Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

91. SURAT ASH-SHAMS

(Imeteremka Makka)

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameapa kuanzia Sura hii kwa vitu kadhaa wa kadhaa miongoni mwa viumbe vyake vitukufu, vyenye kueleza utimilivu wa uweza wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na Upweke wake, juu ya kufuzu kwa mwenye kuisafisha nafsi yake kwa Imani na ut'iifu, na kukhasiri kwa kupinga mwenye kuidhoofisha kwa ukafiri na maasi. Kisha ikaingilia mfano wa Thamudi, kaumu ya Saleh, na yaliyo wafika hao, ili apate kuzingatia kila mwenye inda mwenye kukadhibisha. Kwani hakika wao walipo mkadhibisha Mtume wao, na wakamuuwa yule ngamia, Mwenyezi Mungu aliwaangamiza wote, na Yeye hakhofu matokeo ya kuwaangamiza hao, na aliyo wateremshia, kwani Yeye hasailiwi kwa anayo yatenda, na hakika amewateremshia wanayo stahiki.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa jua na mwangaza wake! Maelezo

2. Na kwa mwezi unapo lifuatia! Maelezo

3. Na kwa mchana unapo lidhihirisha! Maelezo

4. Na kwa usiku unapo lifunika! Maelezo

5. Na kwa mbingu na kwa aliye ijenga! Maelezo

6. Na kwa ardhi na kwa aliye itandaza! Maelezo

7. Na kwa nafsi na kwa aliye itengeneza! Maelezo

8. Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake, Maelezo

9. Hakika amefanikiwa aliye itakasa, Maelezo

10. Na hakika amekhasiri aliye iviza. Maelezo

11. Kina Thamudi walikadhibisha kwa sababu ya upotofu wao, Maelezo

12. Alipo simama mwovu wao mkubwa, Maelezo

13. Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipo waambia: Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, mwacheni anywe maji fungu lake. Maelezo

14. Lakini walimkadhibisha na wakamchinja ngamia, kwa hivyo Mola wao Mlezi aliwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akawafuta kabisa. Maelezo

15. Wala Yeye haogopi matokeo yake.  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani