Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

96. SURAT AL-A'LAQ

(Imeteremka Makka)

 

Katika Sura hii upo wito wa kusoma na kujifunza, na kwamba aliye weza kumuumba mtu kutokana na asli nyonge ni Mweza wa kumfunza kuandika kwa kudhibitia ilimu na kutimizia kufahamu, na amfunze aliyo kuwa hayajui. Kwani Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kummiminia ilimu mwanaadamu. Na Sura  inanabihisha kwamba utajiri na nguvu huenda zikampelekea mtu kupindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu, lakini marejeo ya wote ni kwa Mwenyezi Mungu mwishoni. Na mazungumzo yanamwelekea kila mwenye kusilihi kusemezwa kuwaonya hao majeuri wanao pinga kheri, kuwaonya kuwa watakuja kushikwa kwa nywele zao za utosi wakibururwa Motoni; na hawatofaliwa na wasaidizi wowote. Na Sura inakhitimisha kwa kuwataka wasikivu wende kinyume na hao wenye inda wanao kadhibisha, na wajijongeze kwa ut'iifu kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Maelezo

2. Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Maelezo

3. Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Maelezo

4. Ambaye amefundisha kwa kalamu. Maelezo

5. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui. Maelezo

6. Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri Maelezo

7. Akijiona katajirika. Maelezo

8. Hakika kwa Mola wako Mlezi ndio marejeo. Maelezo

9. Umemwona yule anaye mkataza Maelezo

10. Mja anapo sali? Maelezo

11. Umeona kama yeye yuko juu ya uwongofu? Maelezo

12. Au anaamrisha uchamngu? Maelezo

13. Umeona kama yeye akikanusha na anarudi nyuma? Maelezo

14. Hajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anaona? Maelezo

15. Kwani! Kama haachi, tutamkokota kwa shungi la nywele! Maelezo

16. Shungi la uwongo, lenye makosa! Maelezo

17. Basi na awaite wenzake! Maelezo

18. Nasi tutawaita Mazabania! Maelezo

19. Hasha! Usimt'ii! Nawe sujudu na ujongee!  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani