Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

89. SURAT AL-FAJR

(Imeteremka Makka)

 

Imeanza Sura hii kwa viapo vya mambo yanayo onekana namna mbali mbali, yanayo pelekea kuangalia athari ya kudra kwamba wanao mkanya Mwenyezi Mungu na kukanya kufufuliwa watakuja adhibiwa, kama walivyo kwisha adhibiwa walio kadhibisha kabla yao. Na Sura ikaingia kuthibitisha mwendo wa Mwenyezi Mungu wa kuwajaribu waja wake kwa kheri na shari, na kwamba kupa kwake na kunyima kwake sio dalili ya kuridhika kwake au kukasirika kwake. Tena mazungumzo yakawaelekea wanao semezwa ya kwamba hali zao zinafichua wingi wa pupa yao na choyo chao. Kisha inakhitimisha kwa kuashiria majuto ya wanao pindukia kiasi na kutamani kwao kwamba laiti wangeli tanguliza mema ya kuwaokoa na hayo wanayo teseka nayo ya vitisho vya Siku ya Kiyama, na yanayo kuwa ya kuiliwaza nafsi iliyo tua iliyo tanguliza mema wala isikiuke mipaka, na itavyo itwa iingie pamoja na walio kirimiwa miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu katika Pepo ya Mwenyezi Mungu.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa alfajiri, Maelezo

2. Na kwa masiku kumi, Maelezo

3. Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja, Maelezo

4. Na kwa usiku unapo pita, Maelezo

5. Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili? Maelezo

6. Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A'di? Maelezo

7. Wa Iram, wenye majumba marefu? Maelezo

8. Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi? Maelezo

9. Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni? Maelezo

10. Na Firauni mwenye vigingi? Maelezo

11. Ambao walifanya jeuri katika nchi? Maelezo

12. Wakakithirisha humo ufisadi? Maelezo

13. Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu. Maelezo

14. Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia. Maelezo

15. Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu! Maelezo

16. Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge! Maelezo

17. Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima, Maelezo

18. Wala hamhimizani kulisha masikini; Maelezo

19. Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa, Maelezo

20. Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi. Maelezo

21. Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande, Maelezo

22. Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu, Maelezo

23. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini? Maelezo

24. Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu! Maelezo

25. Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake. Maelezo

26. Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake. Maelezo

27. Ewe nafsi iliyo tua! Maelezo

28. Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha. Maelezo

29. Basi ingia miongoni mwa waja wangu, Maelezo

30. Na ingia katika Pepo yangu.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani