Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

79. SURAT ANNAZIA'AT

(Imeteremka Makka)

 

Imeanza Sura hii kwa kiapo juu ya kumkinika kufufuliwa na kutokea kwake, na ikafuatia hayo hadithi ya Musa na Firauni kumliwaza Mtume s.a.w., na ikataja khabari za binaadamu na juhudi zake, na ikadhihirisha yanayo wangojea majabari, na yanayo wangojea makhaini. Na Sura ikakhitimisha kwa kuuliza kwao washirikina lini itakuwa hiyo Saa ya Kiyama, na ikabainisha kwamba kazi ya Mtume ni kuwaonya wenye kukiogopa Kiyama, sio kujua wakati wake.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa wanao komoa kwa nguvu, Maelezo

2. Na kwa wanao toa kwa upole, Maelezo

3. Na wanao ogelea, Maelezo

4. Wakishindana mbio, Maelezo

5. Wakidabiri mambo. Maelezo

6. Siku kitapo tetemeka cha kutetemeka, Maelezo

7. Kifuate cha kufuatia. Maelezo

8. Siku hiyo nyoyo zitapiga piga, Maelezo

9. Macho yatainama chini. Maelezo

10. Sasa wanasema: Ati kweli tutarudishwa kwenye hali ya kwanza? Maelezo

11. Hata tukiwa mifupa iliyo bunguliwa? Maelezo

12. Wanasema: Basi marejeo hayo ni yenye khasara! Maelezo

13. Kwa hakika hayo ni ukelele mmoja tu, Maelezo

14. Mara watakuwa kwenye uwanda wa mkutano! Maelezo

15. Je! Imekufikia hadithi ya Musa? Maelezo

16. Mola wake Mlezi alipo mwita katika bonde takatifu la T'uwaa, akamwambia: Maelezo

17. Nenda kwa Firauni. Hakika yeye amezidi jeuri. Maelezo

18. Umwambie: Je! Unapenda kujitakasa? Maelezo

19. Nami nitakuongoa ufike kwa Mola wako Mlezi, upate kumcha. Maelezo

20. Basi alimwonyesha Ishara kubwa. Maelezo

21. Lakini aliikadhibisha na akaasi. Maelezo

22. Kisha alirudi nyuma, akaingia kufanya juhudi. Maelezo

23. Akakusanya watu akanadi. Maelezo

24. Akasema: Mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa. Maelezo

25. Basi hapo Mwenyezi Mungu akamshika kumuadhibu kwa la mwisho na la mwanzo. Maelezo

26. Kwa hakika katika haya yapo mazingatio kwa wanao ogopa. Maelezo

27. Je! Ni vigumu zaidi kukuumbeni nyinyi au mbingu? Yeye ndiye aliye ijenga! Maelezo

28. Akainua kimo chake, na akaitengeneza vizuri. Maelezo

29. Na akautia giza usiku wake, na akautokeza mchana wake. Maelezo

30. Na juu ya hivyo ameitandaza ardhi. Maelezo

31. Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake, Maelezo

32. Na milima akaisimamisha, Maelezo

33. Kwa nafuu yenu na mifugo yenu. Maelezo

34. Basi itakapo fika hiyo balaa kubwa, Maelezo

35. Siku ambayo mtu atakumbuka aliyo yafanya, Maelezo

36. Na Jahannamu itadhihirishwa kwa mwenye kuona, Maelezo

37. Basi ama yule aliye zidi ujeuri, Maelezo

38. Na akakhiari maisha ya dunia, Maelezo

39. Kwa hakika Jahannamu ndiyo makaazi yake! Maelezo

40. Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio, Maelezo

41. Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake! Maelezo

42. Wanakuuliza Saa (ya Kiyama) itakuwa lini? Maelezo

43. Una nini wewe hata uitaje? Maelezo

44. Kwa Mola wako Mlezi ndio mwisho wake. Maelezo

45. Kwa hakika wewe ni mwonyaji tu kwa mwenye kuikhofu. Maelezo

46. Ni kama kwamba wao siku watapo iona (hiyo Saa) hawakukaa ila jioni moja tu, au mchana wake.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani