Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

80. SURAT A'BASA

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanza kwa kumlaumu Nabii Muhammad s.a.w. kwa kumpuuza Ibnu Ummi Maktoum alipo mjia kutafuta ilimu na uwongofu. Naye Nabii s.a.w. alikuwa kashughulika kuwalingania Dini baadhi ya mabwana wa Kikureshi kwa kutaraji watamwitikia, ili kwa kusilimu kwao wange silimu watu wengi. Kisha Sura inamkumbusha binaadamu kwa neema alizo pewa na Mwenyezi Mungu tangu kuumbwa kwake mpaka kufufuliwa kwake. Na ikakhitimisha kwa kusimulia khabari za Siku ya Kiyama, ikibainisha kwamba watu siku hiyo ni makundi mawili, kundi la Waumini lenye furaha, na kundi la makafiri wapotovu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Alikunja kipaji na akageuka, Maelezo

2. Kwa sababu alimjia kipofu! Maelezo

3. Na nini kitakujuulisha pengine yeye atatakasika? Maelezo

4. Au atawaidhika, na mawaidha yamfae? Maelezo

5. Ama ajionaye hana haja, Maelezo

6. Wewe ndio unamshughulikia? Maelezo

7. Na si juu yako kama hakutakasika. Maelezo

8. Ama anaye kujia kwa juhudi, Maelezo

9. Naye anaogopa, Maelezo

10. Ndio wewe unampuuza? Maelezo

11. Sivyo hivyo! Huku ni kukumbushana. Maelezo

12. Basi anaye penda akumbuke. Maelezo

13. Yamo katika kurasa zilizo hishimiwa, Maelezo

14. Zilizo inuliwa, zilizo takaswa. Maelezo

15. Zimo mikononi mwa Malaika waandishi, Maelezo

16. Watukufu, wema. Maelezo

17. Ameangamia mwanaadamu! Nini kinacho mkufurisha? Maelezo

18. Kwa kitu gani amemuumba? Maelezo

19. Kwa tone la manii, akamuumba na akamkadiria. Maelezo

20. Kisha akamsahilishia njia. Maelezo

21. Kisha akamfisha, akamtia kaburini. Maelezo

22. Kisha apendapo atamfufua. Maelezo

23. La! Hajamaliza aliyo muamuru. Maelezo

24. Hebu mtu na atazame chakula chake. Maelezo

25. Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu, Maelezo

26. Tena tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu, Maelezo

27. Kisha tukaotesha humo nafaka, Maelezo

28. Na zabibu, na mimea ya majani, Maelezo

29. Na mizaituni, na mitende, Maelezo

30. Na bustani zenye miti iliyo songana baraabara, Maelezo

31. Na matunda, na malisho ya wanyama; Maelezo

32. Kwa manufaa yenu na mifugo yenu. Maelezo

33. Basi utakapo kuja ukelele, Maelezo

34. Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, Maelezo

35. Na mamaye na babaye, Maelezo

36. Na mkewe na wanawe - Maelezo

37. Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha. Maelezo

38. Siku hiyo ziko nyuso zitazo nawiri, Maelezo

39. Zitacheka, zitachangamka; Maelezo

40. Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi, Maelezo

41. Giza totoro litazifunika, Maelezo

42. Hao ndio makafiri watenda maovu.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani