Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

78. SURAT ANNABAA

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imethibitisha khabari ya kufufuliwa, na inawahadharisha hao wenye kutilia shaka jambo hilo. Na ikasimamisha hoja na dalili juu ya kuwezekana kwake kwa kuyaeleza yanayo onekana ya kudra ya Mwenyezi Mungu. Na ikatilia mkazo kuwepo kwake, na ikataja baadhi ya alama zake. Kisha ikataja khatima ya wenye kuasi, na khatima ya wachamngu. Na ikamalizikia kwa kuonya na kukhofisha kwa siku hiyo inayo tisha.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. WANAULIZANA nini? Maelezo

2. Ile khabari kuu, Maelezo

3. Ambayo kwayo wanakhitalifiana. Maelezo

4. La! Karibu watakuja jua. Maelezo

5. Tena la! Karibu watakuja jua. Maelezo

6. Kwani hatukuifanya ardhi kama tandiko? Maelezo

7. Na milima kama vigingi? Maelezo

8. Na tukakuumbeni kwa jozi? Maelezo

9. Na tukakufanya kulala kwenu ni mapumziko? Maelezo

10. Na tukaufanya usiku ni nguo? Maelezo

11. Na tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha? Maelezo

12. Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu? Maelezo

13. Na tukaifanya taa yenye mwanga na joto; Maelezo

14. Na tukateremsha maji yanayo anguka kwa kasi kutoka mawinguni, Maelezo

15. Ili tutoe kwayo nafaka na mimea, Maelezo

16. Na mabustani yenye miti iliyo kamatana. Maelezo

17. Hakika siku ya uamuzi imewekewa wakati wake, Maelezo

18. Siku litapo pulizwa barugumu, nanyi mtakuja kwa makundi, Maelezo

19. Na mbingu zitafunguliwa, ziwe milango, Maelezo

20. Na milima itaondolewa na itakuwa kama sarabi. Maelezo

21. Hakika Jahannamu inangojea! Maelezo

22. Kwa walio asi ndio makaazi yao, Maelezo

23. Wakae humo karne baada ya karne, Maelezo

24. Hawataonja humo chochote kibaridi wala kinywaji, Maelezo

25.Ila maji yamoto sana na usaha, Maelezo

26. Ndio jaza muwafaka. Maelezo

27. Hakika hao hawakuwa wakitaraji kuwa kuna hisabu. Maelezo

28. Na wakikanusha Aya zetu kwa nguvu. Maelezo

29. Na kila kitu Sisi tumekidhibiti kwa kukiandika. Maelezo

30. Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu! Maelezo

31. Hakika wachamngu wanastahiki kufuzu, Maelezo

32. Mabustani na mizabibu, Maelezo

33. Na wake walio lingana nao, Maelezo

34. Na bilauri zilizo jaa, Maelezo

35. Hawatasikia humo upuuzi wala uwongo - Maelezo

36. Malipo kutoka kwa Mola wako Mlezi, kipawa cha kutosha. Maelezo

37. Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, Arrahman, Mwingi wa rehema; hawamiliki usemi mbele yake! Maelezo

38. Siku atakapo simama Roho na Malaika kwa safu. Hawatasema ila Mwingi wa rehema aliye mruhusu, na atasema yaliyo sawa tu. Maelezo

39. Hiyo ndiyo Siku ya haki. Basi anaye taka na ashike njia arejee kwa Mola wake Mlezi. Maelezo

40. Hakika tumekuhadharisheni adhabu iliyo karibu kufika; Siku ambayo mtu atakapo ona yaliyo tangulizwa na mikono yake; na kafiri atasema: Laiti ningeli kuwa udongo!  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani