Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

95. SURAT AT-TIN

(Imeteremka Makka)

 

Mwenyezi Mungu anaapa katika Sura hii kwa matunda mawili yenye baraka, na pahala pawili pazuri, ya kwamba Yeye hakika amemuumba mtu kwa njia kunjufu kabisa, kwa kumkamilishia akili, na uwezo wa kutaka na kutotaka, na mengineyo katika sifa za ukamilifu. Kisha Aya zikataja kuwa mtu hakusimama kwa mujibu wa alivyo umbiwa, bali akateremka kwa daraja mpaka akawa wa chini kabisa, isipo kuwa walio amini na wakatenda mema kati yao. Hao Mwenyezi Mungu amewakunjulia vipawa.  Kisha Sura imewageukia kuwakemea wanao kadhibisha kufufuliwa baada ya kudhihiri dalili zote za uweza wa Mwenyezi Mungu na khabari za hikima yake.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa tini na zaituni! Maelezo

2. Na kwa Mlima wa Sinai! Maelezo

3. Na kwa mji huu wenye amani! Maelezo

4. Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa. Maelezo

5. Kisha tukamrudisha kuwa chini kuliko walio chini! Maelezo

6. Lakini wale walio amini na wakatenda mema, hao watapata ujira usio kwisha. Maelezo

7. Basi ni kipi baadaye kitacho kukukadhibishia malipo? Maelezo

8. Kwani Mwenyezi Mungu si muadilifu kuliko mahakimu wote?  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani