Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

86. SURAT ATT'AARIQ

(Imeteremka Makka)

 

Sura hii imeanzia kwa kiapo cha kuashiria dalili za kudra ya Mwenyezi Mungu, na inatilia mkazo kuwa kila nafsi ina mlinzi wake na muangalizi, na inamtaka mtu ajifikirie kuumbwa kwake, na ya kwamba yeye kaumbwa na maji yenye kutoka kwa kasi, ili ipatikane hoja kwamba Mwenye kuumba hivi ni Mweza wa kumrejeza tena baada ya kufa kwake.Tena ikaapa mara ya pili kwamba Qur'ani ni kauli ya kufafanua wala si maneno ya maskhara. Na juu ya kuwa hivyo makafiri bila ya shaka wameshughulika kuikanya na kuipangia njama. Na Mwenyezi Mungu amezirudi njama zao kwa njama kali kuliko zao. Kisha Sura imekhitimisha kwa kutaka wapewe muhula makafiri.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa mbingu na Kinacho kuja usiku! Maelezo

2. Na nini kitakacho kujuulisha ni nini hicho Kinacho kuja usiku? Maelezo

3. Ni Nyota yenye mwanga mkali. Maelezo

4. Hapana nafsi ila inayo mwangalizi. Maelezo

5. Hebu naajitazame mwanaadamu ameumbwa kwa kitu gani? Maelezo

6. Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa, Maelezo

7. Yatokayo baina ya mifupa ya mgongo na mbavu. Maelezo

8. Hakika Yeye ana uweza wa kumrudisha. Maelezo

9. Siku zitakapo dhihirishwa siri. Maelezo

10. Basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi. Maelezo

11. Naapa kwa mbingu yenye marejeo! Maelezo

12. Na kwa ardhi inayo pasuka! Maelezo

13. Hakika hii ni kauli ya kupambanua. Maelezo

14. Wala si mzaha. Maelezo

15. Hakika wao wanapanga mpango. Maelezo

16. Na Mimi napanga mpango. Maelezo

17. Basi wape muhula makafiri - wape muhula pole pole.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani