Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

83. SURAT AL-MUT'AFFIFIIN

(Imeteremka Makka)

 

Imeanzia Sura hii kwa onyo kali kwa huyo anaye jipimia mwenyewe sawa na akampimia mtu mwingine kwa upungufu; na ikaeleza hayo kwa wayatendayo watu katika kutaka watimiziwe haki zao katika vipimo na mizani, na ikaonya mtindo kama huo kwa kuwa ipo Siku ya Hisabu, na ikathibitisha kuwa vitendo vyao vimedhibitiwa katika daftari la hisabu, ambalo halimkadhibishi ila mwenye kupindukia mipaka, mwenye dhambi aliye zuiliwa na rehema za Mola wake Mlezi, na mwisho wake ni Jahannamu.
Tena Aya zikawageukia watu wema, zikawatuza nyoyo kwa vitendo vyao, na zikataja neema zao na alama zao, zikiashiria namna moja wapo katika neema hizo, na kwa ajili ya hizo washindanie wanao shindana. Na Aya zikaeleza walio kuwa wakiyafanya makafiri wakosefu kuwafanyia Waumini wanapo waona, au wanapo kuwa Waumini wanapita mbele yao. Na Sura ikakhitimisha kwa kuwatuliza Waumini kwamba Siku ya Kiyama itawafanyia insafu, wao watakuwa katika neema wakiwacheka makafiri, nao wamekaa juu ya makochi wakiwaangalia, na makafiri watalipwa kwa waliyo kuwa wakiyatenda.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Ole wao hao wapunjao! Maelezo

2. Ambao wanapo jipimia kwa watu hudai watimiziwe. Maelezo

3. Na wao wanapo wapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza. Maelezo

4. Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa Maelezo

5. Katika Siku iliyo kuu, Maelezo

6. Siku watapo msimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote? Maelezo

7. Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin. Maelezo

8. Unajua nini Sijjin? Maelezo

9. Kitabu kilicho andikwa. Maelezo

10. Ole wao siku hiyo kwa wanao kadhibisha! Maelezo

11. Ambao wanaikadhibisha Siku ya Malipo. Maelezo

12. Wala haikadhibishi ila kila mwenye kuruka mipaka, mwenye dhambi. Maelezo

13. Anapo somewa Aya zetu husema: Ni visa vya watu wa kale! Maelezo

14. Hasha! Bali yametia kutu juu ya nyoyo zao hao walio kuwa wakiyachuma. Maelezo

15. Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi. Maelezo

16. Kisha wataingia Motoni! Maelezo

17. Kisha waambiwe: Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyakadhabisha. Maelezo

18. Hasha! Hakika maandiko ya watu wema bila ya shaka yamo katika I'liyyin. Maelezo

19. Na nini kitakacho kujuvya nini I'liyyin? Maelezo

20. Kitabu kilicho andikwa. Maelezo

21. Wanakishuhudia walio karibishwa. Maelezo

22. Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema. Maelezo

23. Wakae juu ya viti vya enzi wakiangalia. Maelezo

24. Utatambua katika nyuso zao mng'aro wa neema, Maelezo

25. Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri, Maelezo

26. Muhuri wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana. Maelezo

27. Na mchanganyiko wake ni Tasniim, Maelezo

28. Chemchem watakayo inywa walio kurubishwa. Maelezo

29. Kwa hakika wale walio kuwa wakosefu walikuwa wakiwacheka walio amini. Maelezo

30. Na wanapo pita karibu yao wakikonyezana. Maelezo

31. Na wanapo rudi kwa watu wao hurudi nao wamefurahi. Maelezo

32. Na wanapo waona husema: Hakika hawa ndio khasa walio potea. Maelezo

33. Na wao hawakutumwa wawe walinzi juu yao. Maelezo

34. Basi leo walio amini ndio watawacheka makafiri, Maelezo

35. Nao wako juu ya viti vya enzi wakiangalia. Maelezo

36. Je! makafiri wamelipwa malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda?  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani