Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

82. SURAT AL-INFIT'AAR

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeeleza baadhi ya vitisho vya Saa ya Kiyama kwa njia ya kutangaza kuwa hakika litatokea jambo katika siku ambayo kila mtu atajua nini alilo litanguliza na nini alilo liakhirisha. Tena Aya zikaingia kumhadharisha mwanaadamu aliye danganyika na Mola wake Mlezi aliye muumba akamweka sawa, akamjenga kwa namna ya pekee, na kwa umbo bora kabisa. Inathibitisha Sura kuwa huyo mtu anaikadhibisha Siku ya Malipo, na inatilia mkazo kuwepo Malaika juu yake, walinzi mahashumu, waandishi. Na ikamalizia kusema kuwa watu wema watapata neema. Na wapotovu hawatapata ila Jahannamu, watakayo iingia Siku ya Kiyama, siku ambayo nafsi haitoweza kuimilikia nafsi nyengine chochote. Na amri yote itakuwa ni ya Mwenyezi Mungu tu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Mbingu itapo chanika, Maelezo

2. Na nyota zitapo tawanyika, Maelezo

3. Na bahari zitakapo pasuliwa, Maelezo

4. Na makaburi yatapo fukuliwa, Maelezo

5. Hapo kila nafsi itajua ilicho tanguliza, na ilicho bakisha nyuma. Maelezo

6. Ewe mwanaadamu! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu? Maelezo

7. Aliye kuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha, Maelezo

8. Katika sura yoyote aliyo ipenda akakujenga. Maelezo

9. Sivyo hivyo! Bali nyinyi mnaikanusha Siku ya Malipo. Maelezo

10. Na hakika bila ya shaka wapo walinzi juu yenu, Maelezo

11. Waandishi wenye hishima, Maelezo

12. Wanayajua mnayo yatenda. Maelezo

13. Hakika wema bila ya shaka watakuwa katika neema, Maelezo

14. Na hakika waovu bila ya shaka watakuwa Motoni; Maelezo

15. Wataingia humo Siku ya Malipo. Maelezo

16. Na hawatoacha kuwamo humo. Maelezo

17. Na nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani? Maelezo

18. Tena nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani? Maelezo

19. Siku ambayo nafsi haitakuwa na madaraka yoyote juu ya nafsi; na amri yote siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu tu.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani