Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

81. SURAT ATTAKWIR

(Imeteremka Makka)

 

Katika Sura hii yanaelezwa yatakayo tokea wakati wa Saa ya Kiyama na baada yake, na yanaelezwa ya kuonyesha dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, na kutilia mkazo cheo cha Qur'ani tukufu, na kupinga madai ya uzushi katika Qur'ani, na kumtakasa Mtume s.a.w. na tuhuma za wazimu, na kuwatisha na kuwaonya hao wanao endelea na upotovu, na inataka yaangaliwe mazingatio yaliyomo katika Qur'ani ambayo yatawafaa watu wenye kusimama msimamo wa sawa, na inarudisha mambo yote ya watu kwenye mapenzi ya Mola Mlezi wa walimwengu wote.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Jua litakapo kunjwa, Maelezo

2. Na nyota zikazimwa, Maelezo

3. Na milima ikaondolewa, Maelezo

4. Na ngamia wenye mimba pevu watakapo achwa wasishughulikiwe, Maelezo

5. Na wanyama wa mwituni wakakusanywa, Maelezo

6. Na bahari zikawaka moto, Maelezo

7. Na nafsi zikaunganishwa, Maelezo

8. Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa, Maelezo

9. Kwa kosa gani aliuliwa? Maelezo

10. Na madaftari yatakapo enezwa, Maelezo

11. Na mbingu itapo tanduliwa, Maelezo

12. Na Jahannamu itapo chochewa, Maelezo

13. Na Pepo ikasogezwa, Maelezo

14. Kila nafsi itajua ilicho kihudhurisha. Maelezo

15. Naapa kwa nyota zinapo rejea nyuma, Maelezo

16. Zinazo kwenda, kisha zikajificha, Maelezo

17. Na kwa usiku unapo pungua, Maelezo

18. Na kwa asubuhi inapo pambazuka, Maelezo

19. Kwamba hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu, Maelezo

20. Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi, Maelezo

21. Anaye t'iiwa, tena muaminifu. Maelezo

22. Na wala huyu mwenzenu hana wazimu. Maelezo

23. Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho ulio safi. Maelezo

24. Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu. Maelezo

25. Wala hii si kauli ya Shetani maluuni. Maelezo

26. Basi mnakwenda wapi? Maelezo

27. Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote. Maelezo

28. Kwa yule miongoni mwenu anaye taka kwenda sawa. Maelezo

29. Wala nyinyi hamtataka isipo kuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani