Qur'ani Tukufu

Tarjuma ya Qur'ani Tukufu Kwa Kiswahili

Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani (Nani Yeye?)

 

100. SURAT AL-A'ADIYAAT

(Imeteremka Makka)

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu ameapa katika kifungulio cha Sura hii kwa farasi wa Jihadi, kwamba hakika mwanaadamu bila ya shaka ni mwingi wa kuikufuru neema ya Mola wake Mlezi. Na kwamba juu ya hivyo katika Akhera bila ya shaka atakuwa ni shahidi dhidi ya nafsi yake kwa aliyo kuwa nayo. Na kwamba bila ya shaka yeye kwa kuyapenda mali ni bakhili na mwenye choyo juu yake. Na khatimaye ametaja khabari za kufufuliwa, na akazindua kuwa ipo hisabu na malipo.


KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

1. Naapa kwa farasi wendao mbio wakipumua, Maelezo

2. Na wakitoa moto kwa kupiga kwato zao chini, Maelezo

3. Wakishambulia wakati wa asubuhi, Maelezo

4. Huku wakitimua vumbi, Maelezo

5. Na wakijitoma kati ya kundi, Maelezo

6. Hakika mwanaadamu ni mtovu wa fadhila kwa Mola wake Mlezi! Maelezo

7. Na hakika yeye mwenyewe bila ya shaka ni shahidi wa hayo! Maelezo

8. Naye hakika bila ya shaka ana nguvu za kupenda mali! Maelezo

9. Kwani hajui watakapo fufuliwa waliomo makaburini? Maelezo

10. Na yakakusanywa yaliomo vifuani? Maelezo

11. Kuwa hakika Mola wao Mlezi siku hiyo bila ya shaka atakuwa na khabari zao wote!  Maelezo  


Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejea uliko toka

Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii qurani-tukufu@geocities.com

Copyright 22 August 1997, Sheikh Ali Muhsin Al Barwani