Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

88. SURAT AL-GHAASHIYAH

(Imeteremka Makka)

 

Imeanza Sura hii kwa njia ya kutia shauku kuisikiliza hadithi ya Siku ya Kiyama, na hayo mambo yatakayo tokea humo. Inaashiria kwamba watu ni makundi mawili: miongoni mwao wapo ambao hawatapata hishima yoyote kwa watakavyo pokewa na wataingia kwenye Moto mkali. Na wapo watakao ifikia siku hiyo kwa furaha kwa namna ya rehema na radhi zilizo andaliwa kwa ajili yao. Kisha Sura ikaeleza dalili zilizo wazi za uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kufufua kutokana na wanavyo ona wenyewe kwa macho yao na wanayo nafiika kwayo katika uhai wao. Na baada ya kuzitaja dalili hizi ikageukia khabari za Mtume s.a.w. kwa kukumbusha kwamba waajibu wake mkubwa kwa mintarafu yao ni wazi, ya kwamba yeye hakutawalishwa juu yao awalazimishe kuamini, na kwamba mwenye kugeuka na akakufuru baada ya waadhi huu ni Mwenyezi Mungu ndiye atakaye mshika kwa dhambi zake, na atamuadhibu kwa adhabu kubwa kabisa, atapo rejea kwake baada ya kufa, kwani marejeo ya wote na kuhisabiwa kwao wote ni kwake Yeye Mwenyezi Mungu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Je! Imekufikia khabari ya msiba wa kufudikiza? Maelezo

2. Siku hiyo nyuso zitainama, Maelezo

3. Zikifanya kazi, nazo taabani. Maelezo

4. Ziingie katika Moto unao waka - Maelezo

5. Zikinyweshwa kutoka chemchem inayo chemka. Maelezo

6. Hawatakuwa na chakula isipo kuwa kichungu chenye miba. Maelezo

7. Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa. Maelezo

8. Siku hiyo nyuso nyengine zitakuwa kunjufu. Maelezo

9. Zitakuwa radhi kwa juhudi yao, Maelezo

10. Katika Bustani ya juu. Maelezo

11. Hawatasikia humo upuuzi. Maelezo

12. Humo imo chemchem inayo miminika. Maelezo

13. Humo vimo viti vilivyo nyanyuliwa, Maelezo

14. Na bilauri zilizo pangwa, Maelezo

15. Na matakia safu safu, Maelezo

16. Na mazulia yaliyo tandikwa. Maelezo

17. Je! Hawamtazami ngamia jinsi alivyo umbwa? Maelezo

18. Na mbingu jinsi ilivyo inuliwa? Maelezo

19. Na milima jinsi ilivyo thibitishwa? Maelezo

20. Na ardhi jinsi ilivyo tandazwa? Maelezo

21. Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji. Maelezo

22. Wewe si mwenye kuwatawalia. Maelezo

23. Lakini anaye rudi nyuma na kukataa, Maelezo

24. Basi Mwenyezi Mungu atamuadhibu kwa adhabu iliyo kubwa kabisa! Maelezo

25. Hakika ni kwetu Sisi ndio marejeo yao. Maelezo

26. Kisha hakika ni juu yetu Sisi hisabu yao!  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani