu, na wazidi Imani wale walio amini, wala wasiwe na shaka walio pewa Kitabu na Waumini, na wapate kusema wenye maradhi katika nyoyo zao na makafiri: Mwenyezi Mungu amekusudia nini kwa mfano huu? Ndio kama hivyo Mwenyezi Mungu humwacha apotee amtakaye, na humwongoa amtakaye. Na hapana yeyote anaye jua majeshi ya Mola wako Mlezi ila Yeye tu. Na haya si chochote ila ni ukumbusho kwa binaadamu. Maelezo

32. Hasha! Naapa kwa mwezi! Maelezo

33. Na kwa usiku unapo kucha! Maelezo

34. Na kwa asubuhi inapo pambazuka! Maelezo

35. Hakika huo Moto ni katika mambo yaliyo makubwa kabisa! Maelezo

36. Ni onyo kwa binaadamu, Maelezo

37. Kwa anaye taka miongoni mwenu kutangulia au kuchelewa. Maelezo

38. Kila nafsi imo rahanini kwa mabaya iliyo yachuma. Maelezo

39. Isipo kuwa watu wa kuliani. Maelezo

40. Hao watakuwa katika Mabustani, wawe wanaulizana Maelezo

41. Khabari za wakosefu: Maelezo

42. Ni nini kilicho kupelekeni Motoni? Maelezo

43. Waseme: Hatukuwa miongoni walio kuwa wakisali. Maelezo

44. Wala hatukuwa tukiwalisha masikini. Maelezo

45. Na tulikuwa tukizama pamoja na walio zama katika maovu. Maelezo

46. Na tulikuwa tukiikanusha siku ya malipo. Maelezo

47. Mpaka yakini ilipo tufikia. Maelezo

48. Basi hautawafaa kitu uombezi wa waombezi. Maelezo

49. Basi wana nini hata wanapuuza onyo hili? Maelezo

50. Kama kwamba wao ni mapunda walio timuliwa, Maelezo

51. Wanao mkimbia simba! Maelezo

52. Ati kila mmoja katika wao anataka apewe nyaraka zilizo funuliwa. Maelezo

53. Hasha! Kwani wao hawaiogopi Akhera? Maelezo

54. Hasha! Kwa hakika huu ni ukumbusho! Maelezo

55. Basi anaye taka atakumbuka. Maelezo

56. Na hawatakumbuka isipo kuwa Mwenyezi Mungu atake. Uchamngu ni kwake Yeye, na msamaha ni wake Yeye. Maelezo   


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani