Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

92. SURAT AL-LAYL

(Imeteremka Makka)

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameapa kwa viapo vitatu juu ya kuwa vitendo vya watu vinakhitalifiana, baadhi yake ni vya uwongofu, na baadhi yake ni vya upotofu. Mwenye kutoa, na akamchamngu, na akawafiki tabia yenye kukusanya kheri, basi Mwenyezi Mungu atamsahilishia mambo yake kwa wepesi. Na mwenye kufanya ubakhili, na akajiona hana haja na mtu, na akakanusha tabia zenye kukusanya kheri Mwenyezi Mungu atamfanyia wepesi kuingia mashakani.  Na wala mali yake hayatamfaa kitu kumwokoa akitumbukia katika adhabu! Na Aya zikabainisha baada ya hayo kwamba hakika Mwenyezi Mungu amechukua jukumu kubainisha njia za uwongofu kwa fadhila zake, na kwake yapo mambo ya maisha mawili, ya Akhera na ya duniani. Na kwamba hakika Yeye amekwisha onya kwamba Moto watauingia waovu na watauepuka walio wema.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa usiku unapo funika! Maelezo

2. Na mchana unapo dhihiri! Maelezo

3. Na kwa Aliye umba dume na jike! Maelezo

4. Hakika juhudi zenu bila ya shaka ni mbali mbali. Maelezo

5. Ama mwenye kutoa na akamchamngu, Maelezo

6. Na akaliwafiki lilio jema, Maelezo

7. Tutamsahilishia yawe mepesi. Maelezo

8. Na ama mwenye kufanya ubakhili, na asiwe na haja ya wenzake, Maelezo

9. Na akakanusha lilio jema, Maelezo

10. Tutamsahilishia yawe mazito! Maelezo

11. Na mali yake yatamfaa nini atapo kuwa anadidimia? Maelezo

12. Hakika ni juu yetu kuonyesha uwongofu. Maelezo

13. Na hakika ni yetu Sisi Akhera na dunia. Maelezo

14. Basi nakuonyeni na Moto unao waka! Maelezo

15. Hatauingia ila mwovu kabisa! Maelezo

16. Anaye kadhibisha na kupa mgongo. Maelezo

17. Na mchamngu ataepushwa nao, Maelezo

18. Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa. Maelezo

19. Na wala si kwa kuwa yupo yeyote aliye mfanyia hisani ndio anamlipa. Maelezo

20. Ila ni kutaka radhi ya Mola wake Mlezi aliye juu kabisa. Maelezo

21. Naye atakuja ridhika!  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani