Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

77. SURAT AL-MURSALAAT

(Imeteremka Makka)

 

Lilio muhimu kabisa katika yaliyo kusanywa na Sura hii tukufu ni maneno yaliyo khusu kufufuliwa, na Kiyama, na dalili za kuthibitisha kuwa kitatokea, na kutishwa kwa waliyo yakataa hayo, na kurudishwa kutishwa huko kwa "Ole wao" mara kumi, na kuwatisha kwa unyonge na adhabu itayo wapata; na kubashiriwa wachamngu kwa starehe na neema watazo zikuta, na mwisho wake masaibu yatayo wapata makafiri wasio iamini Qur'ani.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa zinazo tumwa kwa upole! Maelezo

2. Na zinazo vuma kwa kasi! Maelezo

3. Na zikaeneza maeneo yote! Maelezo

4. Na zinazo farikisha zikatawanya! Maelezo

5. Na zinazo peleka mawaidha! Maelezo

6. Kwa kuudhuru au kuonya, Maelezo

7. Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka yatakuwa! Maelezo

8. Wakati nyota zitakapo futwa, Maelezo

9. Na mbingu zitakapo pasuliwa, Maelezo

10. Na milima itakapo peperushwa, Maelezo

11. Na Mitume watakapo wekewa wakati wao, Maelezo

12. Kwa siku gani hiyo wamewekewa muda huo? Maelezo

13. Kwa siku ya kupambanua! Maelezo

14. Na nini kitakacho kujuulisha siku ya kupambanua ni nini? Maelezo

15. Ole wao, siku hiyo hao wanao kanusha! Maelezo

16. Kwani hatukuwaangamiza walio tangulia? Maelezo

17. Kisha tukawafuatilizia walio fuatia? Maelezo

18. Ndio kama hivi tuwatendavyo wakosefu! Maelezo

19. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! Maelezo

20. Kwani hatukukuumbeni kwa maji ya kudharauliwa? Maelezo

21. Kisha tukayaweka mahali pa utulivu madhubuti? Maelezo

22. Mpaka muda maalumu? Maelezo

23. Tukakadiria na Sisi ni wabora wa kukadiria. Maelezo

24. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! Maelezo

25. Kwani hatukuifanya ardhi yenye kukusanya Maelezo

26. Walio hai na maiti? Maelezo

27. Na ndani yake tukaweka milima mirefu yenye kuthibiti, na tunakunywesheni maji matamu? Maelezo

28. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! Maelezo

29. Nendeni kwenye adhabu mliyo kuwa mkiikanusha! Maelezo

30. Nendeni kwenye kivuli chenye mapande matatu! Maelezo

31. Hakikingi moto, wala hakiwaepushi na mwako. Maelezo

32. Hakika Moto huo unatoa macheche kama majumba! Maelezo

33. Kama kwamba ni ngamia wa rangi ya manjano! Maelezo

34. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! Maelezo

35. Hii ni siku ambayo hawatatamka kitu, Maelezo

36. Wala hawataruhusiwa kutoa udhuru. Maelezo

37. Ole wao siku hiyo hao walio kanusha! Maelezo

38. Hii ndiyo siku ya kupambanua. Tumekukusanyeni nyinyi na walio tangulia. Maelezo

39. Ikiwa mnayo hila, nifanyieni hila Mimi! Maelezo

40. Ole wao siku hiyo hao walio kanusha! Maelezo

41. Hakika wachamngu watakuwa katika vivuli na chemchem, Maelezo

42. Na matunda wanayo yapenda, Maelezo

43. Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda. Maelezo

44. Hakika ndio kama hivyo tunavyo walipa watendao mema. Maelezo

45. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! Maelezo

46. Kuleni na mjifurahishe kidogo tu. Hakika nyinyi ni wakosefu! Maelezo

47. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! Maelezo

48. Na wakiambiwa: Inameni! Hawainami. Maelezo

49. Ole wao siku hiyo hao wanao kanusha! Maelezo

50. Basi maneno gani baada ya haya watayaamini?  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani