Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

98. SURAT AL-BAYYINAH

(Imeteremka Madina)

 

Watu wa Kitabu, yaaani Mayahudi na Wakristo, wamejua kutokana na Vitabu vyao, na¬  washirikina wa Makka wakajua kutokana nao sifa za Nabii wa zama za mwisho. Na yalikuwa yanatakikana kutokana na hayo ni kuwa wamuamini huyo Nabii pindi akiteuliwa. Lakini alipo teuliwa miongoni mwao Mtume wa Mwenyezi Mungu mwenye kuungwa mkono na Qur'ani, walikhitalifiana na wakaacha ahadi yao. Na vitendo vya Watu wa Kitabu katika hayo vilikuwa viovu zaidi kuliko vya washirikina. Na hukumu ya watu hawa wote Akhera ni kukaa milele katika Moto. Na Waumini, watu wa vyeo vya juu kwa fadhila, ndio bora wa viumbe. Malipo yao ni kukaa milele Peponi, na kuridhika kwa kuyapata wayatakayo na kupewa wanayo yapenda. Hii ndiyo neema ya mwenye kumkhofu Mola wake Mlezi.

 


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Hawakuwa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina waache walio nayo mpaka iwajie bayana, Maelezo

2. Yaani Mtume aliye toka kwa Mwenyezi Mungu anaye wasomea kurasa zilizo takasika, Maelezo

3. Ndani yake mna maandiko yaliyo nyooka. Maelezo

4. Wala hawakufarikiana walio pewa Kitabu ila baada ya kuwajia hiyo bayana. Maelezo

5. Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Sala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti. Maelezo

6. Hakika walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina wataingia katika Moto wa Jahannamu wadumu milele humo. Hao ndio viumbe waovu kabisa. Maelezo

7. Hakika walio amini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe. Maelezo

8. Malipo yao kwa Mola wao Mlezi ni Bustani za daima, zipitazo mito kati yake. Wakae humo milele. Mwenyezi Mungu yu radhi nao, na wao waradhi naye. Hayo ni kwa anaye mwogopa Mola wake Mlezi.¬  Maelezo ¬ 


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright © 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani